ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 21, 2011

Mmiliki wa Dowans azua jambo

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), ambalo liliamuliwa na Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), kuilipa Kampuni ya Dowans Tanzania Limited Sh bilioni 94, limeguswa na ujio wa mfanyabiashara anayedaiwa kumiliki kampuni hiyo, Brigedia mstaafu Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi. 

Al Adawi ambaye pia anamiliki Kampuni ya Dowans Holdings SA, yuko nchini na juzi alikutana na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari Dar es Salaam hasa magazeti, na kuzungumzia sakata linalohusisha kampuni yake ambalo limegusa hisia za watu wengi nchini kwa miaka kadhaa sasa. 


Lakini katika ufafanuzi wake kwa mambo kadhaa kuhusu Dowans Tanzania Limited ikiwamo malipo hayo ya fidia ya Sh bilioni 94, mfanyabiashara huyo raia wa Oman, alisema yuko tayari kufuta kiasi cha deni hilo, lakini mitambo yake iachwe izalishe umeme kwa sababu ni mipya, lakini pia umeme wake ni wa bei nafuu. 

Kwa msingi huo, Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud alipoulizwa jana kuhusu kuja kwa mmiliki huyo wa Dowans na kama wamezungumza naye, Masoud alijibu kwa kifupi, “najua unachotaka kuniuliza. Tutatoa taarifa rasmi kesho (leo).” 

Hata alipoulizwa kama Tanesco wameshakutana na mmiliki huyo ambaye alisema moja ya sababu za ziara yake ni kujua kama kuna uwezekano wa kufikiwa makubaliano juu ya mambo yaliyopo kwa sasa, Msemaji huyo wa Tanesco, alisisitiza kwamba taarifa rasmi itatolewa leo. 

Al Adawi katika mkutano wake huo na wahariri, alisema yeye ndiye mmiliki wa kampuni hizo mbili na kwamba aliteua rafiki yake wa siku nyingi, mfanyabiashara na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM), kufanya kazi zake nchini na kumpa nguvu kisheria ya kufanya hivyo. 

Alisema aliombwa na Rostam kuja kuwekeza nchini mwaka 2006, baada ya kutokea matatizo ya umeme Tanzania; na kama alikuwa tayari kuwekeza na kwa msingi huo, alikubali mwito huo. 

Aidha, katika mkutano huo na wahariri juzi, mfanyabiashara huyo inaelezwa kuwa alishangazwa na watu wanaoiponda kampuni yake na kudai ni feki, akisema inawezekanaje kwa kampuni feki kuwekeza mitambo yenye thamani ya dola za Marekani milioni 109 nchini. 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba alipoulizwa jana kuhusu kuja kwa mfanyabiashara huyo na kama wanafahamu lolote lililofikiwa kati yake na Tanesco, alisema taarifa hizo amezisoma katika vyombo vya habari, 

“Nimesoma taarifa zake katika vyombo vya habari. Na amesema amewaandikia Tanesco. Lakini kesho (leo) tuna kikao na watu wa Wizara (Nishati na Madini), kwa hiyo tutaliulizia suala hili. Na keshokutwa (kesho) tunakutana na Tanesco, kwa hiyo yote tutayafahamu,” alisema mbunge huyo wa Bumbuli. 

Suala la Dowans limegusa hisia za watu wengi nchini na katika siku za karibuni, hukumu ya ICC inayoitaka Tanesco kulipa fidia hiyo ya Sh bilioni 94; hatua ambayo imepingwa na Watanzania wengi, lakini wapo wanaotaka mitambo yake iwashwe sasa kukabili tatizo kubwa la mgawo wa umeme nchini.


CHANZO:HABARI LEO

No comments: