.jpg)
Kashfa ya rushwa katika ununuzi wa Rada ambayo inamwandama Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, imezidi kumyima usingizi mwanasiasa huyo maarufu kama ‘mzee wa vijisenti’ na sasa ameibuka na kudai kwamba yeye ni mtu mwadilifu na msafi.
Chenge alitoa kauli hiyo ya kujisafisha jana jijini Dar es Salaam, huku akisisitiza kwamba asiulizwe swali lolote na waandishi wa habari.
"Kwa leo sitataka mniulize swali lolote baada ya kusema haya nitakayoyasema kwa kuwa taarifa kamili mtagawiwa ili muisome wenyewe," alitahadharisha Chenge na kisha akaanza kuisoma.
Alisema Kitengo cha Kuchunguza Makosa Makubwa Nchini Uingereza (SFO), pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa hapa Nchini (Takukuru) wamekamilisha uchunguzi wao na hakuna sehemu yoyote ambapo alitajwa kuwa alipokea fedha kama rushwa wakati wa ununuzi wa Rada hiyo.
Alisema anamshukuru Mungu kwamba uchunguzi huo umekamilika na hakuna sehemu yeyote aliyotajwa kama alipokea rushwa kwenye ununuzi wa Rada hiyo ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
"Mimi ni mwadilifu, nimefanya kazi katika awamu zote nne za uongozi wa nchi yetu hata nilipojiuzulu uwaziri sikuwa na hofu wala mashaka ya kupoteza kazi," alisema serikali
Wakati wa ununuzi wa Rada hiyo, Chenge alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambapo mikataba yote ya serikali ilikuwa lazima aione.
Mbunge huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria,alisema siku zote alikuwa akiamini kwamba ipo siku suala hilo la uchunguzi wa kashfa ya Rada lingefika mwisho na ukweli ungeonekana na uongo ukajitenga.
"Mimi siku zote nasema mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni na mimi ndugu zangu watanzania kwa hili haki yangu nipeni vyombo vyote wiwili vilivyofanya uchunguzi mimi sikuhusishwa kwa namna yoyote," alisema Chenge
Alisema matokeo ya uchunguzi yameonyesha ununuzi wa Rada hiyo kutoka kampuni ya BAE ya nchini Uingereza ulifanyika kwa kufuata sheria zote za nchi.
Mwaka 1,999 mkataba wa ununuzi wa Rada ulisainiwa kati ya Serikali ya Tanzania na British Aerospace Systems Limited ukiwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 39.37
Ununuzi wa Rada ulilalamikiwa na wananchi wengi wakiwemo wanaharakati, wanasiasa na wasomi amabao walisema hapakuwana umuhimu wa kununua chombo hicho kwa gharama kubwa wakati uchumi wa nchi ukiyumba.
Serikali ilifumbia macho kelele hizo ilishikilia msimamo wake na hatimaye ikainunua.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment