
Kilikuwa ni kisasi kitamu wakati Simba walipoifunga Polisi Dodoma kwa magoli 2-0 katika mechi yao ya marudiano iliyowarejesha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa jana huku wenyeji wakimaliza wakiwa 10 uwanjani.
Simba ambao walikuwa wamemaliza msimu uliopita na kutwaa ubingwa bila ya kupoteza mchezo walianza kwa kishindo pia msimu huu kwa kushinda mechi tatu mfululizo kabla ya kukutana na kipigo chao cha kwanza katika ligi baada ya mechi 30 wakati walipochapwa 1-0 na Polisi Dodoma jijini Mwanza.
Mshambuliaji aliyekuwa katika kiwango cha juu kabisa jana, Mussa Hassan 'Mgosi', alifunga mara mbili na kufikisha idadi ya magoli saba ya ligi msimu huu na ilikuwa almanusura apige 'hat-trick' kama goli lake jingine la 'fri-kiki' iliyokwenda moja kwa moja wavuni lisingekataliwa na mwamuzi Alex Mahagi wa Mwanza katika dakika ya 42 kwa maelezo kwamba mpira ulitakiwa kuguswa zaidi ya mara moja kabla ya kuelekezwa langoni.
Baada ya kukataliwa goli, Mgosi alifunga goli la kwanza la Simba kwa 'fri-kiki' nyingine kali iliyokwenda moja kwa moja wavuni kufuatia wachezaji wa Polisi kumuangusha mshambuliaji wa Simba, Mbwana Samatta dakika nane baadaye ya kipindi cha pili kuanza.
Polisi walipoteza mchezaji wao Semsue Juma katika dakika ya 63 kufuatia kadi ya pili ya njano kwa kumchezea rafu kiungo wa Simba, Mohammed Banka, kadi ambayo ilizidi kuwadhoofisha wenyeji.
Mgosi alikamilisha furaha ya wana-Msimbazi katika dakika ya 84 kwa goli la pili alilofungwa kwa kichwa kufuatia piga-nikupige langoni mwa wenyeji katika mechi hiyo ambayo kipa chaguo la kwanza Juma Kaseja alirejea langoni baada ya kutemwa katika mechi mbili mfululizo kufuatia kuomba msamaha kwa makosa yaliyoigharimu timu katika kipigo chao cha tatu msimu huu cha 3-2 kutoka kwa Azam FC.
Kwa ushindi huo, Simba imekwea kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na pointi 33, moja juu ya Yanga iliyoshikiliwa kwa sare ya 0-0 nyumbani kwa Majimaji ya Songea juzi. Simba bado ina mechi moja mkononi.
Kocha wa Simba, Patrick Phiri alisema baada ya mechi hiyo kuwa cha muhimu kwake kilikuwa ni pointi tatu na kwamba ushindi katika mechi hiyo utaongeza morari ya wachezaji wake ambao wanajiandaa na mechi yao ya marudiano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Elan Club de Mitsoudje ya Comoro jijini Dar es Salaam wikiendi hii.
John Simkoko, kocha wa Polisi, alisema kutoelewana pamoja na makosa yaliyofanywa na mabeki wake kulichangia kuizamisha timu. Hata hivyo, Simkoko aliwataka wadau wasikate tamaa kuichangia na kuishangilia kwa sababu hiyo ndiyo timu pekee ya mkoa.
Ligi hiyo inaendelea tena leo wakati JKT Ruvu wakatapocheza dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Vikosi vilikuwa; Polisi: Said Kombo, Nahoda Bakari, Eliasa Mashaka, Noel Msalava, Salmini Kissy, Ismail Mkulo, Sihaba Mathias/ Pascal Maige (dk.68), Ally Khalid/ Abdalla Seif (dk.82), Juma Semsue, Mohammed Seif, Delta Thomas
Simba: Juma Kaseja, Amir Maftah, Shamte Ally, Jerry Santo, Kelvin Yondani, Juma Nyosso, Amri Kiemba/ Mohammed Banka (dk.81), Patrick Ochan, Mbwana Samatta, Nico Nyagawa/ Shija Mkina (dk 51), Mussa Hassan 'Mgosi'.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment