ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 9, 2011

Stars kupambana na Wapalestina leo-Habari Leo

Image
TIMU ya soka ya Taifa ‘Taifa Stars’ leo itashuka kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kuikaribisha Palestina katika mechi ya kimataifa ya kirafiki. 

Licha ya kwamba ni mechi ya kirafiki, lakini ina ugumu hasa kwa Stars ambayo imeizidi Palestina kwenye ubora wa viwango vya Fifa. 

Kwa mujibu wa viwango vya ubora vya Fifa viliyotolewa Februari 2 mwaka huu, Tanzania ‘Taifa Stars’, inashika nafasi ya 123 huku Palestina ni ya 178. 


Hiyo inamaanisha Stars inatakiwa ishinde mechi hiyo, lakini kinyume na hapo ni kuipa faida Palestina ambayo itapanda kwenye ubora wa Fifa na Tanzania kuzidi kuporomoka. 

Mechi hiyo itakuwa ya kwanza kwa Stars tangu itoke kwenye michuano ya Bonde la Mto Nile iliyofanyika mjini Cairo, Misri Januari mwaka huu na kushika nafasi ya sita kati ya timu saba. 

Kocha Mkuu wa Palestina, Mousa Bezaz akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jana, alisema timu yake inawania kupata ushindi ili ipande katika viwango vya ubora vya Fifa. 

Lakini kocha wa Stars Jan Poulsen yeye alisema atatumia mchezo huo kujiweka sawa kabla ya kukutana na Jamhuri ya Afrika ya Kati katika mechi ya michuano ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika za mwaka 2012 mchezo utakaofanyika mwezi ujao na si kwa sababu ya kupanda kwenye ubora wa viwango vya Fifa. 

“Kwangu mimi viwango vya ubora vya Fifa sio muhimu sana kwa sababu sijui wanatumia vigezo gani katika kupanga orodha hiyo , lengo langu katika mchezo wa kesho (leo) ni kuwajaribu wachezaji wangu kwa ajili ya mchezo wetu CAN wa mwezi ujao, ” alisema. 

Poulsen wiki iliyopita alitangaza kikosi chake kwa ajili ya mchezo huo akiwa amefanya mabadiliko mbalimbali ukilinganisha na kikosi kilichoenda Misri. Amewarudisha katika timu washambuliaji John Bocco, Mussa Mgosi na kiungo Mohammed Banka hali ambayo inaonesha ameona udhaifu katika umaliziaji. 

Ni jukumu la safu hiyo ikiongozwa na Mrisho Ngasa kuhakikisha inapambana vilivyo kuibuka na ushindi na kuwapa raha Watanzania ambao walio wengi wanaiona Stars kama timu isiyokuwa na uhakika wa ushindi. 

Lakini pia safu ya ulinzi inayoongozwa na Nadir Haroub na Aggrey Morris ina jukumu kubwa la kumlinda kipa Juma Kaseja na kuhakikisha hapati madhara.

No comments: