*Ni kupinga bunge kubadili kanuni kuwabana
Na Kulwa Mzee, Dodoma
KIONGOZI wa Upinzani bungeni, Bw. Freeman Mbowe jana aliwaongoza na wabunge wa chama hicho kutoka nje ya bunge kupinga
kubadilishwa kwa kanuni iliyokuwa inakitambua Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilichofikisha asilimia 12.5 ya wabunge kama Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Wabunge hao waliamua kutoka bungeni mara baada ya mchango wa Bw. Mbowe kuhusu mjadala wa kubadili kanuni hiyo, ambayo mtoa hoja, Naibu Spika wa Bunge, Bw. Job Ndugai, alisema ni Azimio la kutafsiri kanuni maneno 'Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni'.
Katika mchango wake Bw. Mbowe alisema wamba hawatendewi
haki, watakuwa wanafiki kama watashiriki katika utaratibu wa mwisho wa suala hilo.
Bw. Mbowe alilazimika kuwa mchangiaji wa mwisho baada ya Mbunge wa ubungo, Bw. John Mnyika kuomba mwongozo wa spika, kwa kuwa mjadala ulikuwa unaelekea kumalizika bila Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani kupewa nafasi, na hivyo kuomba mjadala uahirishwe, lakini Spika Anna Makinda aliamua kumpa nafasi.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA, alisema hawawezi kuingizwa katika ndoa wasiyoiridhia kwa kuwa wananchi walioamua kutoa ridhaa kwa CHADEMA kuwa chama kikuu cha upinzani ndio hao waliamua kila chama kipate kura zilizopatikana katika uchaguzi mkuu.
"Hatuna ugomvi na chama chochote, tunatofautiana kwa misimamo, tuheshimu kanuni lakini kanuni ikiua msingi wa haki ni batili," alisema.
Alisema kila chama kina haki, katika hilo hawakutendewa haki hivyo watakuwa wanafiki kama watashiriki katika utaratibu wa mwisho wa kubariki hilo. Baada ya kauli hiyo, wabunge wote wa chama hicho waliinuka na kutoka ndani ya ukumbi.
Akizungumzia hilo Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda alisema katika hilo CHADEMA wamepitiwa, hawana uhalali wowote na kuongeza kwamba siasa ni kuvumiliana na kuwa wakweli.
"Kutoka nje hiyo si tabia ya kibunge, wanatakiwa kuonesha wanaweza kutawala na kuongoza baadaye," alisema na kuhoji kwamba hali itakuwaje ambapo kila panapokuwa na hoja ya kubishania wanatoka nje kwani hiyo ndiyo kazi waliyotumwa na wananchi?
Baada ya CHADEMA kutoka nje, Bunge lilipitisha hoja kwa sauti za ndiyoooo, kutoka kwa wabunge wa vyama vingine, hivyo Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni itaundwa na wabunge wote wa vyama vya upinzani.
Mapema akichangua hoja hiyo, Mbunge wa Kawe, Bi. Halima Mdee (CHADEMA) aliwashtukia baadhi ya wabunge wa upinzani akisema sasa wamegeuka kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) B, baada ya muafaka wa Zanzibar kuonekana kuingizwa kinyemela kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mjadala huo ulihusu hoja ilizowasilishwa na Mbunge wa Kigoma Kusini, Bw. David Kafula (NCCR-Mageuzi) na Mbunge wa Wawi, Bw. Ahmad Rashid (CUF) waliotaka neno 'Kambi Rasmi ya Upinzani' lifutwe kwenye Kanuni za Bunge za mwaka 2007 na wabunge wote wa upinzani waunde kambi ya upinzani badala ya chama chenye viti vingi bungeni.
Kutokana na hoja hiyo, bunge liliwasilisha azimio la kutaka 'kutafsiri' kanuni hiyo na kufanya maneno 'Kambi Rasmi ya Upinzani yamaanishe wabunge wa vyama vyote, ambao si wa chama tawala.
Kulingana na kanuni hizo, kambi Rasmi ilikuwa imaanisha wabunge wa chama ambacho kimefikisha asilimia 12.5 ya wabunmge wote, ambacho kwa bunge hili ni CHADEMA, bila kukilazimisha kuwajumuisha wapinzani wengine.
Bi. Mdee alisema kwa mara ya kwanza wapinzani wanapigiwa makofi na wabunge wa CCM wakati wakiunga mkono hoja hiyo, hali aliyosema inaonesha wabunge wanajivisha viremba vya wawakilishi kama wapinzani, leo wanageuka CCM B.
Alisema anachoona ni muafaka Zanzibar unataka kuletwa bungeni kinyumenyume kuzimisha nguvu ya CHADEMA kwani haiwezekani kuwaongoza watu wanaotofautiana kisera, lakini kwa kuwa wako wengi wanaopigia kura azimio la mabadiliko hayo litapita, ukweli utabaki pale ple.
"Tunajua wenyeviti wa kamati kazi yao ni kupata ajenda za bunge, upepo huu wa ushirikiano na CCM tutakuta ajenda zinazoletwa ni zile za mtawala anazotaka," alisema.
Akichangia mabadiliko hayo, Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), Bw. John Cheyo alisema lazima nchi itawalike kwa amani, hivyo kitu chochote kinachowasilishwa kwa ajili ya kufanya nchi isitawalike kwa kuwepo kwa migomo na mauaji lazima kikataliwe.
Alisema Watanzania wanataka kambi ya upinzani yenye nguvu, kama kuna vipengele vya kudhoofisha hivyo vinakwenda kinyume na kanuni, aliwaomba CHADEMA kupunguza hasira watengeneze bunge litakalotegemewa na wananchi, wasiendeleze uadui.
"Nanyi chama tawala mambo ya kura myaache, mtawale nchi, Rais Jakaya Kikwete tawala nchi baada ya miaka mitano wengine wapigiwe kura," alisema.
Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tindu Lissu (CHADEMA) alisema waliowasilisha maombi hayo lengo lao kupata madaraka wakati Watanzania hawakuwapa nafasi katika vyama vyao.
Alisema chama cha upinzani chenye viti vingi bungeni ndio chenye nafasi ya kushika nafasi za uenyekiti katika kamati za kusimamia fedha za umma, chama chenye kiti kimoja kupata nafasi hiyo ya ulinzi wa fedha za umma haiwezekani.
"Hatuko tayari kuwa na ndoa na chama chenye ndoa na chama kingine ukivuka Bahari ya Hindi, sheria inaruhusu ndoa ya wake wengi lakini si ndoa ya wanaume wengi," alisem na kuongeza kwamba hawako tayari CHADEMA kuburutwa katika hoja hiyo ya mabadiliko.
Bw. Kafulila akichangia alisema upinzani kutofautiana wenyewe kwa wenyewe ni jambo la aibu, wale wanaopinga mabadiliko hayo haoni sababu zaidi ya ubaguzi.
"Tunashinda kwa asilimia 20 tunakataa mseto, tukipata asilimia 60 hali itakuwaje, ukipata kidogo uoneshe una busara ya kufanya kazi pamoja, kwa hali hiyo ukipewa kikubwa huwezi kuaminika," alisema.
Naye Bw. Mohamed alisema kuna dhana kwamba kuna watu wanabebwa na CCM, hakuna anayebebwa na chama hicho kufanya mabidiliko pale panapoonekana kuna haja, ni jambo la kawaida, hizo tofauti za ubaguzi zinazojengwa si wanazotaka Watanzania kusikia.
"Mkuki kwa nguruwe kumbe, CUF mbona hatukulalamika? Tushirikiane tumepata ridhaa kwa wananchi," alisema na kuunga mkono azimio hilo.
No comments:
Post a Comment