
WaziriI wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige
Arusha
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige amesimamisha mkataba, unaoruhusu kiwanda cha kufuma vyandarua cha A to Z, kukata matawi ya miti kwenye shamba la miti la serikali la Meru Usa River, lililopo Olmotonyi wilayani Arumeru kwa malipo ya Sh 1,000 kwa tani moja.
Pia Maige amemsimamisha kazi na kumshusha cheo, meneja wa shamba hilo, Rumisha Maro baada ya kushindwa kusimamia maduhuli ya serikali yatokanayo na mauzo ya miti na mazao yake katika shamba hilo.
Maige amefikia uamuzi huo, baada ya kufanya ziara katika shamba hilo, na kushangazwa na Sh200 milioni kama mapato yaliopatikana kwenye shamba hilo.
Awali waziri huyo, alishangazwa na utawala wa shamba hilo, kuruhusu matawi kutoka katika shamba hilo, kutumika kuchemshia maji ya kutengezea vyandarua na kuuzwa kwa bei hiyo.
Waziri Maige aliagiza iundwe kamati maalumu ya kuchunguza ubadhirifu wa mapato ya shamba hilo, na kuagiza kuvunjwa kwa mkataba huo.
“Mkurugenzi, na hili pia lifanyiwe kazi katika kamati maalumu mtakayoiunda, yaani mnafikia kuuza matawi ya miti tani moja kwa elfu moja?"alihoji Maige.
Licha ya kumwagiza mkurugenzi wa misitu katika Wizara ya Maliasili na Utalii, kumsimamisha kazi meneja huyo, pia Maige alimuagiza mkurugenzi huyo, kumtafutia kazi nyingine wizarani ili awe chini ya uangalizi maalumu.
Alisema shamba hilo, lenye ukubwa wa hekta 26,000 kuanzia mwaka 2000 hadi sasa mapato yake yamekuwa Sh 200 milioni kwa mwaka mmoja wakati lina uwezo wa kukusanya zaidi ya Sh500 milioni.
Alimtaka Mkurugenzi huyo, kuunda kamati maalumu ya kuchunguza mitambo yote ya shamba hilo, ya kutengeneza barabara na kujua kiasi cha fedha kilichokusanywa tangu mwaka 2008 na kuhakikisha mitambo, iiliyoharibiika inatengenezwa na ambayo iko nje ya shamba hilo, inapaswa kurejeshwa.
Pia aliitaka kamati hiyo, kufanya ukaguzi wa mahesabu yote ya shamba hilo, pamoja na kukagua vitalu vya miti na makusanyo na kutoa ripoti kwa kwake.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment