ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 17, 2011

Waziri Makame atwishwa zigo

Madiwani wa Chama cha Wananchi (CUF), wamesema uamuzi wa kuwatimua wafanyabiashara wenye maduka ya makontena Darajani ni utekelezaji wa agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini.
Waliyasema hayo jana wakati wakizungumza na waandishi wa habari katika eneo la Vuga Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja kuhusu mgogoro kati ya wafanyabiashara hao na Manispaa ya Mji wa Zanzibar.

Diwani Nassor Amin Said wa Wadi ya Mkunazini wakizungumza kwa niaba ya wenzake, Ahmed Salim Bashut Wadi ya Mchangani na Arafa Mohammed Said wa Viti Maalum, walisema operesheni inayoendelea siyo ya Manispaa bali ni Waziri huyo ndiye aliyeagiza wafanyabiashara hao waondolewe.
“Operesheni ya kuwahamisha wafanyabiashara haikutokana na Baraza la Manispaa ni utekelezaji wa agizo la Waziri kama tulivyoambiwa na Mkurugenzi katika kikao cha Febuari 14, mwaka huu,” alisema Diwani Bashut huku akiungwa mkono na wenzake.
Alisema katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Baraza hilo, Rashid Ali Juma aliwaeleza kuwa alipokea wito wa waziri mwenye dhamana wa baraza hilo na kumueleza kuwa Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, ameagiza wafanyabiashara hao waondolewe na kupelekwa Saateni.
Alisema katika kikao hicho, ajenda zilikuwa mbili kujadili hotuba ya Waziri huyo aliyotoa alipofungua baraza hilo na kujadili utendaji wa kamati zinazounda Idara za Manispaa.
Alisema ghafla ilichomekwa ajenda kuhamishwa kwa wafanyabiashara hao jambo ambalo wao hawakuridhia bila ya kuwapo matayarisho ya kutosha kwa vile Baraza la Manispaa limekuwa likiwauzia fomu za leseni za mwaka na madiwani kuwagongea muhuri katika maeneo yao.
CHANZO: NIPASHE

No comments: