ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 17, 2011

Simba yavutwa sharubu

Goli la kusawazisha la dakika za nyongeza liliwanyima mabingwa Simba ushindi wakati waliposhikiliwa kwa sare ya 2-2 na Toto African mkoani Mwanza huku Azam FC ikiivuka Yanga kwenye msimamo wa ligi kuu ya Bara kufuatia ushindi wa 3-0 dhidi ya African Lyon jijini Dar es Salaam jana.
Toto walitangulia kupata goli lililofungwa kwa kichwa na Tete Kang’ang’a katika dakika ya 25 na Simba walipoteza nafasi ya kusawazisha dakika saba baadaye wakati penati ya Rashid Gumbo ilipopanguliwa na kipa Wilbert Mneta.
Hata hivyo, Gumbo alirekebisha makosa yake katika dakika ya 61 wakati alipopiga kona ‘kali’ iliyomshinda kipa Mneta na kuipatia Simba goli la kusawazisha.

Mshambuliaji aliye katika kiwango cha juu hivi sasa, Mbwana Samatta aliifungia Simba goli la pili katika dakika ya 71 baada ya kupokea pasi ya Mussa Hassan ‘Mgosi’ na kumlamba chenga kipa kabla ya kupiga shuti lililojaa wavuni.
Huku Simba wakiwa na matumaini ya kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi, wenyeji waliwanyamazisha mabingwa kwa goli la ‘usiku’lililofungwa kwa kichwa pia na Mohamed Soud kufuatia piga nikupige langoni mwa wageni.
Awali, Toto waliamini kuwa wanaongoza 2-0 katika dakika ya 34 baada ya mfungaji bora wa zamani wa ligi kuu, Sammy Kessy kupiga shuti lililomshinda kipa Juma Kaseja na kutinga wavuni lakini refa Zacharia J. kutoka Pwani kulikataa kwa maelezo kwamba yalifanyika madhambi kabla mpira kumfikia mfungaji.
Jijini Dar es Salaam, Mrisho Ngassa alijiimarisha kileleni mwa orodha ya wafungaji wanaoongoza katika ligi kuu wakati alipoisaidia Azam FC kushinda 3-0 dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Uhuru.
Ngassa alifunga goli lake la 11 la ligi msimu huu katika dakika ya 9 kabla ya Himid Mao Mkami na Ramadhani Chombo ‘Redondo’ kuongeza mengine yaliyoipaindisha Azam juu ya Yanga katika msimamo kwa tofauti ya magoli, lakini Yanga ina mechi moja mkononi.
Yanga itakuwa ugenini Bukoba dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba katika mechi pekee ya ligi kuu itakayochezwa leo.
Katika mechi ya Mwanza, vikosi vilikuwa:
Toto: Wilbert Mneta, John Bosco, Philemon Mwandisilo, Ladislaus Mbogo, Laban Kambole, Maregesi Mwangwa, Tete Kang’ang’a, Jacob Massawe, Sammy Kessy, Hussein Kessy na Mohamed Soud.
Simba: Juma Kaseja, Haruna Shamte, Amir Maftaha, Juma Nyoso, Kevin Yondan, Mohamed Banka, Rashid Gumbo, Patrick Ochan, Ali Ahmed Shiboli, Mbwana Samatta na Mussa Hassan ‘Mgosi’.
CHANZO: NIPASHE

No comments: