ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, February 17, 2011

Unazianika siri za mpenzi wako hadharani ili iweje?-GPL

Romantic Silhouette Brushes
Tunakutana tena kupitia safu hii ya mashamsham nikiamini kuwa u mzima na unaendelea freshi na mishemishe zako za kimaisha.

Juzi ilikuwa ni siku muhimu sana kwa wapenzi. Naizungumzia Valentine’s Day au kwa lugha iliyozoeleka tunaiita Siku ya Wapendanao. Ilikuwaje kwa upande wako? Uliifurahia au ulitamani hata siku hiyo isingekuwepo?


Anyway, tuachane na hayo na turudi kwenye mada ya wiki hii. Nazungumzia tabia mbaya isiyoleta picha nzuri ambayo imejengeka kwa baadhi ya watu walio katika uhusiano hasa wanaume.

Juzi nikiwa maeneo flani, nilimsikia kijana mmoja akimchana vibaya mpenzi wake mbele za washkaji zake. Alichokuwa akiongea kuhusu mpenzi wake, kilinikera sana.

Mwenyewe aliona kufanya vile ni sifa lakini wanaojua mapenzi walimuona limbukeni. Binafsi najua umuhimu wa watu kukutana maeneo mbalimbali kama vile baa na vijiweni kisha kubadilishana mawazo juu ya maisha yao ya kila siku.

Ni jambo la msingi sana kwani naamini watu zaidi ya mmoja wanapokutana na yanayozungumzwa yakawa ni yenye maana, lazima yatakuwepo mabadiliko chanya kwa wahusika.

Lakini pamoja na yote hayo, nimegundua kuna baadhi ya wanaume wanapokuwa kwenye mazungumzo kama hayo, huzungumzia maisha yao ya kimapenzi. Baya zaidi ni kwamba, badala ya kuzungumzia yale ambayo ni mazuri, huingia kwenye kuzianika kasoro walizonazo wapenzi wao.

Eti wanafanya hivyo wakiwa na imani kwamba kwa kuzieleza kasoro hizo, wenzao watawasaidia kutafuta ufumbuzi. Unaweza kumsikia jamaa akisema mbele ya wenzake, “Ah! Demu wangu ananuka sana sehemu zake muhimu, yaani ananiboa sana.”

Huo ni mfano, kuna mambo ya ndani ambayo katika mazingira ya kawaida haileti picha nzuri kuyazungumza mbele za watu!

 Nasema hivyo kwa sababu mapenzi ni mambo ya siri hivyo ni vyema yakaheshimiwa na ifike wakati basi tuchuje yale ambayo tunastahili kuyanadi mbele za watu kuhusu wapenzi wetu na mengine yabaki kuwa siri ya wewe na mpenzi wako.

Yako mambo mengi ya mpenzi wako yasiyostahili kusemwa mbele za watu. Muhimu kabisa ni masuala yote yanayohusu tendo la ndoa, kasoro za kimaumbile hasa za mwili, uwezo wa kuelewa mambo na elimu hasa inapokuwa ya chini.

Migogoro ya ndani, hitilafu za kitabia na dhiki mnazokabiliana nazo hazitakiwi kujulikana kwa wengine kama kweli mnapendana kwa dhati.

Athari za kutoa siri za mpenzi wako zipo na uchunguzi unaonesha kwamba sababu nyingi za kusalitiana au kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi hutokana na kuvuja kwa siri za ndani za wapenzi.

Endapo mwanaume atatangaza jinsi mpenzi wake asivyotosheka na tendo la ndoa au namna mkewe anavyoongoza kwa usaliti, sina shaka wafitini watapata pa kuanzia.

Labda nijaribu kutoa mfano mmoja ambao utawafanya wale wenye tabia ya kuzianika siri za wapenzi wao kwa washkaji zao wanielewe ninachokizungumza.

Jamaa mmoja alikuwa na mpenzi wake ambaye hajawahi kufanya mapenzi hata siku moja. Kwa kifupi demu yule alikuwa ni mgeni kwenye ulimwengu wa mapenzi. Baada ya mwanaume huyo kumpata, siku moja wakakutana faragha.

Demu alikuwa hajui chochote, mwanaume badala ya kuona amepata mpenzi sahihi aliyejitunza, akaanza kulalamika kwa wenzake eti demu wake mshamba na anataka kumuacha.

Unajua walichokifanya washkaji zake? Kila mmoja akawa anatamani kumpata demu yule kwani walijua jamaa hajui vitu vizuri.

Ndiyo maana nauliza, hivi kuwaambia washikaji zako kwamba mpenzi wako hajui mapenzi unataka wao wamfundishe au anataka wakushauri uachane naye? Ukishamuacha je? Jibu ni kwamba watamchukua wao, sasa sijui kama wewe utafurahi.

Niseme tu kwamba, kama mpenzi wako si mtundu wala mbunifu kunako yale mambo yetu, suluhisho si kumchana kwa wenzako. Chukua jukumu la kumuelekeza katika hili na lile na mwisho atakuwa bora zaidi na mtayafurahia maisha yenu. Siri yake ibaki kwako na yako ibaki kuwa yake.

Ni hayo tu kwa leo, tuonane tena wiki ijayo kwa mada nyingine kali zaidi.

1 comment:

Anonymous said...

Mademu ndio wanaongoza kubwatuka siri za wapenzi wao hapa DC ukichukua demu wa kibongo ujue maswahiba wake wote wanajua mnaishije.Mzee unaingia Swahili mademu wenzie wanakung'ong'a tu coz mamsap' kashasanua kila kitu.