8th March 2011
.jpg)
Waathirika wote wa mabomu yaliyolipuka Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam, wamezidi kung'ang'ania kulipwa fedha taslim badala ya kujengewa nyumba na Jeshi la Kujenga la Taifa (JKT).
Msimamo huo ulitolewa na waathirika hao jana katika mkutano wa pamoja baina yao na Kamati ya Maafa Mkoa wa Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake, ambaye ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (KIU), Gongo la Mboto.
Hata hivyo, kamati hiyo imesema madai ya waathirika hao wa mabomu ya kutaka walipwe mikononi fidia ya fedha taslim badala ya kujengewa upya au kukarabatiwa nyumba zao na JKT, yataamuliwa na Rais Jakaya Kikwete.
Mbali na kupinga kujengewa nyumba na JKT kupitia Shirika lake la Uchumi (Suma), waathirika hao, pia walilalamikia ugawaji mbovu wa misaada inayotolewa na wasamaria wema, baadhi ya nyumba zilizoharibiwa na mabomu kurukwa katika uhakiki na kuwapo mabomu, ambayo hayajaondolewa katika makazi hadi sasa.
Kabla ya kamati hiyo kutoa tamko hilo, waathirika hao kwa nyakati tofauti, walisema katika mkutano huo kuwa wanahofia nyumba zao kujengwa na JKT chini ya viwango na thamani ya gharama walizotumia katika ujenzi wa awali.
Pia wanahofia ujenzi wa JKT utachelewa kukamilika, huku wakiendelea kuishi maisha ya dhiki, hasa katika msimu wa masika unaotarajiwa kuanza wakati wowote nchini, kuanzia sasa.
Fadhili Saidi, ambaye nyumba yake imeteketea moto baada ya bomu kutua kitandani, katika Mtaa wa Markaz Gongo la Mboto, aliiomba kamati kumfikishia Rais Kikwete ujumbe kwamba, abadili uamuzi wake wa kutaka nyumba zao zijengwe na JKT, badala yake kila mmoja alipwe mkononi fedha zake stahiki ajenge mwenyewe haraka.
“Kwa sababu ujenzi wa JKT utachelewa na mvua za masika zinakuja. Sasa kila mmoja akikasimiwa chake, atajua mwenyewe cha kufanya,” alisema Fadhili.
David Johnson, mkazi wa Pugu, alisema kila nyumba ilijengwa kwa gharama tofauti na kutolea mfano wa nyumba yake, ambayo alisema aliijenga mwaka 1994 kwa gharama ya Sh. milioni 30 na kusema ana wasiwasi kwamba, ujenzi wa JKT unaweza kuwa wa gharama ya Sh. milioni 10.
“Kwa maana hiyo, sikubaliani Suma-JKT kujenga nyumba zetu. Aje injinia athamini kiwango halisi. Maana kuna wengine wanasema tukipewa fedha tutakunywa. Mimi wakati najenga mbona sikunywa?” alihoji Johnson na kushangiliwa na waathirika wenzake waliofurika katika mkutano huo.
Masunya Mbegete, mkazi wa Mtaa wa Mwembe Madafu, alisema naye nyumba yake aliijenga mwaka 1994 wakati huo mfuko mmoja wa saruji ulikuwa ukitoa matofali 25 na kusema hadhani kama Suma-JKT wanaweza kujenga tena kwa kiwango hicho.
“Kwanza Jeshi wanajenga kwa amri. Hivyo, Hatutaki JKT, tunataka pesa cash (taslimu). Tunaomba mtufikishie hili kwa Mheshimiwa Rais,” alisema Mbegete.
Musa Lugoma, mkazi wa Majohe, alisema kazi ya uhakiki wa nyumba zilizoharibiwa na mabomu iliyotarajiwa kukamilika siku tatu, ilichukua wiki tatu, hivyo ana wasiwasi Suma-JKT nao wanaweza kupewa mwezi mmoja kukamilisha ujenzi wa nyumba zao.
Alisema haoni sababu kwa serikali kulazimisha JKT kujenga nyumba zao kwani ina wataalamu wengi, hivyo akataka ifanye utaratibu wa kila mmoja kulipwa fedha ili akajenge mwenyewe nyumba yake.
“Kama ni mizengwe hata Suma-JKT wakijenga mizengwe inaweza pia kujitokeza, kwani JKT wengine hawajui thamani ya ujenzi, wanachojua ni kubeba matofali na kujenga tu,” alisema Lugoma.
Akijibu hoja hizo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Saidiki alisema madai hayo yatafafanuliwa na Rais Kikwete kwa vile ndiye aliyetoa tamko la kuiagiza JKT kujenga nyumba hizo.
Hata hivyo, Sadiki alilaumu kitendo cha waathirika hao kukimbilia kuwahukumu JKT kabla ya kuelewa tamko hilo la Rais Kikwete.
Alisema Suma-JKT wanaaminika, kwani ndio wanaojenga majengo ya serikali, zikiwamo nyumba wanazoishi mawaziri, hivyo haoni sababu ya kuwa na wasiwasi na jeshi hilo.
Alisema mwathirika, Mwajuma Mtoro, mkazi wa Kipunguni ‘B’ Machimbo, aliyefiwa na mumewe kutokana na mabomu, watoto wake wataingizwa katika orodha ya watoto yatima watakaosomeshwa kwa gharama za serikali.
Sadiki alisema amewasiliana na Mkuu wa Majeshi la Ulinzi na Usalama, Jenerali Davis Mwamunyange pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ili kuwapeleka wataalamu bingwa kwa ajili ya kuwapima waliolalamika afya zao kuathiriwa na mabomu.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Leonidas Gama, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, alisema wameiagiza timu ya uhakiki kuzirudia kuzihakiki nyumba zilizoachwa kwa udhaifu wa kibinadamu katika uhakiki wa awali na kwamba, kazi hiyo ilianza jana.
Kuhusu madai ya baadhi ya waathirika kutopata msaada, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Gabriel Fuime, alisema misaada hiyo haitolewi kwa kila mtu, bali kwa wale tu wanaostahili.
Viongozi wote walitoa namba za simu zao kwa waathirika kwa ajili ya kuwasiliana na kamati kama kuna jambo, badala ya kubaki na hisia.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment