ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 8, 2011

Refa Oden Mbaga alonga ya moyoni

8th March 2011


Mwamuzi wa kimataifa mwenye beji ya Shirikisho la Soka duniani (FIFA) Oden Mbaga

Mwamuzi wa kimataifa mwenye beji ya Shirikisho la Soka duniani (FIFA) Oden Mbaga, ambaye Jumamosi alichezesha mechi kati ya watani wa jadi nchini, Yanga na Simba, amesema kuwa yeye alifanya kazi yake kwa mujibu wa kanuni za mchezo huo na kama alifanya kosa lolote kamati ya waamuzi hapa nchini ndiyo yenye mamlaka ya kutathmini kazi yake aliyoifanya.
Mbaga ambaye alikuwa katikati katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa akisaidiana na Mohammed Mkono kutoka jijini Tanga na Maximillian Nkongolo wa Rukwa aliliambia gazeti hili jana kwamba hakuwa na tatizo lolote katika mechi hiyo iliyomalizika kwa watani hao kutoka sare ya goli 1-1.
"Nashukuru nilimaliza na kutoka salama baada ya kumaliza mchezo ule, ila siwezi kuzungumzia lolote kuhusiana na yanayosemwa kwa sababu kanuni haziniruhusu kuzungumza," alisema mwamuzi huyo.

Mbaga aliongeza kuwa mwamuzi haruhusiwi kuuzungumzia mchezo kabla na baada na wenye mamlaka ni kamati ambayo ndiyo huwapangia majukumu.
Magoli yote mawili yaliyopatikana katika mchezo huo yamelalamikiwa na viongozi, wachezaji na wadau wa soka nchini ambapo kwa upande wa goli la Yanga, kipa, Juma Kaseja, aliyekuwa langoni alidai kuwa mpigaji wa penati ya Yanga, Stephano Mwasika, alitoka kabla ya filimbi huku wengine wakisema kuwa mshambuliaji, Davies Mwape, hakufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari.
Mmoja wa viongozi wa soka nchini ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema kuwa kama Mwape alifanyiwa madhambi ndani ya boksi, ilipaswa beki wa Simba, Juma Nyoso apewe kadi nyekundu na ndipo penati hiyo itolewe.
Goli la Simba pia lilijaa utata na lilikubaliwa baada ya Mbaga kupata msaada wa Nkongolo. Wadau wa soka waliokuwa wakiungalia mchezo huo kupitia televisheni walidai kwamba mfungaji, Mussa Hassan 'Mgosi' alikuwa ameotea kabla ya kufunga goli hilo la kusawazisha kwa timu yake.
Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa, Taifa Stars, Yanga na Pan African, Mohammed Rishard 'Adolph' alisema kuwa magoli yote ni sahihi na watu wanatakiwa kukubaliana na mwamuzi ambaye hupewa dhamana ya kusimamia mchezo.
Sare hiyo iliifanya Yanga iendelee kuongoza katika msimamo wa ligi kutokana na kufikisha pointi 39 huku Simba ikiwa ya pili baada ya kujikusanyia pointi 38. Hata hivyo, Simba ina kiporo cha mechi moja ambayo wataicheza kesho dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Ligi hiyo inaendelea leo kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam kwa African Lyon kuikaribisha Polisi Dodoma ambayo nayo iko katika hatari ya kushuka daraja.
CHANZO: NIPASHE

No comments: