Mchezaji wa klabu ya Polisi, Bero Hamad, ambaye alijeruhiwa vibaya baada ya kutuhumiwa na polisi mwenzie kuwa ni mwizi ameruhusiwa kutoka hospitali alikokuwa amelazwa.
Bero alijeruhiwa mwishoni mwa wiki maeneo ya Area D alipokuwa akienda dukani kununua vocha ya simu lakini cha kushangaza alianza kuitiwa kelele za mwizi.
Mchezaji huyo ambaye ni mwenyeji wa Zanzibar alikuwa amelazwa kwenye Hospitali ya Mkoa ya Dodoma kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Akizungumza na NIPASHE jana, mwenyekiti wa timu hiyo, Israel Mwansasu alisema mchezaji huyo kwa sasa anaendelea vizuri na ameruhisiwa baada ya kumaliza matibabu yake.
“Kwa sasa yupo kwenye hali nzuri, nina imani baada ya muda mfupi ataanza kuichezea tena timu yake,” alisema.
Hata hivyo, Mwansasu alilaani kitendo cha kinyama ambacho kilifanywa na baadhi ya watu waliomtuhumu mchezaji huyo kuwa mwizi na kudai hakiitakii mema timu ya Polisi.
Alisema kuwa hao ni baadhi ya watu wachache wasioipenda timu ya Polisi na ndiyo maana wakaamua kumfanyia unyama mchezaji wao.
Aliongeza kwa sasa mchezaji huyo anahojiwa na viongozi wao kwa ajili ya kutambua kama alifanya kosa. “Siwezi kuzungumza sana ila ngoja amalizane na masuala ya ofisi kwanza,” alisema.
Polisi aliyemwitia mwizi mchezaji huyo bado hajatajwa kwa maelezo kwamba suala hilo linafanyiwa kazi kiofisi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment