Lasema maandamano ni haki kwa kila chama
John Tendwa awaahidi kulifanyia kazi
Lapendekeza kukutana na JK kumshauri
John Tendwa awaahidi kulifanyia kazi
Lapendekeza kukutana na JK kumshauri.jpg)
Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini wameitaka serikali kukutanishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa lengo la kujadiliana tofauti zao ili kufikiana mwafaka.
Pendekezo hilo lilitolewa jana jijini Dar es Salaam na wajumbe wa Bazara hilo wakati wakitoa mapendekezo yao katika mkutano ambao uliitishwa kujadili mwenendo wa hali ya kisiasa nchini na mahusiano baina ya vyama vya siasa na dola hususani kampeni za Chadema dhidi ya serikali.
Hata hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, alisema suala la serikali kukutanishwa na Chadema na serikali atalifanyia kazi.
Serikali imekuwa ikikishutumu Chadema kuwa kinaendesha maandamano na mikutano ya hadhara yenye lengo la kuwachochea wananchi kuichukia serikali.
Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi, alisema Chadema kina lengo la kutaka nchi isitawalike.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, naye alikishutumu Chadema kwa kutoa kauli za uchochezi katika maandamano yaliyofanyika mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Kagera na kuonya kuwa itafika mahali serikali itakosa uvumilivu.
Naye Tendwa, alisema kuwa kauli zilizotolewa na viongozi wa Chadema ni za uchochezi.
Aidha, katika mkutano wa jana, wajumbe walipendekeza mambo sita.
Akisoma mapendekezo hayo, Mwenyekiti wa baraza hilo, Dk.
Emmanuel Makaidi, alisema Rais Kikwete anatakiwa kukutana na Baraza la Vyama vya Siasa ili kujadili hali halisi ya siasa na uchumi wa nchi.
Katika pendekezo la pili, chama chochote cha siasa kisitumie maneno ya matusi dhidi ya chama kingine na maandamano kwa chama chochote ni haki ya kikatiba ila kinachotakiwa kufuatwa ni sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa. Maazimio mengine ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iangalie uwezekano wa kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa, chama chochote cha siasa katika kueneza sera zake kisiwe na nia ya kuangusha serikali iliyopo madarakani isipokuwa kupitia uchaguzi halali na Baraza litoe mapendekezo ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) kurekebisha katiba yake ili kiwe chombo cha vyama vyote na mwelekeo wa kitaifa chini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Makaidi alisema lugha ya matusi haitolewi na Chadema peke yake bali hata chama tawala kimekuwa kikifanya hivyo na kueleza kuwa lugha za matusi zinapaswa kuachwa na vyama vyote.
Hata hivyo, Dk. Makaidi alisema viongozi wa vyama vya siasa watakaoshiriki katika maandamano watatakiwa kufuata maadili yaliyopangwa. Alisema kutokana na matatizo ambayo yanaikabili nchi Baraza hilo litamshauri Rais Kikwete kutumia mbinu mbalimbali za kutatua matatizo hayo.
Dk. Makaidi alisema baadhi ya matatizo yaliyopo yanasababishwa na serikali na hivyo wakikutana na Rais watamshauri.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment