ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 8, 2011

CCM Dar yataka mitambo ya Dowans iwashwe


Leon Bahati
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, kimeitaka serikali kuwasha mitambo ya Dowans kama moja ya mipango ya kukabiliana na hali ngumu ya maisha kwa wananchi walio wengi.

Mapendekezo mengine ni kutafuta ufumbuzi wa haraka kuhusu kupanda kwa bei ya vyakula nchini, upungufu wa ajira na kufidiwa kwa wafanyabiashara ndogondogo waliovunjiwa vibanda vyao na Manispaa ya Kinondoni kwenye soko maarufu kama Big Brother, jijini Dar es Salaam.


Tamko hilo lilitolewa jana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita, kwenye mkutano na waandishi wa habari. 
Akitoa tamko hilo kwa niaba ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Guninita alisema walijadili kwa kina juu ya hali ngumu ya maisha inayowakabili wananchi walio wengi na kuona mambo makuu manne yanapaswa kufanywa.

"Kamati ya siasa imeunga mkono ushauri uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, iliyotaka mitambo yote iliyoko mikononi mwa Tanesco iwashwe kukabili upungufu wa umeme," alisema Guninita.
Ingawa Guninita kwenye maelezo yake hakutaja Kampuni ya Dowans,  lakini Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ilipendekeza Tanesco kuingia mkataba mpya na kampuni hiyo ili kutatua tatizo la umeme nchini.
Lakini Guninita alitaja Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) izalishe umeme kwa kiwango cha juu kwa sababu kwa sasa inazalisha chini ya uwezo wake.

Mbunge wa Viti Maalum, Zarina Madabida, alisema wanashauri Tanesco pia kuacha kuipa umeme migodi kwa asilimia 100 ili kupunguza makali ya mgawo kwa wananchi.

"Migodi ina uwezo wa kuzalisha umeme wao wenyewe. Sio sahihi wao kutoingia kwenye mgawo...wananchi wengi wanaathirika kwa mgawo kama vile saluni na wauza vinywaji vya baridi," alisema Madabida.

Kuhusu tatizo la chakula, Guninita alisema serikali inaweza kufanikiwa kushusha bei kwa kuunda kamati maalumu itakayosimamia ununuzi wa mahindi, mchele na maharage nje ya nchi kwa kuondoa ushuru na kuhakikisha wananchi wanauziwa bei isiyo ya kulangua.

Alisema kamati ya siasa inashauri serikali kutenga fedha kama ilivyofanya mwaka 2009, ili kukabiliana na tatizo la ajira ambalo linawakumba vijana wengi.

Pia, Guninita alilalamika kuwa kitendo cha Manispaa ya Kinondoni kuwavunjia vibanda zaidi ya 350 ya wamachinga soko la Big Brother kwa kushtukiza na kusababisha mali nyingi kupotea.

"Kamati imebaini kuwa kitendo hicho sio cha utu," alisema Guninita akitaka watumishi waliotekeleza mkakati huo kuchukuliwa hatua na wafanyabiashara hao kufidiwa.


CHANZO:MWANANCHI

No comments: