MELI 16 zimeshambuliwa na maharamia katika pwani ya Tanzania kuanzia Septemba 25, mwaka jana hadi Februari 2, mwaka huu, imeelezwa.
Katika mashambulio hayo, vikosi vya ulinzi vya Tanzania vilifanikiwa kutibua mashambulio dhidi ya meli tatu na kumkamata haramia mmoja.
Akifungua mkutano wa makubaliano ya kuanzisha vituo viwili vya Mombasa na Dar es Salaam katika kupashana habari kuhusu mashambulio ya maharamia, Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu alisema matukio manane ya kwanza yalitokea Septemba 25, mwaka jana hadi 11 Oktoba mwaka huo huku mengine manane yakitokea Oktoba 12, mwaka jana hadi Februari 2, mwaka huu.
Mkutano huo ulioshirikisha nchi 17 zilizotia sahihi mfumo wa Kanuni wa Djibouti kuhusu sheria za kuwahukumu maharamia na kuandaliwa na Shirika la Kimataifa la Usafirishaji Baharini (IMO).
Nundu alisema katika mashambulio hayo, ipo la meli ya Comoro iliyokuwa ikienda Dar es Salaam ambayo ilitekwa Novemba mwaka jana, ikiwa na watu 29, kati yao 14 wanasadikiwa kuwa ni Watanzania. Meli hiyo baadaye ilipatikana nchini Madagascar na watu wote wakiwa salama.
Alisema mashambulio hayo yameathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi kutokana na meli nyingi kuhofia kupita katika pwani hiyo huku nyingine zikizunguka kufikia Bandari ya Dar es Salaam.
“Nchi inaathirika sana na suala hili kutokana na meli kuongeza gharama kutokana na kuzunguka kufikia bandari hii, meli zinazotumia bandari kupungua ambapo pamoja na sababu nyingine kontena zimepungua kutoka milioni moja zinazotegemewa hadi laki nne pekee,” alisema Nundu.
Alisema Tanzania pekee bila ushirikiano wa nchi nyingine haiwezi kudhibiti uharamia huo uliokuwa kwa kasi kuanzia miaka ya 1990 baada ya kuanza kwa mgogoro wa Somalia na kuwataka washiriki kufikia maamuzi ya kuanzisha vituo hivyo haraka.
Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Maharamia kutoka IMO, Philip Holihead alisema baada ya mkutano huo wa siku mbili, watapitisha makubaliano ya kuanzisha vituo hivyo vitakavyokamilika mwisho wa mwaka huu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), Israel Sekirasa akizungumzia vituo hivyo, alisema cha Mombasa kitahudumia nchi za Ethiopia, Kenya, Somalia na Shelisheli na cha Dar es Salaam kikihudumia nchi za Afrika Kusini, Msumbiji, Comoro, Madagascar na Mauritius.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment