.jpg)
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kufanya maandamano makubwa ya amani mkoani hapa mwezi ujao kupinga hali ngumu ya maisha kutokana na mfumuko wa bei na malipo ya fidia ya Sh. bilioni 94 kwa kampuni ya kufua umeme ya Dowans Tanzania Limited.
Mpango huo ulitangazwa juzi na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, wakati akizungumza katika semina ya madiwani wa chama hicho wa Manispaa ya Kigoma/ Ujiji.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, maandamano hayo ambayo yatahudhuriwa na viongozi wa kitaifa, wabunge na madiwani wa chama hicho, yatafanyika Aprili 6, mwaka huu.
Aidha, alisema maandamano hayo yana lengo la kupinga unyanyasaji wa vyombo vya dola dhidi ya raia na kushinikiza kutumika vizuri kwa rasilimali za taifa badala ya kuporwa na mafisadi.
Katibu huyo alisema pia, maandamano hayo yana lengo la kuishinikiza Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutekeleza ahadi zake ilizotoa kwa muda mrefu ili kuleta maendeleo katika Mkoa wa Kigoma.
“Hayo ndiyo tunayotaka kuyasema kwa serikali ya CCM,” alisema na kuongeza kuwa serikali imeshindwa kupeleka maendeleo katika Mkoa wa Kigoma kwa muda wa miaka mingi na kusisitiza kuwa Chadema inataka mabadiliko mkoani humo.
Akizungumzia kuhusu ujambazi, alisema umekithiri mkoani humo kutokana na askari wa Jeshi la Polisi kulipwa mishahara midogo.
Kuhusu wastaafu wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), alisema wanaidai Serikali Sh. bilioni 140 kwa zaidi ya miaka minane sasa, lakini pamoja na kuandamana hadi Ikulu imeshindwa kuwalipa.
“Leo anajitokeza huyo Dowans fedha iko nje nje, Kamati Kuu ya CCM inasema watalipwa,” alisema na kuongeza: “Ni jambo la kusikitisha sana kuwaona wazee wamelitumikia taifa kwa muda wa miaka mingi halafu wanaishia kunyanyasika.”
Alisema alikwenda Kigoma kwa ajili ya kuwapa semina madiwani wa Chadema ili kuwaelekeza namna ya kuiongoza Manispaa hiyo na kuwaletea wananchi maendeleo katika kata zao. Alisema madhumuni ya semina hiyo ni kuhamasisha ushirikiano kati madiwani na Meya ili kuhakikisha mabilioni ya fedha za Watanzania yanaelekezwa kwenye ujenzi wa zahanati, shule za sekondari, barabara, daraja la Mto Malagarasi na reli ili kubadilisha mkoa wa Kigoma kimaendeleo. “Na ndiyo sababu tumeamua pia kufanya maandamano haya ya amani ili kuibana Serikali kutekeleza haya ambayo imeshindwa kufanya kwa muda mrefu,” alisisitiza Dk. Slaa.
Fabruari mwaka huu, viongozi wakuu wa Chadema pamoja na wabunge walifanya ziara ya wiki moja katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuongoza maandamano makubwa sambamba na mikutano ya hadhara katika makao makuu ya mikoa na wilaya kwa lengo hilo.
Maandamano hayo yalifanyika katika mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Kagera.
Akizungumzia kuhusu fedha wanazotumia kwa ajili ya maandamano, alisema zimechangwa na wabunge na viongozi wa Chadema na si kama ilivyodaiwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba.
Slaa alisema Chadema wanamtaka Simba awaeleze Watanzania ni nani aliyepewa fedha hizo kati ya viongozi wa chama hicho, nchi na wapi makabidhiano hayo yalifanyika.
Alisema waliposema watatembea nchi zima kufanya maandamano walianza kusema Chadema inafadhiliwa na mabalozi wa kigeni kutoka nchi za nje jambo ambalo si kweli.
“Chadema inafanya kazi za siasa kwa kuchangiwa na wabunge na viongozi wake na si vinginevyo,” alisema.
Alisema wabunge wao waliwachangia Sh. milioni 19.2 wakati wa ziara ya Kanda ya Ziwa kwa ajili ya shughuli mbalimbali yakiwamo maandamano. “Hakuna serikali ya nje hata moja iliyochangia Chadema fedha ... tumeamua katika Kamati Kuu Waziri Simba aliyetoa kauli hiyo tunataka athibitishe,” alisistiza.
Alisema katika maandamano yao, watakuwa wakimuuliza mtu mmoja mmoja kama kuna mtu anapewa fedha kwa ajili ya kushiriki maandamano ili kupata ushahidi na kama hakuna Rais Jakaya Kikwete amwajibishwe waziri huyo kwa sababu anawaongopea Watanzania.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment