Umoja sasa ni vipande vipande
Kila kona sasa ni kunyukana tu
Tabora, Kilimanjaro moto mtupu.jpg)
Wajumbe wa Kamati ya utekelezaji ya Jumuia ya Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UV-CCM) Mkoa wa Tabora wamekemea hatua iliyochukuliwa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Tabora, Robert Kamoga, ya kutangaza kumvua ulezi wa Jumuiya mkoa huo, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Vijana hao wamesema kuwa kitendo hicho ni cha kihuni na kusisitiza kuwa Sitta bado ni mlezi wao.
Wakitoa tamko hilo kwa waandishi wa habari mjini Tabora jana, wajumbe hao walisema kuwa, hatua hiyo inadhihirisha kuwa umoja huo hivi sasa unaongozwa kwa maelekezo kutoka kwa watu walioko nje ya Jumuiya.
Walisema kuwa wameshangazwa na taarifa zilizotolewa kwa vyombo vya habari na Kamoga kwa kuwa hakuna kikao chochote ambacho wajumbe walikaa na kutoa maamuzi ya kumvua Sitta wadhifa huo.
Katika tamko lao, vijana hao walidai kuwa Kamoga anatumiwa na baadhi ya vigogo ili kuleta mpasuko kwa kuitumia Jumuiya hiyo.
Walisema kama Kamoga alibaini kuwa Sitta alikuwa ametenda makosa, alipaswa kuitisha kikao kama taratibu za chama zinavyosema.
“Kabla ya mambo yote tunamuomba Mwenyekiti athibitishe kauli za Mheshimiwa Samuel Sitta za kusema kakidhalilisha chama na ni lini alipata muda wa kukaa na kamati yake kutoa tamko na kumwandikia barua Mheshimiwa Sitta juu ya kumuengua, na kama atakosa ushahidi basi awajibike, kwa kumuomba msamaha na ajiuzulu, ilieleza sehemu ya tamko hilo.
“Ndugu Kamoga yeye ni mjumbe wa kamati ya siasa ya mkoa, kikao ambacho ni kikubwa na moja ya shughuli zake ni kuangalia na kusimamia shughuli za chama za kila siku kupitia mienendo na matendo ya viongozi. Ni kwa nini asitumie nafasi hiyo kuwasilisha hoja hiyo kwenye vikao kuliko kukurupuka na kusema yanayokuja kichwani mwake katika vyombo vya habari, je, hayo ndiyo maadili ya vijana kwa viongozi wa chama?” Walisisitiza katika tamko ambalo lilisomwa na Mwenyekiti wa UVCCM wa Wilaya ya Uyui, James January.
January alisema wakati anaisoma taarifa hiyo alisema kuwa, kupitia kikao chao cha kamati ya Utekelezaji ya UVCCM Mkoa wa Tabora, walimpigia simu Sitta kumuuliza kama alipewa barua ya kumsimamisha ulezi wa Jumuiya hiyo mkoa wa Tabora na kwamba Sitta alikana kupokea barua yoyote ya kusimamishwa wadhifa wa ulezi wa Jumuiya hiyo.
Wajumbe hao walisema kuwa Kamoga alitumia nafasi yake kutangaza kumsimamisha Sitta na kwamba kitendo hicho kinaonyesha kuwa kuna shinikizo lenye chuki binafsi kwani kama mlezi huyo ana makosa, taratibu zingefuatwa na kumuonya.
Aidha, kupitia kikao hicho cha dharura, wajumbe hao walimuagiza katibu wa Jumuiya hiyo kuitisha vikao vya kamati ya utekelezaji ya mkoa wa Tabora, Baraza la UV-CCM mkoa ili kunusuru mpasuko ambao umejitokeza.
Jumatano wiki hii, baadhi ya magazeti yanayochapishwa kila siku yalimkariri Kamoga akitoa tamko la kusimamishwa kwa Sitta, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Urambo Mashariki kuwa mlezi wa UVCCM Mkoa wa Tabora.
Kamoga alidai kuwa amekiuka moja ya maazimio ya kikao cha Baraza Kuu la UVCCM Taifa kilichofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita ya kuwazuia viongozi wa CCM na serikali kutoa kauli za kukikosoa chama na serikali nje ya vikao.
Kamoga alidai kuwa Sitta alisema kuwa UV-CCM Mkoa wa Tabora inateswa na siasa za makundi na kuushauri umoja huo utumie muda wake kutatua matatizo yake, kauli ambayo Kamoga alisema ni kukidhalilisha chama.
Kamoga alipotafutwa jana kujibu tuhuma dhidi yake, simu yake ya kiganjani haikupatikana.
UVCCM KILIMANJARO WAMKANA KADA
Wakati huo huo, UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro imesema inawasiliana na mwanasheria wa CCM ili kumchukulia hatua za kisheria mtu aliyejitambulisha kuwa ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Paul Makonda, aliyetoa tamko la kupingana na Baraza Kuu la Taifa la Jumuiya hiyo.
Mwenyekiti wa UVCCM mkoani Kilimanjaro, Godliving Moshiu, alitoa tamko hilo jana jioni katika mkutano na waandishi wa habari mjini hapa akifuatana na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu wa UVCCM mkoani humo,Yassin Lema.
Alisema Makonda si mwanachama kwa kuwa alishapoteza sifa ya kuwa mwanachama baada ya kujiunga na Chama Cha Jamii (CCJ) ambacho kilishafutwa na kwamba alidanganya kwa kujitangaza kuwa ni mjumbe wa mkutano mkuu wa umoja huo mkoa na mjumbe wa mkutano mkuu Wilaya ya Moshi mjini.
“Ametuudhi sana tutachukua hatua za kisheria dhidi yake, ametoa tamko la kuichafua Jumuiya na Baraza Kuu la Umoja. Tunawasiliana na mwanasheria wa chama ili apendekeze hatua za kuchukuliwa,” alisema na kuongeza:
“Mwanasheria wetu aliyekuwepo hapa tumempa tamko alilotoa, atapendekeza hatua za kuchukua kwa mujibu wa taaluma ya sheria.”
Alisema umoja huo mkoani humo haupingani na matamko yanayotolewa na UVCCM kwa kazi nzuri wanayoifanya za kuendeleza umoja huo na walichofanya ni kuwapelekea ujumbe viongozi wa chama kuwa tofauti za kichama zinazojitokeza zimalizwe ndani ya chama na si kutoka nje. Kauli ya sasa ya vijana mkoani Tabora na Kilimanjaro inazidi kudhihirisha kuwa mambo si shwari ndani ya UVCCM kutokana na mfululizo wa kauli za malumbano miongoni mwao na dhidi ya viongozi wa chama hicho.
Mwishoni mwa wiki Baraza Kuu lilitoa kauli ya kuwashambulia baadhi ya makada ndani ya chama; kauli ambayo inafanana na ile ya Kamati ya Utekelezaji iliyotolewa kwenye Jukwaa la wahariri jijini Dar es Salaam mwezi uliopita; lakini pia kuna kauli nyingine iliyotolewa na Baraza Kuu la UVCCM Mkoa wa Pwani hivi karibuni likiwalenga baadhi ya makada.
Mlolongo huu wa kunyukana ndani ya UVCCM kunatafsiriwa kama mbinu za siasa za makundi katika mchakato kuelekea uchaguzi mkuu wa chama mwakani, lakini pia katika kujipanga kwa kiti cha urais mwaka 2015.
Imeandikwa na Simon Kabendera, Tabora na Salome Kitomari, Moshi
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment