ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 25, 2011

Vigogo wazua balaa kwa Babu

VIONGOZI mbalimbali wanaokwenda kupata tiba Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Bw. Ambilikile Masapile katika Kijiji cha 
Samunge, Loliondo mkoani Arusha kwa njia za mkato wamesababisha kuibuka kwa vurugu eneo la Mto wa Mbu na kusababisha watu kadhaa kujeruhiwa vibaya.

Hali hiyo imetokana na baada ya wananchi kupandwa na hasira kutokana na magari waliopanda viongozi wa nchi kupita bila kufuata foleni juzi katika eneo hilo ambapo wananchi walishindwa kuvumilia na kuamua kuvamia gari lililohisiwa kubeba viongozi hao na kulisukumia mtaroni, hali iliyosababisha watu kadhaa kuumia vibaya.


Shuhuda wa mkasa huo aliieleza Majira kuwa, viongozi hao wamekuwa wakizungumza na polisi eneo hilo na kuwapatia 'kitu kidogo' na kuruhusiwa kupita huku wengine wakiendelea kusubiri kwa muda mrefu.

Kutokana na baadhi ya magari hayo ya vigogo kufika na kupita katika eneo hilo, wananchi waliamua kwa umoja wao kuvamia gari na kulisukumia mtaroni kwa madai ya kuchoshwa na urasimu unaofanywa na polisi hao.

Chanzo hicho kilielezwa kwamba, urasimu na upendeleo wa polisi unasababisha watu wengi kupoteza maisha kutokana na kukaa katika foleni kwa muda mrefu huku hali zao zikizidi kuwa mbaya kutokana na kukosa huduma muhimu, na wengine kuishiwa dawa walizokuwa wanatumia kutibu maradhi yao ya muda mrefu.

"Hali ni mbaya, viongozi wamekuwa wakitumia njia za panya kupata tiba hii. Wamekuwa wakiwashawishi polisi kwa pesa na kutowazuia, matokeo yake wao ndio wamekuwa wakifika na kupata tiba kwa haraka huku wengine wakiendelea kukaa katika foleni," kilieleza chanzo hicho.

"Nimefika Mtu wa Mbu Jumamosi ambapo ni kilomita 200 mpaka kufika kwa babu, leo (Alhamisi) nipo kilomita tisa kutoka kwa babu na bado nipo katika foleni...., utaratibu umevurugwa na viongozi ndio chanzo kwani wamekuwa wakimiminika kwa wingi," kilieleza chanzo hicho.

Kutoelewana kati ya polisi na raia pia kulitokana na wananchi kutoridhishwa na uamuzi wa askari hao kuruhusu idadi sawa ya magari kutoka Mwanza na Arusha wakati mabasi kutoka Mwanza yanabeba watu wengi ukilinganisha na Land Cruiser ambazo hutoka Arusha. 

Wakati huo huo, kikao cha Kamati za Ulinzi na Usalama za mikoa saba inayopakana na Arusha kilichoketi juzi jijini hapa chini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Bw. William Lukuvi kujadili mustakabali wa tiba hiyo kilishindwa kufikia tamati licha ya kutumia zaidi ya saa 13.

Kukwama huko kumetokana na kamati hiyo kushindwa kuyafanyia maamuzi baadhi ya mambo yanayohusu tiba ya Babu hadi watakapowasiliana naye, hivyo kulazimika kutuma ujumbe maalumu kwake ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Isidore Shirima  huku wajumbe wengine wakiendelea kujadili masuala mengine.

Wajumbe wa kamati hizo za Mikoa ya Shinyanga, Mwanza, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Mara na mwenyeji Arusha walifika jijini hapa tangu juzi, kubwa likiwa ni kujadili mustakabali wa tiba ya mchungaji huo ambapo licha ya ugumu wa kumfikia idadi ya magari ya watu bado inatisha kiasi ni wazi serikali imeshindwa kudhibiti hali hiyo.

 “Kama serikali tumeona upo umuhimu wa kujadiliana na mchungaji Ambilikile kabla ya kutoa maamuzi, hivyo nimetuma ujumbe maalumu kwa mchungaji unaoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha kushauriana baadhi ya masuala hayo kabla hatujafikia mamuzi,” alisema Waziri Lukuvi bila kueleza zaidi. 

Mgonjwa asahau dawa, afa

Kutoka Shinyanga imeripotiwa kuwa Mkazi wa Majengo, Rehema Khamisi (16) aliyekuwa anasumbuliwa na kisukari kwa miaka mitano amefariki dunia baada ya kuacha nyumbani dawa alizokuwa akiendelea nazo na kukimbilia kwa babu kupata kikombe.

Baba wa Marehemu Bw. Khamisi Mamboleo alisema kuwa mtoto wake alimuaga na kumpa ruksa kuwa aende kwa babu kunywa dawa hiyo kwa sababu inaweza kumsaidia kwa sababu ugonjwa huo umemshambulia kwa muda wa miaka mitano, lakini akaacha dawa zake nyumbani, hali   ambayo imechangia kwa kiasi kukibwa kifo chake kwa sababu alikaa siku nne bila kunywa dawa hizo kabla hajamfikia Babu.

Mbunge apeleka wagonjwa

Mbunge wa Kwimba, Bw. Shaif Mansour amefuata nyayo za wabunge wenzake kwa kugharamia usafiri na chakula kuwapeleka baadhi ya wapigakura wake kwenda kupata kikombe kwa Babu.

Miongoni mwa wananchi hao wamo pia baadhhi ya viongozi wa CCM ngazi ya wilaya ya mkoa walioondoka juzi kwa basi kwenda Loliondo kupata dawa.

Kwa mujibu wa mbunge huyo wananchi ambao wamewezeshwa kwa gharama ya sh. 150,000 kila mmoja, ni wenye magonjwa sugu na wasio na uwezo wa kujigharimia usafiri na chakula kutoka katika kata mbalimbali za jimbo hilo.

Imeandaliwa Said Njuki, Arusha; Yusuf Katiba, Dar; Zuhura Semkucha, Shinyanga na Daud Magesa, Mwanza.

No comments: