ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 18, 2011

JK: Kutokujua kusoma, kuandika ni janga


Rais Jakaya Kikwete (kulia) akihoji jambo kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa (kushoto) wakati alipokuwa akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya elimu nchini.

Rais Jakaya Kikwete, amesema tatizo la watu wazima na vijana kutojua kusoma na kuandika ni janga hivyo ameiagiza Wizara ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi, kufanya kila liwezelakano kuondoa aibu hiyo.
Vile vile, ameaiagiza Wizara hiyo kuhakikisha inatatua matatizo ya watumishi wake na ya idara zilizo chini yake badala ya kusubiri watu wagome ndipo kero zitatuliwe.
Aliyasema hayo jana wakati alipotembelea wizara hiyo akiwa katika mfululizo wa ziara zake kutembelea wizara mbalimbali na kuzungumza na watumishi wa wizara hizo.

Kikwete aliyasema hayo alipoingilia kati na kukatisha hotuba ya Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa, baada ya kusema kuwa idadi ya watu wasio jua kusoma na kuandika inaongezeka.
“Kwanini tatizo liongezeke? Mna mkakati gani wa kulishughulikia maana kweli linaongezeka…Hivi karibuni nilikwenda kijiji kwetu akaja kijana mmoja mtoto wa ndugu yangu akasema hajui kusoma na kuandika, nilipomuuliza kwanini akajibu kuwa alipata tamaa kwenda Chalinze kuuza korosho badala ya kwenda shule, kweli hili ni tatizo kubwa na tuweke mikakati tulimalize,” alisisitiza Kikwete.
Alisema kuongezeka kwa tatizo la watu kutokujua kusoma na kuandika limemtisha na litahitaji mkakati maalum wa kulitatua.
Kikwete alisema atapanga ziara kutembelea idara na taasisi zinazohusika na elimu ili kuangalia lilipo tatizo na kuweka mikakati madhubuti ya kuondokana na aibu hiyo.
Alisema atatembelea Baraza la Mitihani (Necta), Taasisi ya Elimu Tanzania, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (Veta), Mamlaka ya Elimu (Tea) na Chuo cha Adem cha Bagamoyo.
Alishauri watu wazima wanaosoma watengwe na wanafunzi wa kawaida ili wasione aibu ya kwenda shule kwani utaratibu wa sasa unaonekana kama unawadhalilisha.
“Huu utaratibu wa kutumia majengo ya shule za msingi kufundishia watu wazima unawaathiri kisaikolojia, maana inawezekana baba anasoma pale na mtoto wake anasoma hapo hapo sasa baba anasoma a, e na mtoto wake anakwenda kumchungulia baba anasoma hayo hayo inaleta tatizo, tafuteni utaratibu mzuri ambao watu wazima watakuwa huru kusoma,” alisema
“Watu wazima jamani lazima wasome kwa faragha maana inawezekana mtoto hajui kama baba yake hajui kusoma na kuandika, sasa akiona baba yake naye anasoma kama yeye inaleta tabu,” alisema na kuagiza wizara iangalie utaratibu mzuri wa kutumia.
Aliiagiza wizara hiyo kuweka mikakati ya kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule za msingi, sekondaeri na elimu ya juu kwa kuwa hivi sasa iko nyuma ya nchi za Uganda na Kenya.
Alisema ingawa Tanzania ni kubwa kuliko nchi hizo mbili, idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu ni ndogo kulinganisha na nchi hizo.
Kuhusu kufeli wanafunzi wengi wa kidato cha nne mwaka jana, Kikwete alisema kumekuwa na malalamiko kuwa mitihani ilikuwa migumu sana na kubadilishwa badilishwa kwa mitaala mara kwa mara.
“Ingawa kuna malalamiko hayo sisemi kwamba mpunguze ugumu wa mitihani wala vile vile msiongeze ugumu na msirahisishe mitihani ilimradi tu watu wafaulu hata kama hawana uwezo wekeni mitihani ya viwango,” alisema.
Alisema wanafunzi wengi wamekuwa wakifanya vibaya katika masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza hivyo aliagiza wizara iangalie namna ya kuongeza ufaulu kwenye masomo hayo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: