Advertisements

Thursday, March 31, 2011

Kamati ya Bunge yaitwisha Serikali mzigo wa Dowans

Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya mahesabu ya Mashirika ya Umma Zitto Kabwe
Patricia Kimelemeta
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imeibebesha Serikali mzigo wa deni la kampuni ya kufua umeme ya Dowans ikisema ndiyo iliyohusika na mkataba wake. Serikali imekuwa ikidai kwamba Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), ndilo linalopaswa kulipa deni hilo.
Agizo hilo la POAC lilitolewa jana katika kikao cha pamoja baina ya Kamati hiyo na makatibu wakuu wa Wizara za Fedha na Uchumi na Nishati na Madini na watendaji wa Tanesco.


Juzi, Kamati hiyo ilishindwa kuthibitisha deni hilo la zaidi ya Sh96 bilioni kutokana na kukosekana kwa ufafanuzi wa uhalali wake na nani anastahili kuilipa kati ya Serikali na Tanesco.Habari kutoka ndani ya kikao hicho cha juzi zililidokeza gazeti hili kuwa tangu kutolewa kwa hukumu iliyotaka Dowans ilipwe fidia kutokana na mkataba wake wa kuzalisha umeme kuvunjwa kiholela, Serikali na Tanesco wamekuwa wakitupiana mpira wa nani anayepaswa kulipa deni hilo.

“Kamati imeshindwa kuthibitisha uhalali wa deni hili na tumewataka makatibu wakuu kufika kesho (Jumatano) ili waweze kutupa ufafanuzi kabla ya kutoa uamuzi,” aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Murtaza Mangungu, aliwaambia waandishi wa habari.

Baada ya mahojiano ya muda baina ya viongozi hao wa Serikali na Tanesco, Kamati hiyo iliitaka Serikali kuilipa Dowans ikiwa mahakama itatoa hukumu ya deni hilo kulipwa.Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zitto Kabwe alisema jana kuwa kwa mujibu wa vitabu vilivyotolewa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), deni la Dowans lilitakiwa kuingizwa kwenye vitabu vya Serikali na si Tanesco.

"... Kwa sababu wao (Serikali) ndiyo walioingia mkataba na kampuni hiyo (Dowans) ya kuwalipa gharama za ununuzi wa umeme," alisema Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema). Zitto alisema Serikali ilipinga suala hilo na Katibu Mkuu (Hazina) alimwandikia CAG, Februari 9, mwaka huu kuwa Tanesco inapaswa kulipa deni hilo. Tanesco nayo iliandika barua ya kupinga kulipa deni hilo jambo ambalo lilisababisha CAG kukataa kusaini vitabu hivyo.

"Ripoti ya CAG iliyotolewa kwenye kamati hii imeonyesha kuwa deni hili linapaswa kuonekana kwenye vitabu vya Serikali na si Tanesco kwa sababu wao (Serikali), ndiyo walioingia mkataba na kampuni hiyo kwa ajili ya kuzalisha umeme. Hivyo deni lake halipaswi kulipwa na Tanesco. Utata huo ulimfanya CAG aombe mwongozo," alieleza Zitto jana.

Kwa mujibu wa Zitto, baada ya malumbano hayo, POAC iliomba kukutana na makatibu wakuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi; na Nishati na Madini ili wajadili suala hilo na kufikia muafaka."Muafaka ni kuwa deni hilo linapaswa kuonekana kwenye vitabu vya Serikali hivyo wao ndiyo wenye jukumu la kulipa deni hilo ikiwa mahakama itatoa hukumu ya kulipwa," alisema Zitto.

Alisema Tanesco haiwezi kulipa deni hilo kwa sababu wao siyo walioingia mkataba na Dowans... "Tanesco haiwezi kubebeshwa mzigo usiowahusu, badala yake Serikali itawajibika yenyewe katika suala hilo ikiwa hukumu yake itatoka."Zitto alisema Tanesco linajiendesha kwa hasara kila mwaka na hiyo inatokana na wadaiwa kushindwa kulipa madeni yao ipasavyo, hivyo kulibebesha mzigo wa kulipa deni kubwa kama la Dowans ni sawa na kulifilisi au kuliua kabisa.

"Mwaka jana, Tanesco lilipata hasara ya Sh5 bilioni. Hii inatokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ya wadaiwa wao kushindwa kulipa madeni yao. Jambo hilo limesababisha shirika lijiendeshe kwa hasara na kutokana na hali hiyo, hawawezi kubebeshwa mzigo huo wa Dowans," aliongeza.

Sakata la malipo kwa kampuni ya Dowans limeibua mjadala mkubwa miongoni mwa jamii hasa ya wasomi, wanasiasa na watu mbalimbali baadhi yao kupinga na wengine kukubaliana nayo.

Mjadala ulipamba moto baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema kueleza kuwa Serikali haina pingamizi na malipo hayo na kwamba tayari imewaagiza wahusika kutekeleza mara moja.

Kauli hiyo ya Werema na ile iliyotolewa na Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani kuunga mkono malipo hayo ziliwafanya wanaharakati wa haki za binadamu kufungua kesi mahakamani kupinga malipo hayo.

CHANZO:MWANANCHI

No comments: