Advertisements

Thursday, March 31, 2011

Mtoto wa Lowassa mbaroni kwa kumgonga trafiki

Na Masau Bwire

MTOTO wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Bw. Bernard Lowassa (30), anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kituo cha Oysterbay, Kinondoni, Dar es Salaam kwa tuhuma za
kumgonga kwa makusudi askari wa Kikosi cha Usalama barabarani E 9320 Koplo Cyprian akiwa katika kutekeleza majukumu ya kazi.

Watu walioshuhudua tukio hilo waliaalaani na kuhoji sababu za mtoto huyo kufanya hivyo, wengine wakienda mbali zaidi wakidai pengine alifanya hivyo kwa kujiona hawezi kubanwa na sheria kwa kuwa ni mtoto
wa kigogo.
 

Tuko hilo lilitokea juzi saa 1 jioni eneo la Namanga, Oysterbay  katika eneo la taa za kuongoza magari. 

Akiendesha gari lenye namba za usajili T 573 BQV, Corona Primio, kutoka Msasani kwenda Morocco, alikaidi utaratibu wa trafiki huyo wa kuruhusu magari kupita kwa awamu kwa kulazimisha kupita kabla hajaruhusiwa.

Koplo Cyprian pengine kwa lengo la kuepusha magari kugongana na kutaka kuchukua hatua ukaidi wa Bernard, alilazimika kumzuia asipite lakini, bila kujali wala woga, aliendesha gari lake na kumgonga katika mguu na kumsukuma.

Mshuhuda walioshuhudia tukio hilo walisema askari huyo aling'ang'ania gari hilo hadi madereva wengine walipomuokoa kwa kulizuia gari la kijana huyo baada ya kusimama mbele ya gari lake.

Baada ya madereva wengine ambao nao walikuwa wakisubiri kuruhusiwa kupita katika taa hizo kukerwa na kitendo alichokifanya Bernard kumugonga kwa makusudi.

Watu wakiwa na hasira nusura wamshushie kipigo mtoto huyo lakini, askari huyo liwasihi wasifanye hivyo bali waiache sheria ichukue mkondo wake.

Madereva hao walitii kauli ya askari huyo aliyekuwa akichechemea na kulia kwa uchungu kutokana na maumivu makali kutoka katika mguu 

Polisi wa kituo hicho walifika katika eneo hilo na kumchukua mzobemzobe mtoto huyo hadi Kituo cha Polisi Oysterbay, na habari zaidi zinasema baadaye aliachiwa kwa dhamana kwa sharti la kutakiwa kuripoti kituoni leo.

Kamanda wa Jeshi la polisi, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni Bw. Charles Kenyela alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba koplo Cyprian alipelekwa Hospitali ya Mwananyamala kwa matibabu.

Kamanda Kenyela alionesha kusikitishwa na kitendo hicho cha mtu kudhani kuwa yuko juu ya sheria.

"Nimesikitishwa na kitendo hicho, mtu anaamua kutokufuata sheria za
barabarani na kudharau kazi ya askari wakati wa kutekeleza majukumu yao.

"Kijana huyo amekamatwa na anahojiwa na polisi, tuiachie sheria ichukue mkondo wake na kuamua cha kufanya kuhusu kitendo hicho cha uvunjifu wa sheria kilichofanywa na kijana huyo wa Lowassa," alisema Kamanda Kenyela.

Askari wa vyeo vya chini wameonesha wasiwasi kuhusu hatua za kisheria zitakazochukuliwa dhidi ya mtoto huyo wa kigogo wakidai, kumekuwa na kawaida ya vigogo kulindana na kupoteza haki ya mtu
wa hali ya chini. 

Mmoja ya askari ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini alisema kwamba ana uhakika kuwa mtoto huyo atalindwa, hatafanywa chochote, zaidi kulazimishwa askari huyo
 kumsamehe.


CHANZO:MAJIRA

No comments: