ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 11, 2011

Makombora 2 yakutwa ndani ya nyumba

MAKOMBORA mawili yaliyolipuka kwenye Kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Gongo la Mboto wilayani Ilala, Dar es Salaam, yamegundulika yamejichimbia ndani ya nyumba mbili katika vitongoji vya Kimara Baruti na Mbezi kwa Musuguri wilayani Kinondoni. 

Kutokana na hali hiyo, wanajeshi wanaendelea na jitihada za kuyatoa huku kazi ya uhakiki kwa ajili ya malipo ya wananchi walioathirika na mabomu hayo, inatarajia kukamilika Jumapili na ripoti kukabidhiwa kwa Kaimu Mkuu wa Mkoa, wiki ijayo.
 

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Sadiki alisema jana kuwa wanajeshi wanaendelea kukusanya mabomu yaliyotapakaa sehemu mbalimbali Dar es Salaam, na hayo mawili ya Kimara Baruti na Mbezi kwa Musuguri, yamegundulika wiki hii yakiwa ndani ya nyumba hizo. 

Alisema kati ya nyumba hizo mbili, moja mabomu yaliingia kwa kutumia upande mmoja wa nyumba na lingine liko kwenye nyumba ambayo ilikuwa haijahamiwa na wamiliki. 

Akizungumzia uhakiki kwa ajili ya malipo, Sadiki ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, alisema walitarajia kumaliza mapema, lakini wanacheleweshwa na wanaohakikiwa ikiwa ni pamoja na kurejea kwa waliokuwa wamekimbia na kutohakikiwa. 

Alisema awali walijua nyumba zilizoharibiwa kabisa ni 69, lakini katika uhakiki unaoendelea, zimeongezeka na kusema katika kuhakikisha wanamaliza uhakiki haraka vikundi vya uhakiki vilivyomaliza upande wao vimejumlishwa katika sehemu ambazo hazijamaliza, hivyo uhakiki na kuandika ripoti utakamilika Jumapili. 

Alisema watu waliopopteza maisha kutokana na mabomu hayo imeongezeka na kufikia 30 baada ya mgonjwa mwingine kufariki dunia Jumanne wiki hii katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuzikwa siku iliyofuata. 

Alisema hadi jana wamebaki majeruhi 12 ambapo wanane wako Muhimbili na wanne wako katika Kitengo cha Mifupa (MOI). 

Awali, akipokea msaada wa vyakula kwa ajili ya waathirika wa mabomu hayo vyenye thamani ya Sh milioni tatu kutoka Benki ya Twiga Bancorp uliokabidhiwa na Mkuu wa Idara ya Uendeshaji, Richard Kombole, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Leonidas Gama alisema milango iko wazi kwa ye yote anayetaka kuhakiki mfumo wa ugawaji wa misaada hiyo. 

Katika hatua nyingine, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Ali Mwinyi alikabidhi msaada wa Sh milioni 28 kwa Kamanda wa Kikosi cha 511 Gongo la Mboto, Kanali Aloyce Mwanjile kwa ajili ya kusaidia wanajeshi makapera 78 na familia nane za wanajeshi walioathirika na mabomu hayo. 

Fedha hizo taslimu zilitolewa na Jeshi la Ulinzi Sh milioni 10, JKT Sh milioni tano, Mzinga Sh milioni nne, zote zikiwa taasisi chini ya wizara zake. 

Pia alipokea fedha taslimu toka Jumuiya ya Kiislamu ya Istiqaama iliyotoa Sh milioni mbili, Mkurugenzi Mtendaji wa Maxcom Africa, Juma Furaji Sh milioni tano na Mkurugenzi wa Comfix Engeneering, Hashim Lema Sh milioni mbili. 

Dk. Mwinyi alishukuru waliotoa msaada huo kwa wanajeshi kwani watu wengi walisahau kama kuna wanajeshi walioathirika na kutoa misaada mingi kwa raia huku akialika makundi mengine kuwasaidia wanajeshi walioathirika. 

Wakati huo huo, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), leo katika Kamandi ya Ulinzi wa Anga itafanya mazoezi ya kurusha ndegevita katika eneo la Dar es Salaam na Pwani. 

“Mazoezi haya ambayo ni muendelezo wa mazoezi yaliyokwishafanyika katika maeneo mengine nchini, yataanza saa tatu asubuhi hadi saa saba mchana. Hivyo JWTZ linaviomba vyombo vya habari kuwataarifu wanachi wa maeneo husika kuwa mazoezi hayo ni ya kawaida na wasiwe na hofu yoyote,” ilieleza taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano Makao Makuu ya Jeshi jana.


CHANZO:HABARI LEO

No comments: