ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 11, 2011

Penzi lisilo na wivu

HAYA tena, tumekutana kwenye kona yetu ya mapenzi na uhusiano hususan kwa wapendanao. Mu hali gani? Mi mzima wa afya namshukuru Mungu kuweza kunipa nguvu za kuweza kuufikisha ujumbe kwenu ninyi wapenzi wa kona hii.

Kama ada tunaendelea na mada yetu ambayo leo inatimiza mwezi na nusu. Napenda kuwapongeza kwa kuwa nami kwa muda wote huo. Tunaendeleea:


Leo tunaliangalia fungu la mwisho ambalo ndilo litakalo hitimisha makundi yetu nalo ni kundi la penzi liitwalo lipo lipo tu. Ushaanza kujiuliza ni penzi gani hili ambalo lipo lipo tu?

Hili penzi huwa la ajabu, halina gharama wala wivu, najua nimekuacha njia panda na kujiuliza kuna penzi gani duniani lisilo na wivu wala gharama?

Penzi hili lipo hivi unakuwa na mwenza wako huyo njiani na kuanzisha uhusiano, wakati huo labda wewe una mpenzi wako na kumfahamisha lakini mwenzio anakuwa radhi kuwa na wewe japo una mpenzi.

Penzi kama hili halina kanuni wala kufuatiliana mkikutana sawa msipokutana sawa. Vile vile unaweza kuwa na mpenzi ambaye penzi lenu labda lilikuwa shuleni, kitongoji, mkoa au nchi fulani lakini baada ya muda mkapoteana huku mkiwa bado mnapendana.

Mnapokutana kwa mara nyingine hujikuta mnaendeleza mapenzi yenu hata kama mmoja au wote mna wenza wenu.
Penzi hili huwa sawa na mpira wa gombania goli, kwa kuwa mama huruma au baba huruma wa kugawa penzi kwa kila aliye mpenzi wako wa siku za nyuma.

Hasara za penzi la aina hii ni kubwa kwa kuwa uliachana na mpenzio wa zamani bila kujua alipitia hatua gani mpaka kukutana na wewe tena.

Japo kwa upande wako utaona penzi hilo sawa na nyama ya mishikaki haishibishi, kwa kujua hata bila kula haikupunguzii chochote, pia pale mpenzi wako anapokuwa mbali mkikutana mnaendeleza mambo yenu kama kawaida.

Penzi lenu linakuwepo pale mnapoonana tu na si kwa ajili ya kujenga bali kulifanya kama burudani kwenu. Lakini je, unajuaje huyo mpenzi wako ana marafiki wangapi? Anatumia kinga? Huwezi kujua wewe unalifurahia kwa vile halikugharimu chochote au unaona raha kila mkikutana unapata pombe au nyama choma, mkiachana eneo husika anakuacha unakuwa huru.

Starehe ya muda mfupi inaweza kukufanya ujutie maisha yako yote yaliyobakia duniani. Hii huipenda wanawake wasiopenda kuolewa au wanaume wakware kwa kuona ni sehemu ya kujiburudisha.

Mpenzio wa zamani haukatazwi kurudiana naye kama hujapata mtu lakini la muhimu mzijue afya zenu.

Nina imani kwa maelezo mafupi nitakuwa nimeeleweka. Kama kuna mtu anakumbuka kitu ambacho nimekisahau si vibaya kunikumbusha ili nikifafanue kwa upana zaidi.

Tukutane wiki ijayo kumalizia mada yetu kwa kuangalia upande wa pili wa shilingi ili ujijue na kumjua mpenzi wako yupo kundi gani.

No comments: