Advertisements

Thursday, March 31, 2011

Tegete aivuta mkia Simba kileleni



Jerry Tegete alifunga mara mbili na kufikisha jumla ya mabao yake msimu huu kuwa tisa wakati alipoisaidia timu yake ya Yanga kushinda mtihani mgumu dhidi ya Azam FC kwa kuichapa mabao 2-1 na kupunguza pengo la pointi kutoka kwa vinara wa Ligi Kuu ya Bara Simba kuwa pointi 2.
Kwa ushindi huo Yanga imefikisha pointi 43, mbili nyuma ya watetezi Simba wenye 45, huku mechi mbili zikiwa zimebaki msimu kumalizika.

Kipigo kwa Azam kinamaanisha kwamba wazalishaji hao wa 'lambalamba' walio katika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 37, mafanikio ya juu kabisa wanayoweza kuyapata ni kumaliza wa pili, iwapo Yanga watafungwa mechi zote mbili zilizosalia na wao watashinda zote.
Yanga walilazimika kuzinduka kutoka nyuma kufuatia goli la mapema lililofungwa na John Bocco aliyewashangaza Wana Jangwani katika dakika ya 4 baada ya kuuwahi mpira uliookolewa vibaya na beki wa kati wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' na kufanya jumla ya mabao yake ya ligi msimu huu kuwa 10, matatu nyuma ya vinara Mrisho Ngassa wa Azam na Gaudence Mwaikimba wa Kagera Sugar wenye magoli 13 kila mmoja.   
Dakika mbili kabla ya mapumziko, Tegete alirejesha matumaini ya Yanga kwenye mbio za ubingwa wakati alipoisawazishia timu yake goli hilo kwa "kumvisha kanzu" kipa wa Azam, Vladimir Niyonkuru kabla ya kwenda kufunga kati lango tupu. 
Tegete alikamilisha siku yake nzuri kwa kufunga goli la pili kwake na kwa timu yake katika dakika ya 65 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa wa Azam, alishindwa "kumeza" shuti la mshambuliaji Mzambia, Davis Mwape. 
Kulikuwa na kosa-kosa kadhaa jana na Yanga wangeweza kukomboa goli mapema zaidi kama Tegete angeukimbilia mpira badala ya "kushangaa" shuti la Mwape lililogonga mwamba na kurejea uwanjani katika dakika ya 12.  
Kipa wa Azam alikuwa makini tena katika dakika ya 29 wakati alipopangulia nje ya uwanja shuti la Mwape, ambaye ameshindwa kuongeza idadi ya magoli yake matano aliyoyafunga katika mechi zake tatu za kwanza tangu alipojiunga na Yanga katika mzunguko wa pili wa ligi kuu.  
Mchezaji aliyetokea benchi, Kally Ongalla angeweza kuisawazishia Azam katika dakika ya 82 kama angetulia lakini alishindwa kuelekeza kichwa langoni mwa Yanga, ambayo ilimuanzisha kipa mzungu Ivan Knezevic wa Serbia, ambaye aliripoti kuibiwa vifaa vyake na pesa akiwa katika jengo la Yanga analoishi wiki hii.   
Nyota wa zamani wa Yanga, Ngassa hakuwa na mengi ya kutisha kwa klabu yake ya zamani.
Kutoka mjini Arusha, Woinde Shizza anaripoti kuwa wenyeji AFC ambao wameshashuka daraja pamoja na Majimaji ya Songea, walizinduka wakati kumeshakucha katika sare ya 1-1 dhidi ya Mtibwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Nyota wa zamani wa Mtibwa, Abdallah Juma aliifungia timu yake ya sasa ya AFC wakati goli la Mtibwa lilifungwa na Monja Liseki. 
Vikosi katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam vilikuwa; Yanga: Ivan Knezevic, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Nadir Haroub 'Cannavaro', Chacha Marwa, Juma Seif/ Omega Seme (dk.56), Fred Mbuna, Nurdin Bakari, Davis Mwape, Jerryson Tegete, Kigi Makassy.
Azam: Vladimir Niyonkuru, Ibrahim Shikanda, Malika Ndeule/ Himid Mao Mkami, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Mutesa Mafisango, Mrisho Ngassa, Jabir Aziz, John Bocco 'Adebayor', Ramadhani Chombo 'Redondo', Suleiman Kassim/ Kally Ongalla (dk. 71).
CHANZO: NIPASHE

No comments: