Advertisements

Thursday, March 31, 2011

Mamilioni aliyokusanya Babu Loliondo yatajwa



Wakati Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, likitangaza kujenga ukumbi wa kupokea wagonjwa kijijini Samunge, Loliondo kwa Mchungaji mstaafu Ambilikile Masapile, fedha kamili ambayo imekusanywa katika utoaji huduma hiyo imetangazwa.
Kwa mujibu wa Askofu wa KKKT Dayosisi Kaskazini Kati, Thomas Laizer, kiasi kilichokusanywa hadi jana kutokana na malipo ya Sh. 500 kwa kila kikombe anachopewa mgonjwa, ni Sh. milioni 50.

Kutokana na sehemu ya fedha hizo, Kanisa .
litatumia zaidi ya Sh. milioni 100 kwa kujenga jengo la mviringo kwa ajili ya kupumzikia wagonjwa zaidi ya 700, wanaokwenda kupata matibabu kwa Babu huko Loliondo.
Aidha, Kanisa hilo limeiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa kuwasaidia wananchi wa kijiji hicho kwa kupeleka chakula ambacho wamekimaliza katika kukarimu wagonjwa wanaoingia kijijini hapo zaidi ya 1,000 kwa siku.
Akitoa taarifa na maelekezo kuhusu tiba na maombi ya Mchungaji Masapile jana, Askofu Laizer, alisema kuwa jengo hilo litapauliwa vizuri na kuwekwa nguzo bila ukuta.
Alisema litakuwa na vyumba vya kuchemshia dawa na chumba cha kuhifadhia dawa ukumbini, pamoja na kuwekwa jukwaa la kutolea huduma hiyo katika mistari mitano ya watu 20.
Lakini katika kila mstari kutakuwa na Mchungaji, ambaye atagawa dawa aliyobariki Babu na kuwekwa kwenye kikombe tayari kwa kutumiwa na kila mchungaji atakuwa na uwezo wa kuhudumia watu 100 kwa kipindi kisichozidi dakika kumi, ili kwa siku wahudumiwe watu 1,500 hadi 2,000 ili mchungaji huyu aweze kupumzika,” alisema Askofu Laizer.
Alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo utaanza hivi karibuni katika eneo  lililopatikana jirani na nyumbani kwa Babu na tayari michoro ya jengo hilo inakaribia kumalizika.
Akifafanua kuhusu Sh. Milioni 50 zilizikusanywa, alisema kati ya hizo Babu ana Sh. milioni 10 inayotokana na Sh. 100 katika Sh. 500 anazopokea.
Sh. milioni 20 ni fedha za kanisa zilizotokana na makusanyo ya Sh. 200 katika ya Sh.500 na Sh. milioni 20 nyingine ni za wafanyakazi ambao wanamsaidia Babu kuchimba dawa na kuchemsha na shughuli nyingine, ambazo nazo ni sehemu ya Sh. 500.
Aidha, aliomba serikali kupitia Kitengo cha Maafa, watu binafsi na makanisa mbalimbali kuchangia ujenzi huo kupitia akaunti maalum kwenye benki ya CRDB, yenye namba 0150036432600 yenye jina la KKKT  DKAK, Huduma ya maombi na tiba Mchungaji  Masapile.
Alisema fedha hiyo itatumika kujenga jengo hilo na kupanua huduma zitakazohitajika siku za usoni, kwani Mchungaji huyo amefunuliwa kuwa kwa sasa hao watu sawa na bure, baadaye watajitokeza watu wengi zaidi ya hao, hivyo kama Kanisa lazima lijiandae.

HALMASHAURI YAFANYA UKARABATI
Halimashauri ya Jiji la Arusha imeanza ukarabati katika eneo litakalotumiwa na wananchi wanaokwenda kwa Masapile.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Estomih Chang’a, alisema ukarabati wa eneo hilo lililoko jirani na Soko la Kilombero unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh. milioni 10.
Chang’a alisema miongoni mwa mambo yatakapewa kipaumbele katika ukarabati huo ni pamoja na kuhakikisha kuwa huduma ya vyoo, maji na umeme inapatikana katika kituo hicho.
Alisema tayari wameshaweka mahema mawili yatakayotumika kwa ajili ya huduma mbalimbali zitakazotolewa na wadau watakaohusika katika usimamizi wa usafirishaji huo ikiwemo Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
Chang’a alisema awali kituo hicho kilipangwa kuwekwa katika uwanja wa NMC, lakini kutokana na kutokuwa na miundombinu inyoaweza kuhimili huduma hiyo, waliamua kukihamishia katika eneo hilo.
 NJIA ZA PANYA ZATUMIKA
Katika hatua nyingine, msongamano wa wagonjwa nyumbani kwa Mchungaji Masapile bado ni kubwa kutokana na baadhi ya wananchi kukaidi maelekezo yaliyotolewa na kuendelea kwenda kijijini hapo kwa kutumia njia za panya.
Baadhi ya walioshuhudia hali hiyo ni Mama Mtemvu ambaye alisema pamoja na Babu na serikali kuwaomba wananchi kusubiri kwa muda ili msongamano upungue,  bado watu wameendelea kwenda kwa kutumia njia za panya hasa wakati wa usiku.
Alisema hali hiyo imesababisha foleni kutopungua.
DC ATOA ANGALIZO
Mkuu wa wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali, alithibitisha kuwepo  kwa watu wanaotumia njia za panya kwenda kwa Babu na kuwataka waheshimu maelekezo yaliyotolewa.
Ni kweli kuna baadhi ya watu wanajipenyeza na kupita porini nyakati za usiku, lakini ni vyema wakajua kuwa Babu alishasema kuwa mtu atakayetumia hila kupata dawa yake atakuwa amekunywa maji na wala sio dawa hivyo haiwezi kumsadia,“ alisema Wawa Lali.

RC MWANZA ATANGAZA UTARATIBU
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro, amepiga marufuku malori na magari madogo kusafirisha watu kwenda Loliondo kupata tiba huku akitangaza utaratibu mpya wa kufikia huduma hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu utaratibu mpya wa kuwawezesha watu kwenda kwa Babu kwa utaratibu maalum utakaowawezesha kwenda na kupata kikombe haraka.Kandoro alisema kuwa ni marufuku kutumia usafiri wa malori au magari madogo yasiyo na 4 wheel kwenda Loliondo.
Kandoro alilotoa agizo hilo mbele ya mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Hamis Amanzi; Afisa Usalama wa Mkoa, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mwanza, Kaimu Kamanda wa Polisi wa mkoa, wawakilishi wa wenye mabasi ya usafiri wa mikoani na waandishi wa habari.
Alisema Serikali iliunda kamati iliyohusisha wakuu wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, ikiwemo Kigoma na kwa pamoja walikubaliana kuweka vituo vya kuratibu magari pamoja na orodha ya watu wanaokwenda Samunge ili wapate tiba haraka na kurejea salama.
Aliongeza kuwa magari yote yatakayokwenda Loliondo yanatakiwa kukaguliwa na Jeshi la Polisi na baadaye kupewa leseni za muda na Sumatra.
Pia mabasi yatakayokuwa na kibali yatatakiwa kuorodhesha majina ya abiria wao wote na kuacha fomu hiyo katika geti la Magu na watapatiwa kadi maalum ya rangi nyekundu kwa mabasi yote yanayotokea Kanda ya Ziwa.
DAWA  YACHUNGUZWA
Wakati huo huo, Serikali imechukua sampuli ya dawa inayotolewa na mwanamke anayedai kutibu magonjwa sugu, Magreth Mutalemwa (40), kwa ajili ya kuifanyia uchunguzi wa kina na kufahamu iwapo haina madhara kwa binadamu.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Abeid Mwinyimsa, alisema dawa hiyo inapaswa kuangaliwa kitaalam zaidi na hatimaye kufahamu kama ina madhara ama la.
Alisema pamoja na kuichunguza, pia kuna mambo ya msingi yanayopaswa kuangaliwa na kwamba ameunda timu maalum ya kuangalia masuala ya usalama na kiafya kwa dawa hiyo inayoendelea kutolewa kwa wananchi.
Alisema serikali pia itamsaidia mwanamke huyo kupata vifaa zaidi vya kufanyia kazi kama vikombe na sufuria kwa sababu kumekuwa na mrundikano mkubwa wa watu katika eneo hilo na hivyo kuleta wasiwasi wa usalama wa afya za wanaofuata huduma.
Mutalemwa amekuwa akihudumia takriban watu 400 kwa siku na kwamba idadi ya watu imekuwa ikiongezeka kila siku wengine wakitoka mikoa ya jirani.
Tayari serikali imeagiza barabara iendayo katika nyumba anayoitumia kutoa dawa itengenezwe ili kuhakikisha kuwa inapitika kwa urahisi na kwamba tiba hiyo inaendelea kutolewa katika mazingira ya amani na utulivu.
Imeandikwa na Cynthia Mwilolezi, John Ngunge na Asraji Mvungi Arusha; Lucas Macha, Tabora na Cosmas Mlekani, Mwanza
CHANZO: NIPASHE

No comments: