Advertisements

Thursday, March 31, 2011

Wabakaji Zanzibar kuhasiwa

WATU watakaothibitika kubaka visiwani Zanzibar huenda wakahasiwa, kama sheria iliyotungwa itaidhinishwa na Rais. 

Hiyo ni katika juhudi ya Serikali kukabiliana na vitendo vya unyanyasaji dhidi ya haki za watoto, hivyo kuamua kupitisha sheria inayotoa adhabu hiyo.
 

Sheria hiyo ilipitishwa juzi na Baraza la Wawakilishi, kama njia ya kulinda haki za kundi hilo itakayodhibiti vitendo vya unyanyasaji, vinavyodaiwa kuongezeka visiwani hapa, licha ya kuwapo adhabu ya vifungo kwa wanaopatikana na hatia. 

Wakati wa kujadili muswada wa sheria hiyo kabla ya kuipitisha, Mwakilishi wa Chonga kwa tiketi ya CUF, Abdallah Juma Abdallah, alisema, “adhabu ya kifungo imeonekana kushindwa kukomesha vitendo vya uvunjaji wa haki za watoto, kwa kuwa unyanyasaji dhidi yao unaendelea… 

“Hivyo, itakuwa vema endapo adhabu kali kama vile kuhasiwa kwa watakaothibitika kujihusisha na ubakaji wa watoto, zitaruhusiwa kisheria ili kudhibiti vitendo hivyo.” 

Wakati Abdallah akisema hivyo, Mwakilishi wa Matembwe, Abdi Mosi Kombo (CCM), alilaumu kupuuzwa kwa sheria za kiislamu visiwani hapa akisema ndiko kunachangia uvunjaji wa haki za watoto, ukiwamo unyanyasaji na udhalilishaji. 

Wakati wa majadiliano hayo, wawakilishi hao walithibitisha kukithiri kwa vitendo hivyo, huku wakilaumu wazazi na jamii kwa jumla kuchangia kuongezeka kwake kutokana na uzembe wanaouonesha katika matunzo ya watoto wao. 

Vile vile, waliilaumu Serikali kwa kufumbia macho na kushindwa kusimamia kufutwa kwa biashara za baa na klabu za usiku katika maeneo ya makazi ya watu, ambazo walidai zinaharibu watoto. 

“Uwepo wa baa na klabu za usiku katika maeneo ya makazi ya watu na kushindwa kwa wazazi na jamii kutekeleza wajibu wao juu ya malezi bora ya watoto wao, kunachangia kuwaharibu na kuchochea kuongezeka kwa vitendo viovu dhidi ya kundi hilo, kama vile ubakaji na kutelekezwa. 

“Bila kujali kama ni mtoto wa kumzaa au la, kila mtu ana wajibu wa kulinda haki za mtoto, siku hizi wazazi wamebadilika, kila mtu anaangalia mtoto wake pekee wakati zamani kila mzazi aliwajibika kwa kila mtoto,” Subeit Khamis Faki (CUF- Micheweni) alisema. 

Sheria hiyo imeidhinisha kuanzishwa kwa mahakama za watoto, matunzo na ulinzi wa watoto wasio na makazi maalumu na kuruhusu mtu mwenye sifa za kuasili mtoto na kumpa malezi kama mzazi, au mlezi kufanya hivyo kwa kuhakikisha anapata matunzo stahiki. 

Hata hivyo, kipengele cha 76 cha sheria hiyo, kinachozungumzia kuasili watoto hakikuwaridhisha wawakilishi wote.

Mwakilishi wa Chonga, Abdallah, ndiye alikuwa wa kwanza kupinga kipengele hicho kwa maelezo kuwa kinakiuka sheria za dini ya kiislamu. 

Aidha, licha ya kupinga huko, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Omar Makungu, Waziri mwenye dhamana ya maendeleo ya watoto visiwani hapa, Zainab Mohammed na Waziri wa Masuala ya Sheria na Katiba, Abubakari Khamis Bakari, walisimama kila mara kutetea sheria hiyo na kusema inahusu wasio Waislamu pekee. 

“Sheria zinatungwa kwa ajili ya watu wote, lakini hii ya kuasili watoto itahusu wasio Waislamu. Zanzibar ina watu wanaoamini dini tofauti hasa Waislamu na Wakristo, hivyo sheria hiyo itahusu zaidi wasio Waislamu,” alisema Waziri wa Sheria. 

Waziri wa Maendeleo ya Watoto alimalizia kwa kusema: “Ninapinga vikali biashara ya baa na mitandao ya intaneti inayoonesha mambo mabaya hasa katika makazi ya watu, nawaomba wazazi na wanajamii tushirikiane kukomesha uvunjaji wa haki za watoto”.


CHANZO:HABARI lEO

No comments: