.jpg)
Baadhi ya mabasi ya daladala yanayosafirisha abiria katika njia mbalimbali za Jiji la Mwanza, yamepuuza agizo la Mkuu wa Mkoa huo, Abbas Kandoro, la kuzuia mabasi hayo aina ya Hiace kupeleka abiria kwenda kupata tiba ya Mchungaji, Ambilikile Masapile katika kijiji cha Samunge-Loliondo mkoa wa Arusha.
Kandoro wiki iliyopita wakati akielezea utaratibu mpya wa kwenda kwa Babu ambao utasaidia kupunguza msongamano na kuwafanya watu kwenda kupata tiba bila usumbufu, alipiga marufuku mabasi madogo, malori na magari mengine yote yasiyo na 4 wheel, kwenda Loliondo.
Uchunguzi wa NIPASHE jana kuanzia Bunda, Nata, Mugumu hadi Robanda wilayani Serengeti mkoani Mara, ulibaini kuwa baadhi ya mabasi ya daladala yanayofanya safari zake katika maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza, sasa yamekimbilia kupeleka abiria kwa Babu kwani wameona inawapatia kipato zaidi kuliko ile ya daladala.
Baadhi ya mabasi hayo ya daladala yanayojulikana sana kama vipanya, yalionekana juzi majira ya saa 4:00 usiku yakiegesha katika eneo la Lubanda wilayani Serengeti vikisubiri kuche kabla ya kuendelea na safari zao kupeleka abiria kwa Babu.
Pia, Hiace nyingine zilionekana jana njiani, baadhi yao zkiwa zimeharibika kutokana na ubovu wa barabara na kushindwa kumudu hali ya barabara na kuwafanya abiria kusota baadhi yao porini wakisubiri gari hizo zitengenezwe, ili waendelee na safari.
Dereva mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja ya Joachim, alisema safari ya Samunge inalipa zaidi kuliko tripu za jijini Mwanza, hasa kipindi hiki ambacho msungumano wa kwenda kwa Babu ukiwa umepungua sana na hivyo magari kutochukua muda mrefu. “Kaka trip za kwenda kwa Babu zinalipa sana mfano ukipata vichwa vyako 14 halafu kila kimoja ukakitoza Sh. 80,000 kutoka Mwanza, unakusanya Sh. 1,120,000 na unakwenda leo (jana), na kesho (leo), unarudi sasa hapo Mungu akupe nini au unataka bahati gani,” alisema dereva huyo.
Magari hayo inadaiwa pia kuwa mbali na kukiuka agizo la Kandoro kutaka yale tu yenye 4 wheel ndio yapeleke abiria Loliondo, baadhi yake hayakuwahi kukaguliwa na polisi wa usalama barabarani wala hayakupewa leseni za muda na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Baharini (Sumatra), kama ilivyoagizwa na Kandoro.
Baadhi ya vipanya vilivyoonekena vikiegesha Lubanda juzi usiku tayari kwa ajili ya kusubiri kuche ili vipeleke abiria hao kwa Babu ni vile vyenye namba T 969 BEW kilichondikwa Igoma-Bwiru, kingine ni kile chenye namba T 226 BES cha kwenda Igoma Bwiru nacho, huku kingine ni kile chenye namba T 302 AWN cha Igoma Ilemela na kile cha Maduka Tisa Nyasaka chenye namba za usajili T 307 BMM.
Kandoro wakati akitangaza utaratibu mpya kwa watu kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, alisema mbali na magari ya 4 wheel, magari mengine yatakayorusiwa kupeleka abiria huko ni mabasi baada ya kukaguliwa na polisi wa usalama barabarani kitengo cha ukaguzi na kupewa leseni za muda zitakazowawezesha kwenda katika njia hiyo mpya.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment