Ajali zaua 10 Morogoro
Imo ya Sumry, Hiace.jpg)
Mikoa ya Morogoro na Pwani katika kipindi cha wiki mbili imeshuhudia maafa makubwa yaliyosababishwa na ajali za barabarani na kupoteza nguvu kazi ya watu 43 bila sababu.
Umma ukiwa na majonzi ya ajali hizi tatu mbaya za mwezi uliopita ambazo zilitokea Morogoro na Pwani, jana na juzi mkoani Morogoro, ajali tatu tofauti zimeua tena watu 10 zikihusisha mabasi mawili ambayo yaligongana na magari mengine katika ajali mbili tofauti.
Ajali hizi zikijumlishwa na zile za mwezi uliopita kuanzia ile ya wasanii iliyotokea Morogoro Machi 21, ikifuatiwa na nyingine ya Machi 23, mkoani humo na kisha mbili za Machi 26 zilizotokea Pwani na kuua watu 17, inakamilisha watu 43 waliopoteza maisha.
Katika ajali za juzi na jana, mbali ya vifo vya watu 10 watu wengine 14 walijeruhiwa.
Juzi basi la Sumry liligongana na gari ndogo uso kwa uso katika maeneo ya Maseyu na kusababisha vifo vya watu watatu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro, ACP Adolphina Chialo, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea juzi saa 12.45 jioni eneo la Maseyu wilaya ya Morogoro.
Kamanda Chialo alisema gari lenye namba T 924 AHJ Nissan pick-up lililokuwa likiendeshwa na Athuman Mustafa (34), liligongana na basi la Sumry lenye namba za usajili T 608 BEW lililokuwa likitokea Mwanza kwenda Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu watatu waliokuwa katika gari ndogo akiwemo dereva wake.
Aliwataja waliokufa katika ajali hiyo ni dereva wa pick-up Athumani Mustapha, mkazi wa Keko Dar es Salaam; Yona Hamis (37), mkazi wa wilaya ya Manyoni mkoani Singida na mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Lilian.
Kamanda Chialo alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi kwa madereva wote wawili na kuongeza kuwa dereva wa basi hilo aliyetambulika kwa jina la Samson Ibrahimu (50), mkazi wa Dar es Salaam alitoroka baada ya ajali kutokea na polisi wanaendelea kumtafuta.
Kwa upande wa abiria katika basi la Sumry, alisema hakuna aliyejeruhiwa na wote jana walipatiwa usafiri kuendelea na safari yao.
Katika ajali ya pili, watu sita walifariki dunia na wengine 12 kujeruhiwa vibaya jana saa 11:00 alfajiri katika eneo la Mkambarani, Mikese wilaya ya Morogoro baada ya gari aina ya Toyota Hiace namba T 908 BCM kugongana na lori aina ya Scania namba T251 BBG yenye tela namba T 812 BEP.
Hiace ilikuwa imewabeba wafanyabiashara wadogo wa mboga kutoka Mikese kwenda Morogoro mjini wakati Scania ilikuwa ikitoka Morogoro kwenda Dar es Salaam.
Waliofariki katika ajali hiyo ni dereva wa Hiace, Saidi Nyangaji (42), Nimley Salum (28), Suleiman Gogo (55), Rogasi David (35), Athumani Sadick (miezi minane) na Phoeby Manda (50), wote wakazi wa Mkambarani, Mikese.
Majeruhi wa ajali hiyo ni Mariam Hassan (22), Rehema Hussein (55), Zulpha Omary (22), Mauwa Athuman, Salma Salum, Nasma Rajabu (32), Safina Halali (mwezi mmoja), Tausi Rashid (32) na Hadija Ally (40), wote wakazi wa Mikese.
Wengine ni Samuel Kogani (35), mkazi wa mkoni Dodoma; Onesmo Maroda (33), mkazi Mfuy Handeni mkoani Tanga na Hawa Said (34), mkazi wa Mkambarani.
Kamanda huyo alisema kuwa chazo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na kwamba Hiace ilikuwa ikitaka kulipita gari lingine na kukutana na Scania uso kwa uso.
Katika ajali ya tatu, mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Pastory Elia (37), mkazi wa Mkundi aligongwa na gari lisilojulikana katika eneo la Mkundi na kufariki papo hapo.
Ajali hizo ni mfululizo wa ajali zilizotokea mkoani humo mwishoni mwa mwezi uliopita na kusababisha vifo na majeruhi.
Katika siku za hivi karibuni mkoa wa Morogoro umekumbwa na ajali nyingi mbaya za barabarani ambazo zimesababisha vifo vingi.
Machi 21, mwaka huu wasanii 13 wa kundi la muziki la Five Star’s Modern Taarab walifariki dunia na wengine saba kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Mbeya kuelekea Dar es Salaam kuacha njia na kulivaa lori lililokuwa limesimama na kupinduka ndani Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Kesho yake, yaani Machi 22, mwaka huu ajali nyingine iliua watu watatu na kujeruhi wengine saba katika eneo la Ng'apa barabara kuu ya Morogoro-Iringa.
Ajali hiyo ilihusisha basi la kampuni ya Upendo.
Machi 24, 2011, watu 27 walijeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Osaka kuligonga lori la mizigo na kupinduka katika eneo la Maseyu barabara ya Dar es Salaam-Morogoro.
Katika mfululizo huo wa ajali, Machi 26 ajali mbili tofauti mkoani Pwani ziliua watu 17, huku liacha majeruhi wengi hoi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment