ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 7, 2011

Airtel wapeleka huduma kwa ‘Babu’ wa Loliondo

KAMPUNI ya simu za mkononi ya Airtel imezindua huduma ya mawasiliano katika eneo la 
Samunge na maeneo jirani, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha. 

Hatua ya kuwezesha mawasiliano katika maeneo hayo imetajwa na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Sam Elangalloor kuwa kumegharimu dola za Marekani 150,000 sawa na takribani Sh milioni 225.
 

“Uwekezaji huu utawezesha kuleta mawasiliano thabiti kwa watu wa vijiji vya Samunge, Mgongo, Mageri, Yasimdito na Digodigo,” ilisema sehemu ya taarifa ya kampuni hiyo kwa vyombo vya habari. 

Akitoa maoni yake juu ya uzinduzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Airtel, Elangalloor alisema kampuni imejizatiti vilivyo katika kutoa huduma bora na nafuu kwa watu wa Samunge. 

Alisema huduma hiyo itaambatana na uwepo wa mtandao madhubuti pamoja na huduma nyingine ambazo zimekuwa zikipatikana na kufurahiwa na wateja wengine wa Airtel nchini. 

“Uwepo wetu Samunge na maeneo mengine ya jirani, kwa hakika kutaleta chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wakazi na wageni wa maeneo haya,” alisema na kuongeza: “Kuwaunganisha watu wa Loliondo wakati huu ambapo mahitaji ya mawasiliano ni makubwa, kunadhihirisha dhamira yetu ya kuwa mbele zaidi kwa kila tunalofanya”. 

Eneo la Samunge limeonesha kuwepo ongezeko kubwa la wageni wanaotembelea, kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, wengi wao wakiwa wanakwenda kupata tiba maarufu ya kikombe cha Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania 
(KKKT), Ambilikile Mwasapila. 

Inakadiriwa ya kwamba idadi ya wageni wanaoingia na kutoka kwa siku inafikia takribani watu 25,000, huku eneo hilo likiwa linakabiliwa na uhaba mkubwa wa mawasiliano ya simu za mkononi. 

Kuanzishwa kwa huduma ya Airtel, kutawawezesha watu kupiga na kupokea simu, kutuma ujumbe mfupi, kutumia intaneti na kutuma na kupokea fedha kupitia Airtel Money. 

Taarifa hiyo ya Airtel ilimkariri Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isidore Shirima akielezea kufurahishwa na juhudi hizo za kupeleka mawasiliano katika maeneo husika. 

Shirima alisema: “Sisi, kama serikali, tumefarijika sana kuona juhudi hizi za uongozi na wafanyakazi wa Airtel katika kuhakikisha wanafikisha huduma ya mawasiliano ya simu za 
mkononi kwa wana jumuiya ya Samunge na maeneo jirani. 

Kuwepo kwa mtandao wa Airtel hapa siyo tu ya kwamba utaleta manufaa ya kiuchumi, bali pia kutachochea maendeleo ya huduma za kijamii kwa wageni na wenyeji”.


CHANZO:HABARI LEO

No comments: