Advertisements

Friday, April 29, 2011

Anayeua wanawake Dar es Salaam ashitukiwa

WAKATI hofu ya matukio ya kuuawa kwa wanawake jijini Dar es Salaam ikitanda, jeshi la polisi limepokea taarifa kuhusiana na mtu anayedaiwa kuhusika na matukio hayo yanayofanyika katika nyumba za kulala wageni. 

Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova. 

Kamanda Kova alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa polisi imepata taarifa kuhusiana na mwanaume mweupe anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 30, anayependelea kuvaa suruali aina ya Jeans, fulana nyeupe, raba na kofia kwamba ndiye mhusika wa matukio hayo ya mauaji. 


“Inasemekana mtu huyu anapendelea kufuata wanawake weupe na hasa walioolewa na kisha huwapeleka katika nyumba tofauti za kulala hapa jijini na akishamaliza nia yake, huwaua,” alisema. 

Kwa mujibu wa Kamanda Kova, matukio hayo ya mauaji yametokea katika maeneo ya Tandika, Mtoni kwa Aziz Ally, Buguruni kwa Mnyamani na Keko Machungwa. 

Wanawake wameuawa baada ya kufanyiwa mchezo mchafu wa kuingiliwa kinyume cha maumbile na kisha kunyongwa mpaka kufa. 

Kutokana na matukio hayo, Kamanda Kova ametoa onyo kwa wanawake kutokubali kuingia katika mahusiano ya kimapenzi na wanaume wasiowafahamu. 

Kamanda Kova amewakumbusha pia wahudumu wa mapokezi katika nyumba za kulala wageni kuhakikisha wanaandika majina na anuani kamili za mwanaume na mwanamke kabla ya kuingia katika chumba. 

Amesema, Polisi kwa kushirikiana na jamii imeanza msako mkali kuwasaka watuhumiwa wote wanaojihusisha na matukio hayo na kuomba mtu yoyote mweye taarifa za watuhumiwa hao kutoa taarifa katika vituo vya polisi vilivyopo karibu au kutuma ujumbe mfupi katika namba 0783034224. 

Hivi karibuni yaliripotiwa matukio ya mauaji ya wanawake watatu katika nyumba tatu tofauti za kulala wageni katika Manispaa ya Kinondoni na Temeke. 

Polisi ilibaini kuwa wanawake hao wote waliouawa, walikuwa wamekwenda katika maeneo hayo kwa ajili ya kustarehe na wenza wao.


CHANZO:HABARI LEO

No comments: