ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 12, 2011

Baraza lapitisha bajeti bila madiwani wa Chadema Arusha

Baraza la Madiwani Jiji la Arusha limepitisha bajeti ya zaidi ya Sh. bilioni 48.1 kwa mwaka huu wa fedha wa 2011/ 2012,  licha  ya madiwani 11  wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) kususia kikao hicho kilichofanyika jana kwa kutoka ukumbini.
Baraza hilo likiwa na wajumbe  16 kutoka vyama vya CCM na TLP, lililazimika kuendelea na kikao  na kupitisha bajeti hiyo, huku  baadhi ya  wajumbe wa baraza hilo kutoka vyama hivyo viwili wakishutumu hatua ya  madiwani wa  Chadema kususia kikao hicho.

Awali, baada ya wajumbe wote kuingia katika ukumbi, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha,  Estomiah Chang’a, alitoa taarifa ya idadi  ya madiwani  waliokuwa ukumbini wakiwemo wa Chadema, CCM na  TLP kuwa ni 25.
Alisema idadi hiyo ni zaidi ya akidi ya theluthi mbili ya  wajumbe wote 32 wanaotakiwa kuhudhuria kikao hicho.
Lakini wakati Meya wa Jiji la Arusha, Mstahiki Gaudence Lyimo,  aliposimama kwa ajili ya kufungua kikao hicho, madiwani wa Chadema wakiongozwa na John Bayo wa kata ya Elerai walinyanyuka vitini na kutoka nje ya ukumbi.
Hata hivyo, Chang’a, alisema kanuni  na taratibu zinaelekeza kwamba iwapo mjumbe    yeyote  wa kuchaguliwa atapata  wito na akaitikia na kufika ukumbini  ni dhahiri mjumbe huyo atakuwa amehudhuria kikao hicho na hivyo kuchangia kufikia  idadi ya wajumbe wanaotakiwa kufikisha  akidi ya kikao ya theluthi mbili  hata kama atakuwa ameondoka ukumbini.
Mbali na wadiwani wa  Chadema kuingia ukumbini na kujiorodhesha katika kitabu cha mahudhurio, Bayo, aliamua kuchukuwa rejesta ya majina na kukatakata majina yao.
Akizungumza mara baada ya kupitishwa kwa bajeti hiyo, Diwani wa TLP kutoka kata ya  Sokoni One, Maiko Kivuyo, alisema wamepitisha bajeti  ya jiji kwa manufaa ya wananchi wa Arusha.
CHANZO: NIPASHE

No comments: