ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 6, 2011

Bilioni 1.1/- kutumika kuangamiza kunguru

KERO na hasara zinazosababishwa na kunguru waharibifu nchini huenda zikakoma ifikapo mwaka 2013 kutokana na kuanzishwa kwa mbinu mpya za maangamizi zitakazoendeleza juhudi za miradi ya awali iliyoshindwa kumaliza tatizo hilo. 

Kwa kipindi kirefu sasa, Jiji la Dar es Salaam na maeneo ya pwani ya nchi yamekuwa yakisumbuliwa na kunguru weusi zaidi ya milioni 1.2 waliochangia kwa kiasi kikubwa kupotea kwa jamii nyingi za ndege na viumbe wengine wadogo.
 

Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Uhifadhi wa Maliasili na Mazingira Tanzania (WCST), Anne Lema aliyesoma hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa utambulisho wa mradi wa maangamizi ya kunguru kwa viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na manispaa zake, kwa niaba ya Mwenyekiti Philemon Luhanjo, mbinu hizo zitafanikiwa endapo wananchi watashiriki kikamilifu katika mradi huo. 

Lema alisema, Serikali kwa usaidizi wa balozi za Dernmark, Finland na Shirila la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID) ambao kwa pamoja wamechangia Dola za Marekani 748,200 (Sh bilioni 1.12) kufanikisha mradi huo kwa miaka miwili, watatumia sumu, risasi na mitego kuwaangamiza kunguru hao. 

“WCST na wadau wengine tulianza kutekeleza mradi huu Oktoba mwaka jana na bado tunahitaji wafadhili wengine kwa ajili ya kufadhili mwaka uliobaki kwa kuwa hawa wasasa wametufadhili kwa miaka miwili pekee,” alisema Lema katika mkutano huo uliofanyika Dar es Salaam jana. 

Alisema, Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Wanyamapori imetoa Sh milioni 150 zilizotumika kuendesha shughuli za awali za mradi kama kununua kilo 20 za sumu maalumu na kutengeneza baadhi ya mitego. Hadi sasa zimepokelewa Sh milioni 540 kutoka kwa wafadhili na kiasi kilichobaki kikitegemewa kupokelewa Juni mwaka huu. 

Kwa maelezo yake, mradi huo ulianzishwa kufuatia maagizo ya Rais Jakaya Kikwete utazinduliwa baadaye ili kuwezesha shughuli hizo kusogezwa katika maeneo mengine nje ya Dar es Salaam. 

Mtaalamu wa mradi huo kutoka WCST, Lota Melamari alisema, wamelenga kuangamiza kunguru 600,000 kwa mwaka wa kwanza, 400,000 kwa mwaka wa pili na 200,000 kwa mwaka wa tatu katika maeneo ya mijini na vijijiji ambayo wamebaini uwepo wao. 

“Hadi sasa tumeangamiza kunguru wengi na katika eneo la Ikulu ya Dar es Salaam kulipotegwa mitego 10, kunguru 3000 walinaswa na kufa. Kwa kipindi cha miaka miwili tunatakiwa kutengeneza mitego 600 na hadi sasa mitego 150 iko tayari na 50 imekwisha sambazwa,” alisema. 

Alisema, risazi zisizo na madhara kwa mazingira ndizo zitakazotumika zaidi katika maeneo ya vijijini na kwa kipindi hicho, wataagiza zisizopungua 50,00 kutoka New Zealand. 

“Hizi ni ghali kuliko zile za kawaida za moto na hata sumu tunayotumia nayo ni ghali kutokana na bei yake ya Sh 25,000 kwa kilo moja…lakini inasaidia kwa sababu kwa Oktoba 2010 tu, iliua kunguru 113,345 kwa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani,” alifafanua.


CHANZO:HABARI LEO

No comments: