MWENYEKITI Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi, amesema malumbano yanayoendelea nchini ya nani Rais ajaye yanapoteza muda; badala yake amewataka wananchi washirikiane na Serikali iliyopo kujiletea maendeleo.
Ameshauri wananchi na vyombo vya habari, kuacha kushabikia mjadala huo wa nani rais ajaye, kwani serikali iliyopo imechaguliwa hivi karibuni na inahitaji ushirikiano wa karibu.
Mengi ameyasema hayo Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya kisiasa inavyoendelea nchini hivi sasa.
Amesema, Watanzania wana matatizo mengi ya umasikini na wanahitaji kuona serikali ambayo imechaguliwa hivi karibuni ikiwatumikia katika kutekeleza ilani yake ya uchaguzi na si kuchanganywa na mambo ya nani rais ajaye.
Licha ya kuwa Mengi hakutaja chama au mtu katika mazungumzo yake, lakini hivi karibuni ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na baadhi ya viongozi wastaafu waliingia kwwenye malumbano juu ya suala la nani rais ajaye.
“Kitu kinachonipa shida sasa hivi, ni nguvu za Watanzania na vyombo vya habari kuelekezwa kuzungumzia rais wa 2015 badala ya kutafakari tufanye nini juu ya maendeleo ya nchi yetu,” amesema Mengi Jumatano.
Amesema, anashangazwa kuona wazee na vijana wanaingia kwenye malumbano hayo ambayo hayana tija sasa; kwani urais ni wito na Watanzania ndio wanatakiwa kubaini sifa na anayeutaka ajipime kutokana na sifa hizo.
Mwenyekiti huyo wa IPP alisema Watanzania hawafaidiki na malumbano ya nani ni rais ajaye, ila wanachohitaji ni njia zipi zitumike kuwapunguzia umasikini na wawe na uhakika wa chakula cha kila siku.
“Kuliibua suala hili katika muda huu na kushabikiwa na vyombo vya habari, ni dharau kubwa kwa Watanzania, kwani tunadhani kuwa wako pale kwa ajili ya kuchagua marais tu,” alisema.
Aliongeza kuwa ni heri Watanzania wapewe fursa ya kutekeleza majukumu yao na kufikiri ni sifa zipi awe nazo kiongozi ajaye awe diwani, mbunge au rais na si nani atakuwa rais “tujirudi, kwani haya tunayofanya sasa tunalifanya Taifa letu likose mwelekeo.”
Katika mkutano huo pia Mengi alizungumzia suala la kuongezeka kwa rushwa nchini ambalo alisema bado nchi haijaelekeza nguvu vya kutosha katika kukabiliana na wala rushwa wakubwa.
Mengi alisema upo umuhimu wa kushughulika na watoa rushwa wakubwa, kwani kama wataendelea kuwapo, kazi inayofanywa na Serikali ya kupambana na rushwa itakuwa kazi bure.
“Tufike mahali tuseme imetosha na tumechoka na ufisadi,” alisema Mengi na kuwatuhumu Watanzania wanaokubali kuhongwa kuwa nao ni chanzo cha ufisadi kuongezeka.
Mengi pia katika mazungumzo yake, alizungumzia kesi inayomkabili dhidi ya mfanyabiashara maarufu Yussuf Manji na juu ya uamuzi uliotolewa hivi karibuni na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Katika suala hilo, alisema malalamiko yake aliyowasilisha Mahakama Kuu hayakuwa ya kumkataa hakimu, lakini pia akadai kwamba Jaji huyo hakujibu malalamiko yake kisheria.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment