ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 5, 2011

CCM Mbarali kumnyang`anya kadi ya uanachama Mbunge?

Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya kimekumbwa na jinamizi la mpasuko kufuatia baadhi ya viongozi wilaya kwa kushirikiana na mkoa kutaka kumnyang’anya kadi ya uanachama Mbunge wa Mbarali, Dickison Kilufi.
Mbunge huyo anafanyiwa njama hizo kutokana na kuwa na msimamo tofauti na viongozi wa chama na serikali ya wilaya na mkoa kuhusu mgogoro kati ya wananchi wa Mbarali wanaomlalamikia mwekezaji wa shamba la mpunga la Mbarali Estate kuwanyanyasa.

Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Mbarali uliofanyika juzi ambao ulifuatia wa Kamati ya Siasa ya Wilaya iliyomhoji mbunge huyo kwa kumuuliza maswali 14 na baadhi ya wajumbe walipendekeza mbunge huyo anyang’anywe kadi.
Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wilaya ya Mbarali, Kassimu Kondo, aliliambia NIPASHE kuwa wakati wa mkutano wa Halmashauri ya wilaya kulitokea mvutano ambapo baadhi ya wajumbe walitoa pendekezo la kutaka Mbunge huyo anyang’anywe huku wengine wakipinga.
Kondo alisema kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, mbunge huyo aliitwa kwenye kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya chini ya uenyekiti wa Katibu wa CCM Wilaya, Mkanyege Kashiririka, ambapo alihojiwa maswali 14 ambayo kutokana na majibu aliyoyatoa yamepelekwa ngazi ya mkoa.
Mikutano hiyo miwili ya kumjadili Kilufi ilifanyika baada ya wilaya kuagizwa na viongozi wa chama mkoa kupitia kwa Katibu wa CCM Mkoa, Verena Shumbusho, ambapo mapendekezo yamepelekwa ngazi ya mkoa ambao watajua hatua za kuchukua zaidi.
Akizungumza na NIPASHE akiwa Dar es Salaam, Kilufi alipoulizwa kama ana taarifa kwamba upo mpango wa kumnyang’anya kadi alithibitisha kupata taarifa hizo kutoka katika kikao Kamati ya Siasa ya Wilaya na Halmashauri Kuu ya wilaya ambapo baadhi ya viongozi walimpa taarifa hizo.
“Tatizo kubwa ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ambaye ni mwajiriwa katikia shamba la Mbarali Estate kuwa na chuki binafsi juu yangu, ni mgogoro wa muda mrefu kwani hata kwenye kampeni zangu hakuwahi kushiriki, mimi nilidhani baada ya kumalizika uchaguzi na tofauti hizo zitaisha ili tushirikiane kuleta maendeleo kwa wananchi, lakini hali hiyo imekuwa tofauti na sasa anashinikiza niondolewe madarakani,” alisema Kilufi.
Alisema hata aliposhinda katika kura za maoni mwenyekiti aliitisha kikao cha kupinga matokeo hayo na kupeleka mkoani na hata taifa, lakini azima yake haikufanikiwa, na kuuomba uongozi wa chama Taifa kuliangalia kwa makini tatizo hilo.
Mgao alipotakiwa na NIPASHE kutoa maelezo kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwake na Kilufi, alisema msemaji wa chama ni Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi hivyo kumtaka mwandishi awasiliane na katibu huyo.
Hata hivyo mgogoro huo umekuwa hauishi kwa sababu baadhi ya viongozi wa chama na serikali wanadaiwa kupewa maeneo ya kulima katika shamba hilo lenye mgogoro madai ambayo pia yalishawahi kuthibitishwa na Kilufi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: