ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 5, 2011

Rais Kikwete ampa Dk Magufuli agizo jipya

Rais Jakaya Kikwete
Patricia Kimelemeta
RAIS Jakaya Kikwete amemwagiza Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kulishughulikia mara moja “genge la watu waliojipanga kuidhulumu Serikali na wananchi,” kwa kulipwa mabilioni ya fedha huku wakijenga barabara za viwango hafifu.Rais Kikwete alitoa agizo hilo jana wakati wa hafla fupi ya kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa Barabara ya New Bagamoyo, iendayo Mwenge-Tegeta, Dar es Salaam. 

“Tunawalipa kwa nini? Nimelisemea hili na sitaki kulisemea tena. Lipo genge la watu waliojipanga kudhulumu. Waziri hili lazima liishe. Sitaki kulisemea tena,” Rais alimwambia Dk Magufuli na kuongeza:
“Barabara zina gharama kubwa sana na nyingine zinajengwa kwa kiwango hafifu kwa sababu mbili: “Moja ni kwamba mhandisi mshauri wetu ni mzembe au Wizara na Wakala wa Barabara (Tanroads) nao wanazembea na kuwalipa wakandarasi ambao barabara zao ni za kiwango duni.”

Agizo hilo limekuja wiki mbili baada ya Rais Kikwete kumtaka Magufuli kukaza uzi katika kutekeleza sheria katika utendaji wa kazi lakini akimkumbusha kuzingatia ubinadamu katika utekelezaji wake: ''Hili naliongea kwa umakini kwani nataka nieleweke vizuri. Bomoabomoa ipo.
Usilegee katika kutekeleza sheria, lakini uangalie ubinadamu katika bomoabomoa hiyo pamoja na historia ya eneo husika. Pia muwalipe wote wanaostahiki kulipwa fidia na msiwalipe wale wasiostahiki na msiangalie unafuu wa Serikali pekee.''

Jana, Rais Kikwete alionya kuwa mara nyingi barabara hizo zimekuwa zikikabidhiwa wakati hazijamalizika na nyingine zimebomoka kutokana na wahandisi washauri kushindwa kufanya kazi yao vizuri na kuishia kuishinikiza Serikali kulipa wakati barabara ni mbovu.

“Nawashangaa sana wahandisi washauri, wao ndiyo wenye jukumu la kuhakikisha barabara zinajengwa kwa kiwango kinachokubalika, lakini wamekuwa mstari wa mbele kuidhinisha malipo wakati barabara ni mbovu.”
“Hata ujenzi wa Barabara hii ya Mwenge –Tegeta, hapa kuna watu watafaidika na mradi huu. Wametoa macho kwa ajili ya kusubiri kula, naomba Magufuli washughulikie. Hawa wanaisababishia Serikali hasara na lawama isiyokuwa yao,” alisema Rais Kikwete.

Alisema wahandisi hao wamesomeshwa nje ya nchi na fedha za walipakodi, na kwamba ni watalaamu wazuri kwa mambo ya barabara lakini wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa sababu ya tamaa.

“Mimi huwa nawashangaa sana hawa watu na sijui wana maana gani, kwa sababu wanajua sheria na taratibu za kazi zao, lakini wanafanya makusudi kwa ajili ya maslahi binafsi, wako tayari kuandaa 'certificate' (hati) ya malipo haraka ili na wao wapate mgawo, Magufuli hakikisha unawashughulikia ipasavyo,” aliongeza.

Alitaka yasifanyike malipo yoyote kwa makandarasi mpaka ujenzi wa barabara  hiyo na nyingine utakapohakikiwa. Amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuangalia kiwango cha ubora kwenye vitabu na miradi.

“Nimemwambia CAG, asiishie kwenye vitabu peke yake, bali afike hadi kwenye miradi kama hii ili kuangalia kuwa fedha iliyoandikwa na iliyotolewa ndiyo iliyotumika kwenye miradi? Ikiwa watajiridhisha watatoa ripoti ambayo itasaidia kuidhinishwa kwa malipo,” alisema.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete alisema baada ya Serikali kuendesha kwa mafanikio Mfuko wa Barabara (Road Fund) sasa inaanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Barabara (RDF). Alisema kazi ya Road Fund ni kufanya matengenezo ya barabara na mfuko huo mpya utakuwa na jukumu la kujenga barabara.

Rais Kikwete aliusifia Mfuko wa Barabara akisema umefanya kazi kubwa na kuwajia wale wanaodai kuwa maendeleo ya Taifa yanakwenda kwa kasi ndogo kulinganisha na baadhi ya nchi nyingine za Afrika zikiwamo jirani.

“Tanzania ni nchi kubwa. Ukubwa una uzuri wake na una gharama zake. Umeme uliovutwa kutoka Kidatu hadi Tarime, kwa mfano, kama ungewekwa katika baadhi ya nchi nyingine, ungefungwa hata kwenye matendegu ya vitanda.”

“Hata ujenzi wa barabara za lami tunazozijenga katika miradi yetu 105, katika nchi nyingine zingeingia hata majumbani mwa watu. Jamani! Tanzania ni nchi kubwa na maendeleo yetu ni makubwa, tuache kuilinganisha na nchi nyingine hizi ndogo ndogo.”

Barabara hiyo inajengwa kwa ushirikiano na Serikali ya Japan chini ya Shirika lake la Misaada (Jica). Rais Kikwete aliishukuru Japan kwa kuendelea kutoa misaada hiyo muhimu katika maendeleo ya Tanzania.
Wakati akihutubia, Rais Kikwete aliwaomba waliohudhuria kusimama kwa dakika moja kuwakumbuka wananchi wa Japan waliopoteza maisha katika tsumani.

Awali, Dk Magufuli alisema barabara 63 kati ya 105, zimekamilika kwa gharama ya Sh3.7 trilioni.
Aliahidi kusimamia na kuhakikisha zinajengwa kwa kiwango kinachokubalika, ili kuepusha hasara kwa Serikali.
“Kuna miradi ya barabara nchi nzima. Mwananchi anaweza kutembelea Bajaji kutoka Daraja la Mkapa hadi Bukoba. Hii inatokana na kiwango cha lami cha barabara.”

Akizungumzia ujenzi wa barabara hiyo mpya yenye urefu wa kilometa 12.9, Dk Magufuli aliwataka wafanyabishara wa maeneo ya Tegeta kuondoka mapema iwezekanavyo kabla ya kuondolewa kwa vibanda vyao na Serikali ili kupisha ujenzi huo.

CHANZO:MWANANCHI

No comments: