ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 11, 2011

Chadema watamba kuivua gamba CCM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetamba kuwa, kujiuzulu kwa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Sekretarieti ya chama hicho ni mafanikio makubwa sana kwao na wanastahili pongezi. 

Chama hicho kimesema, nguvu yake ndiyo iliyokilazimisha Chama Cha Mapinduzi kikubali mabadiliko na kuanza kujivua gamba, na kwamba, Chadema wataongeza shinikizo la kutaka mabadiliko.
 

Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, amesema, kujiuzulu kwa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya CCM ni ishara kuwa, chama hicho kimeanza kukiri udhaifu na kukubali kubadilika. 

“Kwa hiyo yaani mtupongeze aisee” amesema Mbowe wakati anazungumza na Waandishi wa Habari mjini Dodoma na akaongeza kuwa, CCM bado haijaondoa tatizo la msingi ndani ya chama hicho. 

Amesema, CCM wameanza kusoma alama za nyakati, na kwamba, sasa utayari wa kujiuzulu upalekwe serikalini. 

Mbowe amesema, mabadiliko ya uongozi katika CCM ni kujitia moyo kwa madai kuwa, hata ukijivua gamba, saratani itabaki mwilini. 

Amesema, mpasuko CCM upo siku nyingi na haukuanzia katika Sekretarieti Makao Makuu ya chama hicho hivyo Watanzania hawatadanganywa na mabadiliko ya uongozi ndani ya chama hicho. 

Kwa mujibu wa Mbowe, tatizo la msingi CCM si Makamba, Kamati Kuu au Sekretarieti ya Kamati Kuu ya chama hicho, ila ni fikra za wanaokiongoza chama hicho. 

Mwanasiasa huyo amedai kuwa, kuna saratani inayokitafuna chama hicho katika ngazi zote za uongozi na sasa CCm wameonesha kuwa, nguvu za nje ya chama hicho zimewalazimisha wakubali mabadiliko. 

“Kukiri kujivua gamba ni kukiri udhaifu… bado mkuu wao ni yule yule” amesema Mbowe na kudai kuwa, kujiuzulu kwa Sekretarieti ya CCM ni jambo la kihistoria kwa kuwa haijawahi kutokea tangu tupate uhuru 

“Ni ishara ya kuweweseka, huku ni kuweweseka” amesema Mbowe mjini Dodoma muda mfupi baada ya kufungua kongamano la wanafunzi wa vyuo vikuu vilivyopo mkoani humo. 

Amesema, kujiuzulu kwa Kamati Kuu na Sekretarieti ya Kamati Kuu ya CCM kumewapa Chadema nguvu zaidi, ari zaidi na moyo zaidi kuongeza kasi ya katafuta mabadiliko yenye manufaa kwa Watanzania. 

Wakati huo huo Chadema kimesema, kitapinga kwa nguvu zote mpango wa Serikali wa kuharakisha kuwasilisha bungeni muswada wa sheria itakayosimamia mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Tanzania. 

Mbowe amedai kuwa, haraka ya Serikali inawanyima Watanzania fursa ya kutoa maoni kuhusu Katiba yao, na inajenga mazingira yatakayosababisha vurugu. 

“Tunaishauri Serikali iuondoe muswada huu” amesema Mbowe wakati anazungumza na Waandishi wa Habari muda mfupi baada ya kufungua kongamano lililoandaliwa na chama hicho lililowashirikisha wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma. 

Kwa mujibu wa Mbowe, Chadema wataupinga muswada huo ndani na nje ya Bunge, na akabainisha kuwa, tarehe ambayo Serikali imepanga kuuwasilisha muswada huo, wabunge wa chama hicho watakuwa na maoni ya Watanzania kuhusu muswada huo. 

“Unapokuwa na wrong road map, inakupeleka kwenye wrong destination” amesema Mbowe na kuongeza kuwa, Serikali ilipaswa kuitumia fursa hii ya kukusanya maoni ya wananchi kujenga mshikamano wa kitaifa, uzalendo na kutibu majeraha ya uchaguzi mkuu. 

Amesema, haraka ya Serikali haina maana na haitakuwa na manufaa kwa taifa, na akadai kuwa, yalitokea Zanzibar yanaonesha namna serikali isivyo makini na ni aibu. 

Mbowe amesema, Bunge linapaswa kuitumia fursa hii ya mabadiliko ya Katiba kuleta mshikamano wa kitaifa na si kuwagawa wananchi. 

Amesema, kama serikali haitabadili nia ya kuuwasilisha muswada huo bungeni, Aprili 16, wafuasi wa Chadema wataandamana nchi nzima kuupinga, na watafanya mikutano ya hadhara ili kutoa maoni yao. 

Awali aliwaeleza wanafunzi wa vyuo vikuu kuwa, wana wajibu wa kuwa wazalendo na kujiandaa kuwa viongozi wa baadaye wa taifa hili. 

Amesema, kongamano hilo linalenga kuwafundisha wanafunzi hao fikra mpya ili washiriki katika harakati za kutafuta mustakabali wa taifa hili sanjari na kujifunza wajibu wao katika mchakato unaoendelea wa mabadiliko ya Katiba ya nchi. 

Amesema, chadema pia inaanzisha matawi ya wanafunzi wanawake katika vyuo vikuu vyote Tanzania kwa kuanzia na vya Dodoma ili kuwahamasisha washiriki katika shughuli za siasa tangu wakiwa wanafunzi badala ya kusubiri Viti Maalum wakiwa wazee.


CHANZO:HABARI LEO

No comments: