WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali, imesema zaidi ya wanafunzi 30,000 Visiwani Zanzibar wanakaa chini darasani kutokana na ukosefu wa madawati.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi madawati 100 yaliyotolewa na Kampuni ya Vodacom kwa Shule ya Msingi Darajani Mjini Unguja, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mwanaidi Saleh alisema idadi hiyo ni kubwa na juhudi zinachukuliwa kuondokana na tatizo hilo.
“Vijana wetu wengi bado wanakaa chini madarasani, hivi sasa kwa Zanzibar nzima tunahitaji
madawati yasiyopungua 30,000,” alisema Katibu Mkuu huyo na kuziomba Taasisi mbalimbali kusaidia.
Alisema msaada huo wa madawati kutoka Vodacom wenye thamani ya Sh milioni 10 umetolewa wakati mwafaka.
Katibu Mkuu huyo alisema kwamba madawati yaliyotolewa yatatosheleza mahitaji ya shule hiyo yenye wanafunzi wasiopungua 2,100, ambapo wanafunzi 300 watafaidika na madawati hayo.
Aidha aliwataka wanafunzi kuhakikisha wanayatunza madawati hayo ili wadhamini hao na wengine wawe na moyo wa kusaidia zaidi.
Mkurugenzi wa huduma za jamii kutoka Vodacom, Mwamvita Makamba alisema kampuni yake inajali maendeleo ya jamii katika kila sekta na ndiyo maana imekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii kwa faida itokanayo na Kampuni hiyo ikiwa ni marejesho kwa wananchi.
Katika risala ya walimu wa Shule hiyo iliyosomwa na Mwalimu Asha Abdallah alisema Shule ya Darajani inahitaji pia misaada ya vitabu na vifaa vya maabara.
Mwalimu Asha alisema kwa kuwa Shule ya Darajani ni ya Msingi na Sekondari, inakabiliwa
na changamoto kadhaa ikiwemo wanafunzi kusoma katika mazingira magumu hususan
somo la sayansi linalohitaji vifaa vya kujifunzia kwa vitendo.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment