.jpg)
Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu, amesema gharama za usafiri wa ndege bado ziko juu ikilinganishwa na vipato vya Watanzania.
Akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini, (TCAA), Nundu alisema usafiri huo bado ni tatizo kwa Watanzania walio wengi kwa sababu hawawezi kumudu gharama zake kutokana na vipato vyao kuwa vidogo.
Kwa upande mwingine, Nundu, alisema huduma zitolewazo kwa abiria pia zina mapungufu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kuruka ndege katika muda uliopangwa.
Aliitaka mamlaka hiyo kuangalia sheria inayounda mamlaka hiyo ili kuhakikisha inaendeleza usafiri wa anga bila kudhoofisha usalama wake.
" Mnatakiwa msimamie mwenendo mzima wa watoa huduma bila kuathiri shughuli zao ili huduma zao ziwe bora na za kutumainika kwa gharama nafuu ili wananchi wengi waitumie njia hii ya uchukuzi, " alisema.
Alisema Serikali inaendelea kuhakikisha uwekezaji kwenye sekta hiyo ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu katika viwanja vingi unapewa kipaumbele.
Waziri huyo, alisema lengo ni kueneza huduma ya usafiri wa anga kwa Watanzania walio wengi.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment