Sasa msongamano watishia usalama
Waomba ruhusa kuongeza wanaopita
DC Ngorongoro aweka ngumu.jpg)
Wagonjwa wanaokwenda kwa Babu katika kijiji cha Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro kupitia kituo cha Bunda, wameiomba serikali kuongeza idadi ya watu wanaotakiwa kwenda kwa siku kutoka 200 wa sasa hadi ifikie watu 1,000 kwa siku.
Katika kituo hicho kumekuwa na misururu mirefu ya magari yanayokadiriwa kufikia 500 yanayosubiri kwenda kwa Babu mengine yakiwa yamebeba wagonjwa mahututi.
Wagonjwa hao walitoa kilio chao hicho juzi mjini Bunda ambapo walisema hivi sasa ni watu 200 tu wanaruhusiwa kutoka kituoni jambo ambalo limekuwa likiwaongozea gharama baada ya kujiandikisha na hivyo kusababisha mrundikano mkubwa katika kituo hicho.
Walisema idadi ya wagonjwa 200 iliyoruhusiwa kwa siku na serikali mbali na kuwazidishia gharama za maisha wasafiri hao, pia haikidhi haja kutokana na ukweli kuwa Bunda ni moja ya vituo vikuu vya wasafiri hao kwani hukusanya kanda nzima ya Ziwa Victoria kwa kuhusisha mikoa ya Mara, Mwanza, Shinyanga na Kagera pamoja na Kigoma kanda ya Magharibi.
Mmoja wa wasafirishaji katika kituo hicho kutokea mkoa wa Kagera, Haji Mnyonge, alisema kwa ujumla serikali inapaswa kuangalia upya maazimio yake ya kupitisha watu 200 pekee idadi aliyosema ni sawa na magari 16 kuondoka kituoni hapo kwa siku ili kuwapunguzia gharama za maisha waendaji, lakini pia kupunguza msongamano eneo hilo.
“Kwa hili naishauri serikali iwahurumie watu wake hasa wa kanda ya Ziwa kwani watu 200 ni wachache sana, Bunda inategemewa na kanda nzima ya Ziwa iliyo na watu wengi hivyo ni vyema serikali ikatuongezea hata tukafika watu 1,000 kwa siku,” alisema Haji.
Kwa upande wake, Sokoro Marwa alizielezea gharama za maisha kwa mji wa Bunda kuwa ziko juu kulinganisha na maeneo mengine huku huduma muhimu kama maji,vyoo na malazi zakosekana.
Aidha, wagonjwa na wasafirishaji hao walisikitishwa na kupandishwa bei kiholela kwa vyakula kwenye migahawa pamoja na huduma nyingine muhimu kwa binadamu, hivyo viongozi wa wilaya hiyo kulikemea jambo hilo pamoja na kuboresha mazingira kwa kujenga choo mahali kilipo kituo hicho.
Hata hivyo, Mkuu wa wilaya ya Bunda Francis Isaac, alipoulizwa na NIPASHE alisema serikali ngazi ya wilaya hiyo imeshaona mrundikano kituoni hapo unaosababishwa na kuruhusiwa kwa watu wachache kwenda kwa Babu hivyo imeamua kusitisha zoezi la kutoa vibali kwa siku moja ikisubiri uamuzi wa kutoka ngazi za juu ambako wamepeleka suala hilo.
Kuhusu kupanda kwa gharama za maisha zinazoelezwa na wasafirishaji hao, Isaac alisema zina unafuu zaidi kulinganisha na zilizokuwa zikitolewa katika kijiji cha Samunge inapotolewa tiba.
Huko mkoani Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali amesema mkusanyiko wa watu waliokuwa wakienda kwa Babu unazidi kupungua na watu wanakwenda bila usumbufu.
“Sasa foleni inatembea na mkusanyiko wa watu umepungua, hadi kufikia jana watu walikuwa wanaenda wanapata dawa na kuondoka tunashukuru tumeweza kuthibiti hali,” alisema Wawa Lali.
Hata hivyo, alisema kutokana na mvua ambazo zinanyesha mara kwa mara kumekuwa kukitokea tatizo la magari kukwama na kuwasababisha wagonjwa kuchelewa kwenda kupata huduma.
“Magari mengi ambayo si madhubuti yamekuwa yakikwama sasa watu wanapeleka magari kama Corolla na huku kunamvua barabara mbovu unakuta mengi yamefia njiani kwa hiyo natoa wito kwa wananchi wanaokuja huku wasilete magari kama Corolla watateseka kwani barabara ni mbovu,”alisema Wawa Lali.
Alisema mbali na hilo amekuwa akisikitishwa na watu ambao wanatoka Kanda ya Ziwa kwani wamekuwa hawafuati sheria kwani licha ya kuambiwa wasipeleke magari ya kubebea mizigo kubebea abiria wamekiuka amri hiyo na kuyaleta.
“Sasa kitu ambacho tutakifanya ni kuyarudisha magari yote ambayo tumeyazuia yasiingie huku, wakifika hapa na watu wao tunawarudisha hawapati huduma sisi msimamo wetu watu wanaokuja na mafuso na Corolla hatutawaruhusu kwenda kwa Babu,” alisema.
Alitoa wito kwa uongozi wa njia ya Mwanza na vituo vilivyopo huko kutotoa vibali kwa watu ambao wanapeleka wagonjwa na magari hayo aliyoyataja na kusema kuwa iwapo atabanika mtu anapeleka wagonjwa na usafiri wa aina hiyo basi achukuliwe hatua za kisheria ili iwe fundisho.
Katika stendi ya magari yaendayo wilayani Ngorongoro katika kijiji cha Samunge kwa Babu kulionekana kutokuwa na watu wengi na makondakta wamekuwa wakilazimika kutafuta abiria tofauti na siku za nyuma ambapo watu walikuwa wakigombania usafiri.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment