WANAWAKE katika mikoa ya Kanda ya Kati wamebadilisha mtindo wa ukeketaji wa wanawake uliokuwa unafanyika hadharani, sasa wanafanya vitendo hivyo kwa watoto wa kike wachanga hasa wanapozaliwa ili kukwepa Sheria ya Makosa ya Kujamiiana na kuendeleza vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Women Wake Up (WOWAP), Fatma Toufiq alisema, ukeketaji wa watoto wachanga katika mikoa ya Dodoma na Singida unaendelezwa na wanawake wenyewe kwa njia ya mangariba wa kike na wakunga wa jadi ambao wanashirikiana na wazazi katika uendeshaji wa kazi hiyo ya kuwakeketa watoto wachanga.
Toufiq alisema tofauti na mikoa hiyo, kwa Mkoa wa Mara vitendo vya ukeketaji bado vinafanyika hadharani, ambapo mwaka jana zaidi ya wasichana 1,500 waliandaliwa kufanyiwa ukeketaji licha ya Serikali na wanaharakati kuendesha kampeni za kuondokana na mila hiyo iliyopitwa na wakati.
Alisema vijana wa kiume katika jamii ya Wakurya wilayani Tarime walionekana hadharani wakiwa wamebeba silaha za jadi na kutishia wanaharakati waliofika kwenye eneo hilo kujaribu kuzuia utekelezaji wa mila hiyo inayoungwa mkono na wazee wa jadi ambao wanahitaji kuelimishwa ili kuondokana na mila hiyo.
“Hili ni suala la utamaduni, japokuwa linakiuka haki za binadamu na kusababisha madhara makubwa ya kiafya, kisaikolojia na kiuchumi, kwa kweli halikubaliki,” alilalamika Toufiq.
Alipendekeza njia mbadala ya kuendesha mafunzo ya unyago kwa watoto wa kike bila kuhusisha vitendo vya ukeketaji na kutoa mfano halisi wa tukio la Kijiji cha Wilunze wilayani Bahi ambako WOWAP iliendesha mafunzo mbadala bila kuhusisha ukeketaji kwa wasichana sita na kushirikiana na makungwi wa jadi kutoa mafunzo hayo na kuendesha sherehe zao za kijadi.
Alisema Mfuko wa Jumuiya za Kiraia (FCS), umeanza kugharamia kampeni ya elimu ya sheria za adhabu ya makosa ya jinai baada ya kukamilisha utafiti wilayani Bahi, ambako ulitoa Sh milioni 105 kugharamia mradi huo katika eneo linalosadikiwa kuathiriwa na mila ya ukeketaji kwa watoto wachanga mkoani Dodoma.
Alisema kampeni ya kutokomeza mila ya ukeketaji wa wanawake inakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za ukosefu wa fedha, migongano ya kimaslahi kati ya maofisa watendaji, wanasheria na wanasiasa na rushwa bado inakwamisha utekelezaji wa kampeni ya kutokomeza mila potofu nchini.
CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment