ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 4, 2011

Kanisa lazuia waumini kwenda kwa Babu Loliondo

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Barnabas Mtokambali amewaonya waumini wa kanisa hilo nchini kote kutokwenda katika Kijiji cha Samunge wilayani Loliondo kwa Mchungaji mstaafu wa KKKT, Ambilikile Mwaisapile kwa ajili ya kupata dawa maarufu kama kikombe cha Babu. 

Aidha amesema baadhi ya Watanzania hawataki kufanya kazi, lakini wanataka kuwa na fedha za kunywa pombe saa zote, kuendesha magari na mambo mengi ya anasa, na wamezoea kupata pesa nyingi kwa kufanya ufisadi, na fedha zinapobanwa kidogo wanapiga makelele kwamba hali ya uchumi ni mbaya.
 

Askofu Mtokambali alisema hayo jana mjini Kigoma alipozungumza na mamia ya waumini wa kanisa hilo wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la upanuzi wa Kanisa Kuu la mjini Kigoma na Kituo cha Kanisa hilo, ambalo alisema kwenda Loliondo kwenye kikombe ni sawa na kwenda kinyume cha mafundisho ya Yesu. 

Alisema, katika mafundisho yake na hata wakati wake, Yesu hakuwahi kunywa majani na mizizi na kama jambo hilo halikuwahi kufanywa na kiongozi mkubwa wa kidini kama huyo, kwa nini wao wafanye hivi sasa. 

Aliwaambia waumini hao kuwa ni lazima wachungane kuhakikisha hakuna mmoja wao atakayeenda Loliondo na kama akigundulika, amekwenda huko itakuwa amekwenda kinyume cha Kanisa na litamtenga. 

Ili kuhakikisha maneno aliyosema yanawaingia vizuri waumini hao, Askofu huyo aliwaambia kila mmoja alipokaa apaze sauti na kusema ‘Nitakufa na Yesu, sitakwenda kwa Babu Loliondo kunywa kikombe cha majani na mizizi.’ 

Waumini wake walitii kwa kufanya hivyo. Sambamba na hilo, Askofu Mtokambali alisema anawashangaa Watanzania wanaopiga kelele kwamba kuna hali mbaya ya uchumi hivi sasa nchini na kwamba wanaosema hivyo wamezoea kula chipsi kuku bila jasho. 

Alisema uchumi hivi sasa uko katika hali nzuri, ingawa watu wanapaswa kufanya kazi ikiwemo kuzalisha chakula kwa wingi ili kukabiliana na hali hiyo. 

“Watu hawataki kufanya kazi, lakini wanataka kuwa na pesa za kunywa pombe saa zote, kuendesha magari na mambo mengi ya anasa, wamezoea kupata pesa nyingi kwa kufanya ufisadi, pesa zinapobanwa kidogo wanapiga makelele kwamba hali ya uchumi ni mbaya,” alisema Askofu huyo. 

Alibainisha kuwa, enzi za uhai wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, uchumi uliwahi kuyumba kiasi kwamba hali ilikuwa mbaya ambapo hata sukari ilikuwa kwa foleni na ikipatikana wiki hadi wiki lakini mambo baadaye yalikuwa mazuri hadi sasa. 

Awali, akitoa taarifa ya mradi huo wa ujenzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ya Kanisa hilo, Jackson Philemon alisema Sh milioni 95.3 zinahitajika kukamilisha ujenzi na kwamba hadi Sh milioni 20.6 zimetumika na ujenzi umefikia usawa wa renta. 

Katika harambee iliyoendeshwa na Askofu Mkuu huyo wa TAG ambaye alichangia Sh milioni 10, Sh milioni 27.6 zilipatikana na kati ya hizo, Sh 737,550 zikiwa fedha taslimu.


CHANZO:HABARI LEO

No comments: