ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 7, 2011

Hakuna asiyesalitiwa na mpenzi wake, muhimu ni kuaminiana tu!

Mapenzi ni miongoni mwa vitu vinavyoweza kumfanya binadamu akaishi kwa furaha lakini kwa upande mwingine, mapenzi haya haya ndiyo yamekuwa yakiwaliza watu na kuwafanya wajute kupenda.
Wapo waliokufa kwa sababu ya mapenzi, wapo ambao hawataki kusikia kitu kupenda kwa sababu ya namna ambavyo mapenzi yamewatenda.

Ndiyo maana nimekuwa nikisema, mapenzi usipoyapatia ni sumu.
Hata hivyo, mapenzi ya siku hizi hayana uhalisia, usanii umekuwa mwingi. Matapeli wa mapenzi wamezagaa kila kona kiasi kwamba, mtu anaweza kukwambia anakupenda kwa dhati lakini kumbe ni porojo tu. Hakupendi ila kilichomo moyoni mwake ni kukutamani tu kingono.


Ndiyo maana kuna ambao walipoingia katika mapenzi walidhani wanaingia katika uwanja wa furaha lakini wapo walioishia kuvuliwa nguo na kuachwa huku wengine wakiendelea kuwa katika uhusiano lakini kutoa machozi imekuwa siyo ishu kwao kutokana na namna wanavyosalitiwa.

Hili la wapenzi kusalitiana ni tatizo kubwa sana katika maisha ya sasa ya kimapenzi. Kusalitiana kumekuwa kukiongezeka kila kukicha na ndiyo maana haipiti siku utasikia fulani kafumaniwa na mume wa mtu, jamaa fulani kanaswa akiwa na mke wa mtu.

Mazingira haya yanamfanya kila anayeingia katika uhusiano kuhisi anajiingiza katika matatizo kwa kuwa anajua kusalitiwa na mpenzi wake ni kitu kinachoweza kutokea wakati wowote.

Leo hii hakuna anayeweza kusimama na kujidai kuwa, mpenzi wake katulia na anamwamini kwa asilimia zote. Kila mmoja ukimuuliza atakwambia anahisi anasalitiwa, anahisi penzi lake linamegwa.

Kama ni mwanamke ukimuuliza kwa nini anahisi hivyo, atakwambia wanaume siku hizi hawaaminiki kwa kuwa amekuwa akiona kwa macho yake wenzake wakisalitiwa.

Hakika kuaminiana kwa kiwango kinachotakiwa hakuna tena na hata akijitokeza mtu na kusema anamwamini mpenzi wake, siyo maneno ya kutoka moyoni mwake bali atakuwa anajifurahisha tu. Yaani watu wanaishi ili mradi siku zinakwenda huku kila mmoja akimwinda mwenzake.  

Katika hili naomba niseme kwamba, uaminifu ni kitu cha msingi sana kwa wanandoa na hata wapenzi wa kawaida. Unaposhidwa kumwamini mwenza wako mara nyingi sana utakuwa ukidhani kwamba anakusaliti kwa kuwa na mtu mwingine hata kama unavyodhani vinaweza vikakosa ukweli ndani yake hali inayoweza kulikwamisha penzi lenu lisinoge.

Penzi haliwezi kunoga kwa kuwa, kushindwa kuwa na imani na mtu unayempenda kunaweza kukufanya ukakosa raha kila anapokuwa mbali na wewe.

Si kukosa raha tu anapotoka ama anapokuwa mbali na upeo wa macho yako bali pia anaporudi huwezi kuonesha upendo wako kwake na kuweza kujenga chuki dhidi yake.

Niseme tu kwamba, amini kwamba mwenza wako ni mwaminifu kwako na jijengee mazingira ambayo na yeye ataamini kwamba wewe ni mwaminifu kwake.

Mwamini ili naye akuamini. Ili muweze kuishi kwa amani na furaha, epuka sana kufanya mambo ambayo yanaweza kumsababishia mpenzi wako akahisi unamsaliti.

No comments: