ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 7, 2011

Zitto apasua mawaziri

  Wanampuuza Mkaguzi Mkuu wa Serikali
  John Cheyo naye alia na Maliasili na Utalii
  Mrema ashangaa injector pump ya milioni 15/-
Mbunge wa Kigoma, Zotto Kabwe

Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, imelia na mawaziri kukiuka utawala bora na kuwateua wabunge kuwa wajumbe wa bodi za mashirika ya umma.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe, alisema hayo bungeni jana wakati akiwasilisha ripoti ya kamati yake kuwa uteuzi huo unaofanywa na mawaziri ni kikwazo cha uwajibikaji katika mashirika ya umma.

Alisema kwa kuzingatia dhana ya utawala bora na misingi ya uhuru wa Bunge kama muhimili wa kuisimamia serikali ni vema wabunge wakawa huru nje ya bodiza nashirika ya umma.


Alisema wabunge wasipoteuliwa kuwa wajumbe wa bodi hizo wataweza kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kwa ukamilifu zaidi.

“Kamati inampongeza kwa dhati Gavana wa Benki Kuu wa kutoa mwongozo wa kuwaondoa wabunge kuwa wajumbe wa bodi za taasisi za fedha hapa nchini,” alisema.

Alisema ni jambo la kusikitisha kuona kwamba mamlaka mbalimbali za uteuzi zimeendelea kuteua wabunge kuwepo kwenye bodi za mashirika umma, ambapo baadhi ya mashirika kama Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Umma (PSPF), yana wabunge kama wajumbe wa bodi.

“Kitendo cha mawaziri kuendelea kuwateua wabunge kuwa wajumbe ni dharau kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali,” alisema na kuongeza kuwa uamuzi wa kuwaondoa wabunge kuwa wajumbe wa bodi lilipitishwa bungeni miaka mitatu iliyopita.

Alisema kamati yake itatoa orodha ya wabunge wote ambao wameteuliwa kuwa wajumbe wa bodi na inawashauri wajiondoe wenyewe.

Akichangia baada ya kusomwa kwa taarifa hiyo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), alipinga hoja hiyo kwa madai kuwa uteuzi wa wabunge kwenye bodi hizo unachangia kuleta ufanisi.

“Mashirika yale ambayo yana wabunge yanafanya kazi vizuri kuliko kama yakiachiwa wajumbe waliostaafu tu...kupinga uteuzi wa wabunge kuwa wajumbe wa bodi ni nongwa tu, tunaweza kuwa na uteuzi mzuri zaidi, hata kama ni mbunge wa CUF au wa Chadema anaweza kuteuliwa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Zitto alisema Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN) Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Kudhibiti Mawasiliano (TCRA), ni miongoni mwa mashirika ambayo yamepoteza fedha nyingi kwa kutozingatia sheria katika manunuzi ya umma.

Zitto alisema miongoni mwa sehemu ambazo kiasi kikubwa cha fedha za umma zinapotea ni katika suala la zima la manunuzi.

“Kusipokuwa na udhibiti wa kutosha, eneo hili litaendelea kupoteza fedha nyingi za umma na kwa muda mrefu hubainishwa kama chanzo kikubwa cha sifa mbaya ya matumizi mabaya ya fedha za umma katika mashirika na serikali kwa ujumla,” alisema na kuongeza:

“Ni ushauri wa kamati kwamba sheria na zote za manunuzi zinapaswa kuzingatiwa.”

Alisema kwa mfano, ununuzi wa magari yaliyokwisha kutumika uliofanywa na TSN kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004, ikiwamo ununuzi wa gari aina ya Noah kwa gharama ya Sh. milioni 30 bei isiyokuwa halisi kwa soko hivyo kulinyima shirika thamani ya fedha iliyolipwa.

Kwa upande wa TPA alisema ilifanya manunuzi ya magari bila kufuata sheria ya manunuzi na hivyo kutumia Sh. 102,285,441.

Alisema TCRA iliingia zabuni ya kupitia muundo wa ofisi, tathmini ya utendaji kazi na kupitia ngazi za mishahara, thamani ya kazi na ngazi za utumishi ambayo awali ilitangazwa Agosti 16, 17, na 20, 2007 na kuingia mkataba Januari 28, 2008 kinyume na mapendekezo ya Kamati ya Tathmini.

PAC YAIBANA MALIASILI
Wizara ya Maliasili na Utalii imebainika kuwa na tatizo kubwa la uwajibikaji katika kufuatilia maduhuli yatokanayo na vyanzo mbalimbali vikiwemo vitalu vya uwindaji na leseni za kuendesha biashara ya uwindaji wa kitalii, wakati iliyokuwa Wizara ya Miundombinu sasa Ujenzi, ilikabiliwa na udhaifu katika makusanyo ya maduhuli.
Akiwasilisha ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) bungeni jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, John Cheyo, alisema fedha nyingi za utalii zinalipwa nje ya nchi na fedha za matumizi madogo ndiyo zinalipwa ndani.

Alisema taarifa ya ukaguzi ilionyesha kuwa yapo baadhi ya makampuni ya kitalii ambayo yamekuwa yakifanya kazi bila leseni na hivyo kuikosesha serikali mapato.

Alisema msako uliofanywa na Idara ya Utalii ulibaini makampuni 23 yaliyokuwa yakifanya kazi bila leseni.

“Kwa kuwa makampuni haya ya utalii hulipa ada ya leseni, kutosajiliwa maana yake ni kukwepa kulipa ada ... mamlaka husika ni lazima zifuatilie mara kwa mara vyanzo vyake vyote vya mapato ili kuhakikishi kuwa mapato yote stahili yanalipwa,” alisema.

Kuhusu Wizara ya Miundombinu (Ujenzi), Cheyo alisema, imeonyesha udhaifu katika makusanyo yake ya maduhuli ambapo taarifa inaonyesha kuwa kwa kipindi kinachoishia Juni 30, 2009 kiasi cha Sh. 61,039,560 kilikusanywa ikilinganishwa na makisio yaliyoidhinishwa ya Sh. 100,078,000.

“Kwa ujumla kamati yangu imeona udhaifu mkubwa wa kubuni na kutumia vyanzo vya mapato katika maeneo mbalimbali, hasa yale ambayo si makusanyo yatokanayo na kodi...upo ulazima wa serikali kujipanga vilivyo kukabiliana na changamoto hii,” alisema.

Alisema kwa mfano, mapato yatokanayo na mauzo ya hisa kwa makampuni yaliyomo nchini na yameuzwa nje ya nchi kama vile Bulyanhulu Gold Mine ya Barrick kuuzwa kwa kampuni mpya ya Barrick Africa, Zain kuuzwa kwa Airtel na karibuni Vodacom kununuliwa na Vodafone UK.

Kuhusu eneo la mizani, alisema kumekuwa na udanganyifu wa watumishi juu ya kiasi halisi kinachokusanywa na ucheleweshaji wa magari kwa uzembe ili mtu atoe rushwa.

Alisema kamati yake imeagiza mizani ziangaliwe kwa makini ili barabara ziwe salama na ucheleweshaji wa magari kwa makusudi usiwe kero ya kudumu.

Kwa upande wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), alisema kamati imependekeza kuanzishwa kwa kodi ya elimu na pia kuweka viwango maalum vya wanaostahili kupata mikopo ya elimu ya juu ili suala la mikopo liwe endelevu.

Akizungumzia malipo hewa, Cheyo alisema kumekuwepo na malipo kadhaa ya fedha kwa watu ambao wamefariki, wamestaafu ama wamefukuza kazi.
Alisema kamati inasisitiza kuwa maafisa masuuli wa kila fungu wawe wa kwanza kuondokana na tatizo hili.

Wakati huo huo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa, imeishauri serikali kutafuta teknolojia maalum ya kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma yanayotokea kupitia manunuzi ya mafuta na vipuri vya magari.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Augustino Mrema, alisema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya kamati yake bungeni jana.

Alisema kamati yake imebaini kwamba manunuzi ya aina hii hutumiwa kama mwanya wa kupotezea fedha nyingi za miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema kwa mfano, katika mwaka wa fedha wa 2008/2009, kwa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza ilifanya matengenezo ya pikipiki STK 3746 kwa Sh. milioni 2.9, Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ilinunua injector pump ya gari Toyota Land Cruiser Hardtop kwa gharama ya Sh. milioni 15 ambayo bei ya wastani katika soko ni Sh. 3,000,000.
CHANZO: NIPASHE

No comments: