ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 7, 2011

Mbunge augua ghafla bungeni

Mbunge wa Uzini, Muhammed Seif Khatib, akiwa amebebwa kwenye machela akiingizwa kwenye gari la kubeba wagonjwa kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma jana asubuhi. (Picha: Khalfan Said)
Aliyewahi  kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), ambaye pia ni Mbunge wa Uzini, Muhamed Seilf Khatib (CCM), ameugua ghafla na kupumzishwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema Khatib akiwa katika viwanja vya Bunge jana mchana alianza kujisikia vibaya na kusaidiwa na watu waliokuwa karibu ambao waliompeleka katika zahanati.

Alisema baadaye mbunge huyo alipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

Alisema kuwa Khatib alijisikia vibaya baada ya presha kushuka.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Godfrey Mtey, alithibitisha kupokelewa kwa mgonjwa huyo na kwamba hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.

“Hakuanguka bali alianza kujisikia kuchoka na kujipeleka mwenyewe katika zahanati ya Bunge na sisi huwa hatupuuzi kitu tukaamua kumpumzisha ili aweze kufanyiwa uchunguzi,” alisema na kuongoza:

“Anaendelea vizuri hakuna haja ya kuwa na wasiwasi bado tunamuangalia afya yake.”

Alisema mbunge huyo alipelekwa katika hospitali hiyo jana saa 7.00 mchana na kwamba hali yake ilikuwa inaendelea vizuri.

Hata hivyo, waandishi wa habari hawakuruhusiwa kwenda kumuona baada kuelezwa kuwa alikuwa akihitaji mapumziko.
CHANZO: NIPASHE

No comments: