Vyama vya Siasa vyenye wabunge vimewataka Watanzania kushikamana na kukataa kuruhusu ajenda ya mchakato wa kuandika Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uendeshwe na Serikali.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti mpya wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia. TCD inaundwa na vyama sita vya siasa vyenye uwakilishi bungeni ambavyo ni CCM, Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi, UDP na TLP.
Mbatia alisema ajenda hiyo ilianzishwa na wananchi wenyewe na kwamba wasikubali Serikali iichukue na kuifanya yake.
Mbatia alichaguliwa katika uchaguzi wa jana.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti aliyemaliza muda wake kutoka Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, alisema TCD inasaidia kupunguza misuguano ndani ya vyama vya siasa nchini.
Dk. Slaa alisema katika kipindi cha uongozi wa Chadema kuna mambo mengi yalifanyika katika kuhakikisha demokrasia inaendelezwa na kwamba kama kulikuwa na mapungufu wanachama hawana budi kuyaacha na kuchukua mazuri.
Naye Mwenyekiti mpya wa TCD, Profesa Ibrahim Lipumba alisema misingi ya demokrasia nchini bado inahitajika.
MTIKILA: RAIS ASIPEWE MAMLAKA
Naye Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amesema suala la Rais kupewa mamlaka ya kuunda tume ya kusimamia mchakato wa uundwaji wa katiba mpya halikubaliki.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, alisema suala la katiba liko mikononi mwa Watanzania wenyewe ambao ndio wahusika wakuu.
“Tunataka busara itumike hapa, suala la katiba linawahusu watanzania wenyewe tunashangaa kuona eti Rais ndio anapewa mamlaka makubwa ya kusimamia mchakato wa katiba huku wale wanaohusika hawapewi fursa hiyo, hii siyo haki na hatuwezi kulifumbia macho,” alisema.
Aliongeza: “ Inashangaza sana ina maana Rais anataka kuwaundia wananchi tume ya kuunda katiba yao pasipo wao wenyewe kuhusika? huu ni ukandamizaji na pia ni kuwanyima uhuru wao.”
Alisema suala la katiba mpya linatakiwa kuwahusisha Watanzania wote kutoka katika kila sekta ili waweze kutoa maoni yao kulingana na wanavyohitaji.
Mtikila alishauri kuitisha kongamano la kitaifa la katiba kwa ajili ya kupata maoni ya wadau mbalimbali kutoka katika kila mkoa.
CHIPAKA: WANANCHI WASIKILIZWE
Chama cha Tanzania Democratic Alliance Party (Tadea), kimeiomba serikali kuwashirikisha wananchi kuchangia na kutoa maoni juu ya uundwaji wa katiba mpya.
Akizungumza na aandishi wa habari jana, Rais wa Tadea, Lifa Chipaka, alisema njia nzuri ya kupata katiba bora ni kuwashirikisha wananchi na wadau mbalimbali ili waweze kutoa maoni na hata kwa kupiga kura ya ndio au hapana.
Alisema katika kupata katiba mpya ni vizuri kuwashirikisha wasomi, wanataaluma, taasisi za dini taasisi zisizo za kiserikali, wafanyakazi, walemavu na vyama vya siasa.
Imeandikwa na Richard Makore, Elizabeth Zaya na Elisante William.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment