ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 7, 2011

Misingi ya Karume imejenga Zanzibar imara

IKIWA imepita miaka 39 tangu Abeid Amaan Karume alipotutoka, lakini misingi yake ingali imara. 

Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla tunamkumbuka kiongozi huyo kwa mambo mengi ya kujitolea wakati wa uhai wake. 

Tunaukumbuka mchango wake wakati wa ukombozi wa visiwa vya Zanzibar kupitia Mapinduzi ya Januari 12, 1964. 


Tunamkumbuka kwa ushiriki wake mkubwa katika mipango madhubuti na misingi imara ya maendeleo visiwani humo. 

Ni mmoja kati ya watawala katika nchi za Kiafrika aliyekuwa na mikakati ya kuleta tija kwa wananchi wake. 

Jambo linaodhihirisha hayo ni kwamba ni kiongozi aliyejitolea kwa dhati kuwatumikia watu, kwani mara tu baada ya kufanikisha mapinduzi, alitangaza rasmi kurejesha rasilimali nyingi za kisiwa hicho kwa wananchi wenyewe. 

Ni ukweli usiopingika kuwa siku chache baada ya kufanikisha mapinduzi hayo, Wazanzibari walianza kuona matunda ya uongozi wake ndani ya muda mfupi kwani watu wengi wengi waliweza kumilikishwa ardhi na wengine kurudishiwa mashamba na nyumba zao ambazo hapo awali zilikuwa chini ya utawala wa Sultani. 

Katika harakati za kupanua zaidi wigo wa maendeleo ya visiwa hivyo, miezi mitatu tu baada ya mapinduzi hayo Karume kwa kushirikiana na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere waliasisi Muungano wa nchi hizo na kuzaliwa kwa taifa la Tanzania. 
Lengo la Muungano huo pamoja na mambo mengine ,lilikuwa ni kuunganisha nguvu za Watanganyika na Wazanzibari ili kuleta maendeleo ya haraka pamoja. Jambo hilo lilifanyika kufuatia falsafa ya 'Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu'. 

Karume anakumbukwa kama kiongozi aliyekuwa na mikakati mingi ya maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kwani alikuwa mstari wa mbele kutafuta ufumbuzi wa matatizo sugu na changamoto za maendeleo zilizokuwa zikiwakabili Wazanzibari. 

Baadhi ya maeneo ya vipaumbele aliyoyashughulikia haraka ni pamoja na uhaba mkubwa wa hospitali, shule, ubovu wa miundombinu. 

Pia alishughulikia changamoto zilizokuwa zikiikabili sekta ya ufugaji ambapo kisiwa hicho kama vilivyokuwa vingine vya Comoro na Madagascar kilikuwa kikikabiliwa na uhaba mkubwa wa mifugo. 

Wakazi wengi wa visiwa hivyo hawakuwa na mazao ya mifugo kama nyama, maziwa na faida nyingine, hivyo sehemu kubwa ya uchumi wao ilitegemea zaidi kilimo cha zao la karafuu. 

Kwa kutambua changamoto hiyo na nyingine nyingi zilizokuwa zikikabili uchumi wa Zanzibar, Karume aliamua kusimamia yeye mwenyewe badala ya kutegemea taarifa za wasaidizi wake ndiyo maana alifanikiwa kuacha misingi imara kiasi ya kuboresha uchumi na maisha ya Wazanzibari kwa ujumla. 

Misingi hiyo ilisaidia sana kujenga taswira ya maendeleo visiwani humo katika watawala waliofuatia kama vile, Aboud Jumbe Mwinyi, Salmin Amour 
na wengine waliofuatia. 

Katika utawala wake shule kisiwani Zanzibar ziliongezeka kwa kasi, ujenzi wa barabara kuu, hospitali na makazi ya watu vilianza kujengwa kwa kasi. 

Mkakati mwingine uliofungua njia ya kutatua tatizo la uhaba wa mifugo ni pamoja na kuanzisha Ranchi ya Zanzibar nje ya mji wa Bagamoyo mkoani Pwani. 

Ranchi hiyo ilikuwa ikizalisha mifugo hadi kuzidi mahitaji ya matumizi ya kisiwa cha Zanzibar na Pemba na ziada yake kuuzwa nje ya nchi. 

Historia inaonesha kuwa mafanikio ya Karume yalitokana na roho ya kujituma, uzalendo na kuwajali wengine. 

Miongoni mwa mambo aliyoyachukia Karume ni tabia ya baadhi ya watu kutumia nyadhifa zao na kujilimbikizia mali, ilihali wakiwaacha raia wengine wakibaki masikini. Alichukia kuona wananchi wasiokuwa na kauli katika nchi yao kwa sababu ya umasikini wao. 

Karume alionekana kufuata na kuamini falsafa za kijamaa kwani mara kadhaa alikuwa mkali na anayechukua hatua za haraka kwa watu waliokuwa wakijaribu kujilimbikizia mali na kuwaacha wenzao wakitaabika kwa umasikini. 

Mara kadhaa alikuwa akiwaonya viongozi ambao walipewa dhamana ya kuongoza serikali, vyama au taasisi kwa ajili ya kuhudumia umma, lakini waligeuka viapo vyao na kudidimiza uchumi wa nchi. 

Karume anatakumbukwa kwa hekima alizokuwa nazo zilizopelekea Wazanzibar i kuondoa tofauti zao na kuweza kufuta vyama vidogovidogo kama ZNP, ZPP na hatimaye kuunda chama cha Afro Shirazi Party (ASP), kikiwa na nguvu kiasi cha kufanikiwa kuleta mapinduzi ya kweli. 

Kutokana na jitihada zake, Wazanzibari leo hii wanaweza kusimama na wenzao wa Tanzania Bara na kujadili mafanikio au kero lakini wakiwa wenye amani kutokana na misingi imara ya amani, utulivu na mshikamano iliyojengwa na kiongozi huyo. 

Wana uwezo wa kuanzisha na kuendesha vyama vya siasa kila kona ya nchi, lakini yote hayo ni mafanikio ya misingi iliyowekwa na watawala wetu wa awali waliofanikisha kupata uhuru na hatimaye kuwa na taifa madhubuti lenye watu thabiti. 

Pamoja na juhudi hizo za kuleta maendeleo ya Zanzibar, Karume pia alijitahidi kusimamia maadili ya nchi hiyo ambayo kihistoria ilikuwa imejikita zaidi katika maadili ya dini ya Kiislamu hali ambayo kwa sasa imeanza kupoteza sura hiyo. 

Ni jambo lililo wazi kuwa kwa miaka mingi, licha ya utandawazi kuathiri mila na desturi za mataifa ya Afrika, Zanzibar ni miongoni mwa nchi zilizofanikiwa kwa kiasi kikubwa kusimamia maadili katika jamii na kuhifadhi tamaduni zake ambazo zilitokana na tamaduni za Kiarabu. 

Licha ya kwamba mafanikio hayo yametokana na jitihada za Wazanzibari wote, ukweli unabaki palepale kuwa mwenendo wa maadili ya wananchi katika taifa fulani unaweza kubadilika haraka kama serikali haipo makini katika kufuatilia, kulinda na kuhifadhi mila na desturi zake. 

Msimamo wa utawala wa Karume wa kuwatambulisha Wazanzibari kwa tamaduni zao ndio ulioleta mafanikio katika suala zima la maadili na kuitofautisha Zanzibar na nchini nyingine ambazo zimekuwa na tamaduni zinazolegalega.


chanzo:Habari Leo

No comments: