Joto la mji wa Moshi limefikia wastani wa joto la jangwani, jambo ambalo linahitaji jitihada za kila mwananchi katika kukabiliana nalo kwani ni tishio kwa uhai wa binadamu na vizazi vijavyo.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Alhaj Mussa Samizi, aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya wiki moja ya uhamasishaji uoteshaji miti kwa wakazi wa Manispaa hiyo, ambapo aliongoza zoezi la kupanda miti katika Kata za Bomambuzi na Soweto.
Alisema joto la Moshi miaka 20 iliyopita lilikuwa kati ya nyuzijoto 20c na 29c, lakini kwa sasa na hasa wakati wa kiangazi limeongezeka na kufikia kati ya nyuzijoto 20c hadi 40c na wakati mwingine kufikia nyuzi joto 50c na kufanya mji huo kuwa na joto jingi ukilinganisha na miji mingine nchini.
Samizi alisema ongezeko la joto limekuwa dhahiri na Mlima Kilimanjaro unaendelea kupoteza theluji yote kileleni ambapo wataalam wanasema kuwa ifikapo 2020, theluji yote itakuwa imeyeyuka.
“Tusipochukua hatua kwa kupanda miti kwa wingi, tunaweza kutoweka kama watu watakaokutwa kwenye kisiwa kwani vitadidimizwa na kufutika baada ya barafu iliyoko nchi za baridi kuyeyuka, hii ni dhahiri kwani hapo kale vipo visiwa na nchi zilizozamishwa na wao wataalam wanaozamia baharini kwenda kuona visiwa hivyo vikiwa na majengo lakini hakuna tena uhai wa binadamu,”alisema.
Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa wakazi wa Moshi wanasababu zote za kufutika duniani iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa katika kupunguza hatari za kutoweka kwa theluji ya mlima na inawezekana upo kwenye matayarisho ya kulipuka tena au kuongezeka kuharibika kwa uoto wa ozoni kulikosababishwa na viwanda vya nchi za Marekani na Ulaya.
Alisema kuotesha miti wakati wa mvua ni suala muhimu katika maisha ya sasa na vizazi vijavyo na serikali tayari ilishatoa agizo la kuoteshamiti kila mwaka jumla milion 1.5 kwa kila halmashauri na kuhakikisha inaota, inakua na kulindwa.
Awali, akimkaribisha mkuu wa wilaya kuzungumza na wakazi wa Bomambuzi, Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Bernadetta Kinabo, alisema manispaa hiyo inakadiriwa kuwa na zaidi ya wakazi 210,000 na kila mkazi anatakiwa kuotesha miti minane katika eneo lake, hospitali, zahanati, shule na taasisi nyingine ili kufikia jumla ya miti milion 1.5.
Alisema iwapo theluji ya Mlima Kilimanjaro itayeyuka, waathirika wa kwanza ni wakazi wa Bonde la Pangani ambao wanategemea bonde hilo kwa shughuli mbalimbali za uzalishaji ikiwemo kilimo cha umwagiliaji.
Alisema miti iliyooteshwa hadi sasa ni mijakaranda ya zambarau na Mikrismasi ambayo ni miti ya asili na inatakiwa kupandwa kwa wingi na si miti aina ya mijohoro ambayo matunda yake yanaua nyuki na hivyo kuchangia katika uharibifu wa mazingira.
Naye Naibu Meya wa Manispaa hiyo, Vincent Rimoi, alisema ni vyema
wananchi wakatumia mvua hizi kuotesha miti katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na miti inayotolewa bure na manispaa hiyo kuoteshwa kwa wingi ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment