ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 15, 2011

Nani amekudanganya wewe ni mbaya, huvutii?-2

NISEME nini kama sitamshukuru Mungu wangu wa mbinguni kwa wema wake na kunifanya niendelee kupumua? Hakika kama si yeye, nisingekuwa nilivyo leo. Narudisha sifa, heshima na utukufu kwake aliye juu. Naam! Marafiki zangu, karibuni sana katika kona yetu ya kujadiliana juu ya maisha yetu ya kimapenzi.

Mada iliyopo mezani ni kama inavyoonekana hapo juu, leo ikiwa ni sehemu ya pili. Nazungumza na rafiki zangu ambao kwa namna moja ama nyingine wametoka katika uhusiano na wapenzi wao, fikra zao zikiwa ni kuamini kwamba hawavutii!


Pia, wapo marafiki zangu wengine ambao hawapo katika uhusiano na pengine kwa muda mrefu sana wanatamani kupata wenzi wao lakini jambo hilo halijatokea, sasa kilichofuata vichwani mwao ni kuamini kwamba yawezekana ni kwa sababu  hawana mvuto! Fikra hizi zipo sawa?

Kwa hakika ni potofu kabisa, katika maandishi ya mada hii, utapata ukweli halisi wa kile unachokiamini kama kipo sawa au unajidanganya! Kama mtakumbuka vyema, wiki iliyopita nilianza kwa kueleza juu ya wale ambao wanaamini kwamba hawavutii, dhana ambayo nilipingana nayo vikali kwa hoja zenye nguvu.

Pia nilitoa maelekezo kwamba, kitu cha kwanza kabisa kufanya kama wewe unahisi una tatizo ninalolizungumzia hapa ni kuamini kwamba hakuna mzuri, mwenye mvuto kama wewe. Sasa leo tunaendelea na vipengele vingine.?

WEWE NI ZAIDI YA ULIVYO...
Katika kujisogeza kwenda kundi la wanaovutia, lazima wewe uanze kujitazama katika mtazamo mpya. Kama unadhani, urefu wako hauwavutii wanawake wengi, ndiyo maana wanakutosa, fikiria juu ya wacheza kikapu maarufu duniani ambao ni warefu kuliko wewe na wanafurahia mapenzi na wenzi wao.

Kama unawaza kwamba wanaume wengi wanachukia ufupi wako, watazame wanawake wafupi waliopo duniani na wanafurahia mapenzi na wanaume zao. Fanya zoezi moja jepesi, simama mbele ya kioo, ukiwa peke yako, halafu angalia mtu anayeonekana ndani ya kioo hicho. Ni nani? Anaonekanaje?

Bila shaka ukitazama kioo ukiwa umesimama nyuma yake, atakayeonekana ndani ya kioo hicho ni wewe mwenyewe! Sasa unachotakiwa kufanya ni kusogea hatua moja mbele kimawazo, toa sura yako katika kioo hicho, halafu muweke mwanamke/mwanamke mzuri ambaye unadhani anavutia sana, fanya ndiyo wewe.

“Unatakiwa ukijiangalia kwenye kioo, usione sura yako, badala yake uone sura ya simba ikiwa inakuangalia, hapo lazima utakuwa na ujasiri mkubwa katika kukabiliana na tatizo lililopo mbele yako,” Mwanasaikolojia  Julius P.J wa Uingereza, anaeleza katika mtandao wake, alipokuwa akichambua mada ya ‘Jinsi ya kujenga uwezo wa kujiamini’.  

CHUNGA ULIMI WAKO
Kuna wanawake wazuri sana wanaovutia kwa sura lakini wanashindwa kudumu na wenzi wao, baada ya hayo kutokea, wanakimbilia kuwaza kwamba hawana mvuto, kadhalika wanaume nao.

Rafiki yangu mpenzi, ulimi wako unaweza kuwa chanzo cha wewe kuonekana mbaya, kukimbiwa na kutengwa. Kuna wanawake wana maneno makali sana, mpenzi wake amekosea kidogo tu, anaanza kushusha mzigo wa lawama ambao hauna maana yoyote.

Mwingine anakuwa mtu wa matusi kila wakati, hana lugha nzuri wakati anazungumza na mpenzi wake, hakuna mtu ambaye anapenda kuwa na mpenzi wa aina yako. Hivyo basi, kama una tabia hiyo, tarajia kupata matatizo kila kukicha katika maisha yako.

Hakuna mtu anayependa kuwa na mtu mkorofi, ambaye atampa mawazo badala ya furaha, kila siku awe analia kwa ajili yako. Hakuna mtu wa aina hiyo. Kama umeshindwa kubadilika, lazima utakimbiwa na hapo dhana ya kuwa wewe ni mbaya, huvutii itaendelea kukusumbua kichwani mwako.

MAVAZI YAKO NI SILAHA
Inawezekana haupo katika uhusiano na huko nyuma haukuwa katika uhusiano kwa muda mrefu, sababu ambayo inakufanya uamini kabisa kwamba huna mvuto. Hapo unapotoka. Angalia upya kuhusu mavazi yako, unavaaje?

Kama huna mpangilio mzuri wa mavazi hakuna atakayeona utanashati/urembo wako. Kwani kuvaa vizuri kunaficha mapungufu madogo madogo ya kibinadamu uliyonayo. Jitahidi kuvaa vizuri wakati wote, hasa unapokuwa mbele ya watu. Hiyo itakujengea kujiamini na kuongeza umaridadi wako, hapo lazima hiyo dhana ya kwamba wewe huvutii inayokutawala kichwani mwako itaondoka.  

ZINGATIA USAFI
Kipengele hiki hakipishani sana na kilichopita, baada ya kuboresha mavazi yako, sasa unapaswa kuzingatia usafi, hii ni silaha yako nyingine ambayo kiukweli ina nguvu sana. Usafi unaanzia katika mwili wako, lazima uhakikishe kwamba unakuwa msafi muda wote.

Mavazi yako yakiwa safi, nawe unavutia. Hupaswi kuishia hapo pekee, bali hata nyumba yako na eneo lako la kazi. Kwa hakika kama ukifuata niliyoelekeza hapo hisia zako mbaya juu yako zitafutika mara moja. Anza sasa! Kama unataka kujiunga nami katika ukurasa wa facebook, andika Joseph Shaluwa kisha nitakuunganisha.
Kwa leo naishia hapa, hadi wiki ijayo kwa mada nyingine. USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi ambaye anaandikia magazeti ya Global Publishers, kwa sasa ameandika vitabu vya True Love, Secret Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani. Unaweza kumtembelea kwenye mtandao wake; www.shaluwanew.blogspot.com

No comments: