ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 8, 2011

NIMR yabaini chanzo cha mbu wa Muhimbili

Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), imebaini chanzo cha mbu waliokuwa wakiwasumbua wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Julai na Agosti, mwaka jana.
NIMR imebaini hali hiyo baada ya kufanikiwa kukamata mbu zaidi ya 14,000 kwa muda wa siku tatu na kuwafanyia utafiti wa kina.

Aidha, katika uchunguzi huo wa mbu kuzagaa Hospitali ya Taifa Muhimbili, waligundua kuwa chanzo chake ni chemba za vyoo kuwa wazi na kwa bonde la Msimbazi walikuta matairi ya magari yakiwa yametupwa kwenye mfereji wa maji machafu unaopeleka maji yake baharini ambayo ndio yalikuwa chanzo cha mbu hao aina ya Culex Quinquefasciatus.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, mtafiti wa magonjwa ya binadamu kutoka NIMR, Dk. Leonard Mboera, alisema walifanya utafiti huo kwenye baadhi ya nyumba za wakazi wa Jangwani, Hospitali ya Muhimbili wadi ya Kibasila, Mwaisela na bonde la mto Msimbazi.
Alisema waligundua kuwa bonde la Jangwani kulikuwa na matairi mengi yaliyokuwa yametupwa kwenye mfereji unaopitisha maji machafu kwenda baharini na Hospitali ya Muhimbili walikuta matundu 136 yakiwa wazi katika wodi ya Kibasilia, Sewa Haji na Mwaisela na asilimia 67 ya mashimo ya maji machafu hospitalini hapo yalikuwa matundu ambayo hayana mifuniko.
Alisema mbu waliokuwa wanasumbua wagonjwa ambao walikuwa wanalala kwenye vyandarua pamoja na watu mbalimbali waliokuwa wakifika hospitalini hapo na kufikiria labda mbu hao walikuwa wametoka nje ya nchi.
"Mbu waliokuwa wakisumbua wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, wametoka hapo," alisisitiza.
Aidha, alisema baada ya utafiti huo wamegundua kuwa miundombinu ya Jiji la Dar ni mibovu na ndiyo inayosababisha mazalia ya mbu na kwa mujibu wa utafiti wao waligundua kuwa hakuna mbu hata mmoja kati ya hao waliowakamata aliyekuwa akiambukiza magonjwa.
Alisema asilimia moja ya mbu hao hawaambukizi magonjwa yoyote na asilimai 99 wanaambukiza magonjwa ya mabusha na matende na kuongeza kuwa bonde la Msimbazi kuna mazalia mengi ya mbu kutokana na uchafu uliopo.
Dk, Mboera alisema Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni, Hospitali ya Taifa Muhimbili na wakazi wa bonde la Msimbazi, walishirikishwa kwa pamoja juu ya kuhifadhi mazingira na kuacha kutupa taka ovyo na Hospitali ya Muhimbili walifanya juhudi ya kufunika mashimo ya maji machafu ili mbu wasizaliane.
Aliiomba serikali kuwa na kitengo maalum kwa jili ya uchunguzi wa mbu, kwani baadhi ya mbu hueneza magonjwa mbalimbali kwa binadamu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: