ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 8, 2011

Yanga mkono mmoja kwenye kombe

Davies Mwape (kushoto) na Kigi Makasi (katikati) wakimpongeza mchezaji mwenzao wa Yanga, Iddi Mbaga baada ya kufunga goli la kwanza la Yanga dhidi African Lyon wakati wa mechi yao ya ligi kuu ya Bara
 Yanga jana ilisogea jirani zaidi na kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuifunga African Lyon 3-1 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na kukaa kileleni mwa msimamo kwa tofauti ya nzuri ya magoli dhidi ya watetezi Simba walio katika nafasi ya pili huku ikiwa imebaki mechi moja msimu kumalizika.
Simba waliokuwa na nafasi nzuri zaidi ya kutetea taji lao wakati zikiwa zimesalia mechi tatu, walipoteza pointi nne katika mechi dhidi ya Kagera Suger na JKT Ruvu, ambapo kote walinusurika vipigo na kukamilisha wiki mbaya ambayo pia walitolewa katika michuano ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika kwa jumla ya magoli 6-3 dhidi ya TP Mazembe.

Kwa ushindi wa jana, Yanga ambayo sasa imefikisha pointi 46 sawa na Simba, inaongoza ligi kwa tofauti ya magoli mawili zaidi ya Simba, kwa mujibu wa msimamo wa shirikisho la soka nchini (TFF).
Msimamo wa TFF ambao hauonyeshi magoli ya kufunga na kufungwa kwa timu hizo mbili, umeweka tofauti ya magoli ambayo imeshakokotolewa kutoka kwenye magoli ya kufunga kutoa ya kufungwa, ambapo kwa Yanga tofauti ya magoli yao inaonekana kuwa ni 22, wakati ya Simba ni 20.
Lakini kwa mujibu wa rekodi zilizowekwa na gazeti hili, ni kwamba hadi jana Yanga ilikuwa imefunga jumla ya magoli 29 na kufungwa 7, wakati Simba imefunga magoli 36 na kufungwa 15, jambo linalomaanisha tofauti ya magoli ya kufunga na kufungwa kwa Yanga ni 22, wakati kwa Simba ni 21.
Matokeo ya jana yanamaanisha kwamba bingwa ataamuliwa kwa ushindi mkubwa wa Yanga dhidi ya "ndugu zao" wa Toto African kwenye uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza ambao mwaka jana waliwashindilia magoli 6-0; Au wa Simba dhidi ya timu ambayo imeshashuka daraja ya Majimaji ambayo mmoja wa nyota wake ni winga Ulimboka Mwakingwe, ambaye mwaka jana alituhumiwa katika kashfa ya kutaka kumhonga kipa wa Mtibwa Sugar, Shaaban Kado kwa nia ya kuisaidia Simba ishinde. Hata hivyo, 'kesi' ya Ulimboka haikusikika ilikoishia.
Yanga walipata goli la kwanza jana kupitia kwa mshambuliaji Idd Mbaga katika dakika ya 32 baada ya kuwazidi mbio mabeki wawili wa Lyon na kumchagua kipa wa zamani wa klabu hiyo ya Jangwani, Ivo Mapunda, kwa kuupiga mpira upande aliotokea.
Dakika moja baada ya kipindi cha pili kuanza, Yanga waliandika bao la pili kupitia kwa mfungaji mwenye ukame wa muda mrefu wa magoli, Davis Mwape alipiga shuti kali la juu kutokea kwenye kona ya nje ya boksi la penalti lililokwenda kutinga ndani ya paa la nyavu. Lilikuwa ni bao la sita kwa Mzambia huyo aliyejiunga na Yanga kwenye "dirisha dogo" la usajili na kuanza kwa "mkwara" wa kufunga magoli matatu katika mechi yake ya kwanza na kisha kuongeza mwengine mawili katika mechi iliyofuata kabla ya "kupotea" hadi jana.
Mbaga, ambaye alianza kwenye kikosi cha kwanza kutokana na kutokuwepo kwa Jerryson Tegete aliyekuwa akitumikia adhabu ya kadi tatu za njano, alifunga goli lake la pili jioni ya jana na la tatu kwa timu yake katika dakika ya 61 na kuifanya Yanga ijiamini kwa uongozi wa magoli 3-0.
Beki asiye na namba ya kudumu kikosini Yanga, Chacha Marwa alipunguza goli moja wakati alipojifunga katika dakika 78 wakati akijaribu kuokoa krosi ya Benedict Ngassa aliyeuwahi mpira "mrefu" na kukimbia peke yake kwenye wingi kabla ya kupiga krosi hiyo.
Wakati huo huo, mapato ya mechi ya juzi ya mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kati ya Simba na JKT Ruvu iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam ni Sh. Milioni 21.1, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na TFF.

CHANZO: NIPASHE

No comments: